loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Latra yahamasisha wasafiri kutumia mfumo wa elektroniki

BAADA ya kipindi cha kutumia mfumo kwa majaribio ya ukataji tiketi kieletroniki kukamilika, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeendelea kutoa elimu kwa wadau na kusimamia utekelezaji wa matumizi ya mfumo huo.

Aidha mamlaka hiyo imewataka wasafirishaji wote kujiunga na kutumia mfumo huo kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa matumizi ya mfumo wa utoaji tiketi kieletroniki.

Ngewe pia aliwahamasisha wasafiri wote kutumia mfumo huo ili kunufaika nao na kuepuka usumbufu wa kutoka sehemu moja kwenda kukata tiketi pamoja na ule wa wapigadebe.

Alisema kanuni za leseni za usafirishaji kwa magari ya abiria za mwaka 2020 zinamtaka mtoa huduma ya usafiri wa abiria kuunganishwa na kutumia mfumo wa utoaji tiketi za kieletroniki uliothibitishwa na mamlaka hiyo.

"LATRA kwa kushirikiana na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Mtandao (NIDC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wamiliki wa mabasi, Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), kampuni zilizothibitishwa kutoa huduma ya tiketi mtandao, taasisi za fedha na wadau mbalimbali, iliendelea kutoa elimu, kusimamia na kuhamasisha matumizi ya mfumo huu,"alisema.

Alisisitiza kuwa hakuna changamoto yoyote inayoweza kujitokeza na kusababisha mfumo wa ukataji tiketi kukwama.

Naye Mwenyekiti wa Taboa, Abdallah Mohammed aliwataka wanachama wote kufika jijini Dar es Salaam, Agosti 22 mwaka huu ili kuendelea kupata elimu kuhusu tiketi mtandao, kueleza vizuizi wanavyokutana navyo na kuuliza maswali mbalimbali waliyonayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Utengenezaji wa Mifumo kutoka Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Mtandao, George John alisema mfumo huo utaondoa usumbufu wa abiria wa kwenda kukata tiketi mbali na kuwawezesha kutumia simu ya mkononi kupata tiketi.

Alisema baada ya muda mfupi kuanzia sasa huduma hiyo ya ukataji tiketi kwa njia ya mtandao itaanza kupatikana kwa mawakala.

Alisema mfumo huo ni rahisi, pia abiria anapokata tiketi hiyo fedha za mmiliki wa basi zinaingia moja kwa moja kwenye akaunti yake.

SERIKALI imezindua Mpango Mkuu ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Habari Nyingine