loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

New MV Victoria  kuanza usafirishaji abiria, mizigo Jumapili

SHIRIKA la Huduma za Meli Tanzania (MSCL), linatarajia kuanza kutoa huduma za usafiri wa abiria na mizigo ndani ya Ziwa Victoria kuanzia Agosti 16, mwaka huu, kutoka Mwanza kwenda Kagera na Nansio, wilayani Ukerewe.

Akizungumza na HabariLEO jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa MSCL, Erick Hamis, alisema tayari maandalizi kwa ajili ya kuanza kwa safari hizo yamekamilika, ambapo meli ya New Victoria ‘Hapa Kazi Tu’ itaanza safari zake kwenda Bukoba Agosti 16, mwaka huu kupitia bandari ya Kemondo baada ya kukarabatiwa kwa Sh bilioni 22.7

Alisema meli nyingine iliyopata cheti cha ubora wa usafiri majini ambayo nayo itaanza kutoa huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwenda Nansio wilayani Ukerewe ni Mv New Butiama, ambayo ukarabati wake umegharimu Sh bilioni 4.9.

Hamis alisema meli ya New Victoria yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo, itakuwa na madaraja matatu ya usafiri, ambapo katika daraja la tatu abiria atakuwa akitozwa nauli ya Sh 16,000, daraja la pili Sh 30,000 na daraja la kwanza Sh 45,000.

Alisema meli hiyo awali ilikuwa ikitumia saa 12 hadi 13 kutoka Mwanza kwenda Bukoba, lakini kwa sasa itakuwa ikitumia saa sita, huku ikiwa imewekewa samani na vifaa vya kisasa kwa ajili ya usafiri wa majini na kuifanya kuwa na muonekano mpya na wa kuvutia.

Alisema meli ya New Butiama ina uwezo wa kubeba abiria 180 na tani 100, imefanyiwa ukarabati na kuwa ya kisasa, itakuwa na madaraja mawili ya abiria, la tatu ambalo abiria atatozwa Sh 8,000 kwenda Nansio na daraja la kwanza Sh 10,000.

Akizungumzia kuanza kwa safari hizo, Mkuu wa Kanda ya Ziwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Gloria Munhambo, alisema kutachochea sekta ya utalii katika Kanda ya Ziwa kwani kuna vivutio vingi ndani ya Ziwa Victoria ambavyo watalii watapenda kuviona.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Alexander Sanga, Mwanza

Post your comments

Habari Nyingine