loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wahitimu 400 waliosoma nje ya nchi kukutanishwa

WAHITIMU 400 waliosoma vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi, wanatarajiwa kukutanishwa katika mahafali ambayo yanatarajiwa kuwa daraja na fursa kwao kujua fursa za uwekezaji wanazoweza kutumia ujuzi wao kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa taasisi ya Global Education Link (GEL) inayowaunganisha wanafunzi na vyuo vikuu nje ya nchi, Abdulmalik Mollel, wakati akizungumzia mahafali hayo yanayotarajiwa kufanyika Septemba 19, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

“Lengo la mahafali hayo ni kuhakikisha wanafunzi Watanzania waliosoma nje ya nchi hawarudi kimyakimya na kinyonge, kwani wao ni wazalendo walioamua kuacha fursa zilizoko huko baada ya masomo yao na kuja kuijenga nchi yao,” alisema.

Mollel alisema wahitimu hao walikwenda kusoma nje ya nchi kwa ajili ya manufaa yao na familia zao na nchi yao, hivyo kurudi kwao ni kurejesha shukrani nyumbani, kwani wanatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa nchi.

“GEL itawakutanisha wahitimu hao kwa ajili ya kujenga mtandao na taasisi na watu mbalimbali hapa nchini baada ya kukaa nje ya nchi kwa muda mrefu ambako walishajenga aina nyingine ya maisha.”

“Mfano mwanafunzi ameenda huko akiwa na miaka 17 amekaa huko miaka minne au sita, anarudi amekuwa mtu mzima, amekuta mambo mapya, sasa akifika akikosa timu kama aliyokuwa nayo kule anakata tamaa, kitendo cha kumkutanisha mtu aliyekuwa Uingereza, India, China, Canada au Afrika Kusini kwenye jengo moja ni jambo kubwa na la msingi,” alisema.

Mollel alisema wanafunzi hao wakikutanishwa watatengeneza mtandao mpya na wenzao waliomaliza nao mwaka mmoja kwenye vyuo vya nje ya nchi kwa sababu awali hakukuwa na mahafali ya aina hiyo.

Kwa mujibu wa Mollel, mahafali hayo ni fursa kwa wahitimu hao kwani kuna kampuni ambazo zimetoka nchi mbalimbali ambazo walisoma na zinatafuta wataalamu wa fani wanazozihitaji, hivyo wakikutanishwa itakuwa na manufaa kwao.

“Kuna wawekezaji ambao wanatafuta watu waliosoma kwenye nchi zao angalau wenye kujua lugha zao kidogo, sasa hii ni fursa kwao kwani watakutanishwa na wawekezaji.”

“Kuna taasisi za serikali kama menejimenti ya utumishi wa umma na ile ya kutafutia watu ajira ya Taesa nazo zinahitaji rasilimali watu ambazo zipo lakini hakuna daraja lililowakutanisha, hivyo mahafali hayo ni daraja la kuwaunganisha wahitimu hao na taasisi hizo,” alisema.

Alisema taasisi za serikali na za binafsi zitakaposhiriki kwenye mahafali hayo zitapata kujua orodha ya wanafunzi waliosoma fani mbalimbali wanazohitaji, hivyo kutengeneza daraja baina ya pande hizo mbili na kuondoa malalamiko kwamba kuna uhaba wa wataalamu na vijana kulalamikia tatizo la ajira.

Alisema mahafali hayo pia ni jukwaa kwa serikali kutumia wanafunzi hao kuitangaza nchi kwenye nyanja mbalimbali ikiwamo elimu na utalii kwa wanafunzi wenzao wa nje ya nchi, hivyo kuvutia vyuo kuja kuwekeza nchini na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine