loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Morrison huru orrison huru kwenda Simba

HATIMAYE sakata la Mghana Bernard Morrison dhidi ya Yanga liliochukua siku kadhaa, limemalizika, huku akiwa huru kwenda Simba baada ya mkataba wake kuwa na utata.

Kesi hiyo iliyoanza Agosti 10 ilikuwa inasikilizwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ambapo mchezaji huyo alidai kuwa na mkataba wa miezi sita na umeshamalizika wakati klabu ilidai kuwa mchezaji huyo alikuwa na mkataba wa miaka miwili.

Yanga ilifungua shauri TFF kudai kuwa wana mkataba na mchezaji huyo raia wa Ghana na kumuweka kwenye mikakati yao ya msimu ujao, huku mchezaji huyo akiwa tayari amesaini mkataba wa kujiunga na Simba SC.

Kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa kwa siku tatu mfululizo jana ilitolewa uamuzi kuwa mkataba wa Yanga kwa Morrison ulikuwa na mapungufu, hivyo mchezaji huyo yupo huru kujiunga na timu yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Elias Mwanjala alisema kuwa baada ya kusikiliza shauri hilo kwa siku tatu mfululizo tangu Jumatatu kwa kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, wamebaini mapungufu ambayo hayaoni uhalali wa mkataba, ambao Yanga wanadai waliingia na Morrison.

Aliyataja mapungufu hayo kuwa ni mkataba huo kuwa na tarehe mbili tofauti pamoja na kutokuwepo na saini za pande zote mbili. “Maamuzi yamempa faida Morrison baada ya kuona mapungufu kwenye mkataba ulioletwa kama ushahidi.

“Mkataba uliosainiwa unaonesha tarehe mbili tofauti juu tarehe 20/3/2020 halafu chini unaonesha tarehe 15/7/2020 na pia sehemu inayotakiwa kuwekwa saini kumekatwa na hakuna saini za pande zote mbili, “ alisema Mwanjala.

Aidha, kamati hiyo imemtaka Morrison kurudisha fedha za usajili alizopewa na Yanga ambazo ni dola 30, 000, ambazo alikiri kuzipokea. Pia kamati hiyo imemtia hatiani kwa kosa la kinidhamu Morrison kwa kitendo chake cha kusaini mkataba na klabu nyingine, huku kesi yake ikiwa haijatolewa uamuzi.

“Mwenyewe amekiri kuwa tarehe 8/8/2020 amesaini mkataba na klabu nyingine, kamati imeona amefanya kosa la kimaadili, hivyo tumempeleka kwenye Kamati ya Maadili huko wataangalia kosa lake,” aliongeza Mwanjala.

Nje ya Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mashabiki wa Simba walilipuka kwa furaha baada ya kusikia kuwa mchezaji huyo yuko huru na wala hana mkataba na Yanga huku wenzao wakiondoka kwa unyonge

foto
Mwandishi: Mohamed Mdose

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi