loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mume adaiwa kumnyonga mke aliyetoa mimba

POLISI mkoani Rukwa wanamtafuta kijana mkazi wa mtaa wa Kanisa Katoliki Manispaa ya Sumbawanga, Joseph Kalolo ‘Mwamba’ (35) kwa tuhuma za kumnyonga mkewe na kuutenganisha mwili sehemu mbili kwa shoka.

Inadaiwa kuwa baada ya ‘Mwamba’ kumuua Maria Kaozya (30), alimchukua mtoto wao akamkabidhi kwa mama mkwe wake na kisha akaenda kusikojulikana. Inadaiwa kuwa mama huyo hakujua kama ‘Mwamba’ alikuwa amemuua binti yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Justine Masejo amethibitisha tukio hilo. Alieleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa kifamilia lakini hakufafanua kwa undani.

Awali mtoaji taarifa alidai kuwa ‘Mwamba’ aliondoka nyumbani kwake akaenda mkutafuta riziki sehemu nyingine. Alikaa huko kwa zaidi ya miezi mitatu bila kuwasiliana na mkewe aliyekuwa mjamzito wakati huo.

“Mjamzito huyo aliishi kwa dhiki kubwa kwani mumewe alikata mawasiliano na hakumtumia fedha za matumizi hivyo mama huyo aliamua kuitoa mimba hiyo”alidai mtoa taarifa.

Siku chache baada ya Maria kutoa mimba, mumewe alirudi nyumbani na kumhoji alipeleka wapi ujauzito huo na alijibiwa kuwa ameitoa, kwa sababu endapo angejifungua asingemudu kumlea mtoto wao na ndipo mgogoro wa kifamilia ulipoibuka.

Kamanda Masejo alisema kuwa mauaji hayo yalitokea Agosti 9 mwaka huu saa 11 alfajiri katika Mtaa wa Kanisa Katoliki Kata ya Mafulala Manispaa ya Sumbawanga.

Alisema mtuhumiwa huyo alikimbia na kujificha kusikojulikana baada ya kufanya uhalifu huo. Alisema kuwa mtuhumiwa bado hajakamatwa na juhudi za Polisi za kumtafuta zinaendelea.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame, Sumbawanga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi