loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mionzi ya ‘microwave’ salama, tatizo sahani za plastiki

LICHA ya kuwa kifaa muhimu cha jikoni kwa miongo kadhaa, vitu vichache vya jikoni vimeelezwa kuwa na matatizo fulani kulinganisha ‘microwave’. Kifaa hiki kimekuwa mkombozi kwa wale wasioweza kupika na wapishi wengi katika hoteli mbalimbali wamekuwa wakikitegemea kwa kiwango kikubwa kwa kazi zao.

Hata hivyo, kumekuwa na mjadala mwingine kuhusu ni wapi microwave inakuwa na madhara kwa binadamu na wapi inakuwa salama. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kifaa hiki kinapotumiwa kwa usahihi, hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu suala la mionzi.

Pamoja na hayo, bado yapo mambo yanayotia wasiwasi miongoni mwa watafiti ambayo hayajatolewa ufafanuzi vyema. Haya ni pamoja na madai kwamba, chakula kinachopashwa kwenye microwave hupoteza virutubisho, au endapo ni kweli kwamba chakula kinachopashwa kwa kutumia plastiki kinaweza kusababisha madhara hususani kuvuruga homoni.

Kupoteza virutubisho Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa, mboga za majani zinazopashwa kwenye microwave hupoteza baadhi ya viini lishe vyake. Kwa mfano, katika utafiti mmoja, inadaiwa kwamba, microwave imeonekana kuondoa asilimia 97 ya kitu kinachoitwa ‘flavonoids’ kwenye mboga hususani aina ya braccoli. Kiwango hiki cha upotevu ni mara tatu zaidi ya kiwango cha upotevu unaotokea mboga hizo zinapochemshwa kawaida.

Viini lishe hivyo vina manufaa kadhaa mwilini, ikiwa ni pamoja kupunguza uwezekano wa mtu kuugua magonjwa ya moyo. Aidha, utafiti mwingine ulipingana na huo kwa kuonesha kwamba kuchemshia baadhi ya mboga kwenye microwave ni bora zaidi katika kupunguza upotevu wa flavonoids kuliko kuchemsha kwa kawaida.

Hata hivyo, utafiti huo ulionesha kwamba unapopasha mboga zikiwa na maji mengi kama unavyofanya katika kuchemsha kwa kawaida, ndipo flavonoids hupotea kwa wingi.

Hata hivyo, mtafiti mmoja kiongozi, Xianli Wu, mwanasayansi kutoka Kituo cha Utafiti Lishe ya Binadamu cha Beltsville katika Idara ya Kilimo ya Marekani, anasema hakuna makubaliano ya watafiti kuhusu kwa nini microwave inaweza kuwa na unafuu kuhusu flavonoid.

Halikadhalika anasema, hakuna jibu la moja kwa moja kama mboga iliyopashwa kwenye microwave itabaki na virutubisho zaidi kulinganisha na aina nyingine za upishi.

Hii ni kwa sababu kila chakula kiko tofauti na kingine kwa maana ya muundo wake na virutubishi vyake, kwa mujibu Wu. “Ingawa kwa jumla microwave ni njia inayopendelewa, namna nzuri ya kuitumia inategemea pia utofauti wa mboga,” Wu anasema.

“Wakati wa kuzingatia njia za kupikia za kawaida zinazotumika nyumbani, microwave ni njia bora ya kupikia, angalau kwa mbogamboga nyingi ingawa siyo zote zinafaa kupikiwa kwenye chombo hiki.”

Katika utafiti mwingine, watafiti walilinganisha upotevu wa phenolics (misombo inayohusishwa na faida mbalimbali za kiafya) za mbogamboga kadhaa baada ya kuchemshwa au kupashwa kwenye microwave.

Waligundua kwamba kifaa hicho hupoteza virutubisho kwa baadhi vyakula kama maboga, viazi na vitunguu, lakini siyo mchicha, spinachi, pilipili au maharage ya kijani.

“Utumiaji wa joto kidogo kwenye microwave unaweza kuwa jambo muhimu katika kuzifanya mboga zisipoteze virutubisho vingi,” watafiti wanaandika.

JOTO KWENYE SAHANI ZA PLASTIKI

Mara nyingi tunapasha vyakula vyenye microwave vikiwa kwenye vyombo vya plastiki au katarasi maalumu za kufungia vyakula, lakini wanasayansi wengi wanaonya juu ya hatari ya kumeza sumu inayoitwa phthalates.

Wanasema chombo cha plastiki kinapokuwa kwenye joto, sumu hii inayotumika kutengeneza vyombo hivyo huyeyuka na kuchanganyika ndani ya chakula.

“Baadhi ya plastiki hazijatengenezwa kwa ajili ya kutumika kwenye microwave kwa sababu zina kitu kinachoitwa polima (polymers) ndani mwake ambayo huyeyuka kwa joto hata la chini na inaweza kutoka kwenye chombo cha plastiki wakati wa kupasha chakula kwenye microwave na kuchanganyika na chakula,” anasema Juming Tang, Profesa wa uhandisi wa chakula katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Washington.

Katika utafiti uliofanywa mwaka 2011, watafiti walinunua vyombo zaidi ya 400 vya plastiki vilivyotengenezwa kwa ajili ya kuhifadhia chakula, na waligundua kuwa kemikali nyingi zinazoparaganyisha homoni ziliyeyuka.

Phthalates ni moja ya vitu vinavyotumika kutengeneza plastiki kwani ndiyo hufanya plastiki iwe laini zaidi na mara nyingi hutumika kutengeneza vyombo vya plastiki vya kubebea chakula (takeaway), chupa za maji na kadhakika.

Tafiti zimeonesha pia mtu anapoziingiza mwili huvuruga utendaji wa homoni na mfumo wetu wa uyeyushaji wa chakula. Kwa watoto, phthalates inaweza kuongeza shinikizo la damu na ukinzani wa insulini, hali inayoweza kuongeza hatari ya mwili kushindwa kuyeyusha chakula ipasavyo na hivyo kuleta hatari ya ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu.

Tatizo hili pia limehusishwa na masuala ya upungufu wa nguvu za kiume, utasa na pumu. “Phthalates pia zina uwezo wa kuvuruga homoni za tezi,” anasema Leonardo Trasande, Profesa wa dawa za mazingira katika Chuo cha Tiba cha New York.

Anasema homoni hizi pia ni muhimu kwa ukuaji wa ubongo wa watoto wakati mama anapokuwa mja uzito. Bidhaa iitwayo Bisphenol (BPA) pia hutumiwa katika kutengenezea plastiki, na tafiti zimeonesha pia kuwa zinaweza kuvuruga homoni.

Lakini utafiti kuhusu tatizo hilo bado mdogo, ikilinganishwa na kiasi cha tafiti zinazoangalia madhara ya phthalates. Njia bora za kupunguza hatari hizi ni kutumia vifaa vingine salama vya microwave kama sahani za udongo kuliko plastiki.

Ikiwa unatumia vyombo vya plastiki, epuka vile ambavyo hupoteza umbo/mwonekano wake kwa haraka. Pia unaweza kuangalia alama kwenye chombo chako. Mara nyingi chini ya chombo kunakuwa na namba 3 na herufi “V” au “PVC” hii huonesha kwamba chombo kina phthalates.

HATARI YA JOTO

Unaweza ukaepuka athari za plastiki, lakini kuna hatari nyingine ya kupasha chakula kwenye microwave ikiwa ni pamoja na chakula chote kutokuwa na joto sawa au kutumia joto la juu katika kupasha.

Mara nyingi fikiria kutumia microwave kwa ajili ya kupasha tu chakuka na siyo kupika hadi kiive. “Kulingana na aina ya chakula, kunaweza kuwa na sehemu ambazo zinapata joto sana kuliko nyingine,” anasema Francisco Diez-Gonzalez, profesa wa usalama wa chakula katika Chuo Kikuu cha Georgia.

Anasema chakula kilichopashwa muda mrefu kwa joto kali au chenye joto lisilolingana kina matatizo mengi mwilini ikiwa ni pamoja na kushindwa kuua bakteria kama hakikupashwa chote kwa usawa.

Joto kali hasa kwa vyakula vya nafaka huweza kusababisha kitu kinachoitwa acrylamide ambacho kinavuruga chembe hai za vinasaba (DNA) mwilini.

USALAMA WA MIONZI

Kuhusu mionzi inayotumika kwenye microwaves, wataalamu wanakubaliana kwamba haina madhara kabisa tofauti na dhana iliyokuwepo zamani.

Microwaves hutumia mionzi ya elektroni ya chini - aina ile ile inayotumika kwenye taa za umeme (bulb) na redio. Unapoweka chakula ndani ya microwave, hii mionzi hufanya molekuli za majimaji kwenye chakula kutetema, na kusababisha msuguano ambao unasababisha chakula kupata joto.

Makala haya yametafsiriwa na Hamisi Kibari kwa tafsiri isiyo rasmi kutoka Jarida la BBC la Julai 15 mwaka huu

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England 2020/2021 umeanza na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi