loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Watanzania wanaotumikishwa nje warudishwe-Simbachawene

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwabaini na kuwa na taarifa za Watanzania wanaotumikishwa nchi za nje, ili serikali iangalie namna ya kuwasaidia kurudi nyumbani.

Pia amesema serikali iko mbioni kuifanyia marekebisho Sheria ya Kuzuia Biashara haramu ya Usafirishaji wa Binadamu na kuweka adhabu kali kwa watu wanaojihusisha na biashara hiyo, katika kuongeza kasi ya uthibiti wa biashara hiyo nchini.

Simbachawene aliyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya kupinga biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, ambayo hufanyika Julai 30 kila mwaka na kwa mara hii iliahirishwa kutokana na msiba wa Rais, wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Alisema kuna baadhi ya Watanzania ambao wako nje ya nchi, wamerubuniwa na huko waliko wanateseka na kuwa kuna haja ya watu hao kusaidiwa kurudishwa nyumbani.

“Kwa wale ambao wamekwenda kihalali na wanaendelea na shughuli zao bila mashaka, hao waendelee lakini wale wanaonyanyasika na hawajui watarudije nyumbani tuwabaini na hata kupata taarifa zao kutoka kwa familia zao, ili tuangalie namna ya kuwasaidia,”alisema.

Alisema hali ya sasa ni mbaya kwani biashara hiyo inafanywa na magenge makubwa yenye mbinu mbalimbali na kwamba inahitaji ushirikiano kutoka kwa vyombo vinavyotunga na kusimamia sheria, jamii mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali.

“Kwa sasa wapo watu mabingwa hapa nchini ambao wamekuwa wakichukua watoto wenye umri chini ya miaka 18, kuwasafirisha na kuwapeleka kuwatafutia kazi za ndani na wengine husafirishwa bila kujua wanachokwenda kukifanya, lazima tufike hatua tuache kufanya maadhimisho haya kwa nadharia bali kwa vitendo, kwa kufanya msako mkali ili kubiani wanaojihusisha na vitendo hivyo,”alisema.

Alionya, watanzania kutotumia kigezo cha umasikini na ukosefu wa ajira nchini kama kichocheo cha kuruhusu kirahisi vijana na mabinti kwenda nje ya nchi kwa minajili ya kufutafuta kazi.

Alisema wengi husafirishwa kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi, baada ya kufika huko wamejikuta wanaishi kutumikishwa katika biashara ya ukahaba hususani katika nchi za India, Thailand, China, Indonesia na Malaysia.

Alisema, wengine wanatumikishwa kwa kazi za ndani katika nchi za Oman na baadhi ya nchi nyingine za uarabuni ikiwemo Iraq. Waathirika wengi wanaosafirishwa nje ya nchi wanatokea jijini Dar es Salaam, Tanga na Dodoma (Hususani Wilaya ya Kondoa) na wachache ni kutoka mikoa mingine na waathirika wakubwa ni wanawake kuanzia umri wa miaka 16 hadi 26.

Aidha, alisema serikali inaendelea na mchakato wa kufanya mabadiliko sheria na pia kuendelea na mchakato wa kisheria ili sheria hiyo ianze kutumika kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuanzisha mfuko wa kusaidia waathirika, ili watu wanaokumbwa na kadhia hiyo waweze kusaidiwa na kuunganishwa na ndugu zao.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi