loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kiwanda cha mbao kuajiri 400

UBALOZI wa Tanzania nchini China umetangaza kuwa kampuni ya Shandong Zurk Ltd ya nchini humo, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbao za MDF nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa ubalozi huo, uwekezaji huo utakafanyika katika Wilaya ya Mafinga mkoani Iringa na unatarajiwa kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania 400.

“Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuanza mwezi Novemba 2020”ulieleza ubalozi huo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Ubalozi huo ulieleza kuwa taarifa kuhusu uwekezaji huo, ilitolewa jana jijini Beijing katika mkutano wa Kiongozi wa Kampuni ya Shandong Zurk Ltd, Mark Zhang na Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki.

“Mbao za MDF hutumika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na fenicha, makabati, milango na sakafu ya mbao ”ilieleza taarifa hiyo. Ubalozi wa Tanzania China umeeleza hayo siku moja tangu serikali izindue matumizi ya stempu, iliyotolewa na Baraza la Dunia la Utalii na Usafiri, inayoitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi salama zaidi duniani.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alizindua stempu hiyo juzi jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa stempu hiyo, itabandikwa katika kila tangazo linalohusu utalii wa Tanzania.

“Ndugu zangu sote tuweke nembo hizi kwenye shughuli zetu, biashara zetu, bidhaa zetu, kwenye vipeperushi vyetu, channels zetu, websites zetu, kila kona! Itasaidia kujenga imani ya Tanzania kwa wageni na kila mmoja wetu atafaidika.

Tumeshinda vita hii! Tuchangamkie fursa sasa,” aliandika Dk Kigwangalla kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, watu wengi kabla ya kufanya uamuzi wa kutembelea nchi yoyote huwa wanataka kujihakikishia usalama wa nchi husika kuanzia ulinzi, huduma za vyakula, malazi na usafiri, hivyo stempu hiyo itawapa uhakika wa kupata huduma hizo.

Alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada zilizofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli, kuhamasisha maendeleo ya sekta ya utalii, na kutoa hamasa kwa wadau kuboresha mazingira ya utalii hadi kufikia hatua ya kukubalika kimataifa.

“Hakika hii ni hatua kubwa na yenye mafanikio kwa nchi yetu, hii stempu inatuweka katika mazingira shindani zaidi ya utalii na nchi nyingine, tunachotakiwa ni kuendelea kuitunza heshima hii kwa kuhakikisha kuwa zile sababu za kupatiwa stempu hii zinazidi kuimarika”alisema Kigwangalla.

Ubalozi wa Tanzania nchini China pia umeeleza kuwa leo madini ya tanzanite na kahawa ya Tanzania, vitatangazwa nchini China kupitia Kituo cha Televisheni cha Hainan.

BIASHARA ya masoko ya madini inazidi kupaa na kuwezesha wajasiriamali ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi