loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kupatikana na changamoto za kujifunza lugha

KILA binadamu ana lugha anayoitumia katika mawasiliano ya kila siku. Lakini yawezekana mtu asifahamu kuwa lugha anayoitumia sasa ameipata na imetoka wapi.

Kuna wakati unaweza kugundua kuwa hapa  unajifunza lugha, na kuna wakati inatokea tu unaijua lugha fulani.

Makala haya yatakuonesha jinsi ulivyoipata lugha yako na vitu gani vifanyike kuwasaidia hasa watoto au watu wazima wanapojifunza lugha.

Hapa pia utapata mwanga wa swali linalopasua vichwa vya wengi wanaodai “Sisi Watanzania hatujui lugha yetu ya Kiswahili.”  Je, ni kweli  Watanzania hatujui Kiswahili?  Karibu tujifunze.

Izingatiwe kuwa, lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zenye kubeba maana na zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika  mawasiliano.

Katika sehemu yenye fumbo la lugha ni unasibu, unaomaanisha sauti zilitokea kama bahati tu kwa binadamu kwani hakukuwa na makubaliano yoyote kuanzisha lugha.

Wanyama hawatumii lugha kama chombo cha mawasiliano, kwa kuwa lugha ni sauti zenye maana na kukubaliwa na jamii.

Mbali na maana ya kawaida kuna pia lugha ya ishara inayotumiwa na wenye ulemavu wa kuongea (bubu).

Vilevile, ieleweke kwamba tangu kale, lugha zimekuwa zikichipuka, kukua, kusambaa na kufa. Kwa hivyo, lugha zilizopo leo ulimwenguni, huenda baada ya karne nyingi kupita zitatoweka na kuzuka nyinginezo.

Sifa kubwa ambayo binadamu tunajivunia ni kuweza kuwasiliana kwa lugha zetu. Jambo la kustaajabisha, baadhi  ya watu huona lugha fulani ni bora kuliko nyingine.

Ukweli ni kwamba, hakuna lugha bora zaidi duniani, kwa kuwa lugha zote zina ubora, ili mradi  tu zinakidhi matakwa ya jamii inayohusika. 

Dhana inayowachanganya watu kusema lugha moja ni bora kuliko nyingine yawezekana wameshindwa kugundua umuhimu wa lugha za kimakabila, lugha za kitaifa na lugha za kimataifa.

Kwa hiyo, ubora unaofikiriwa zaidi ni pale lugha inapoitwa ya kitaifa au kimataifa wakisahau kuwa hata ile lugha ya kikabila ni bora maana inawasaidia kuwasiliana na kufanya shughuli zao bila shida.

Hapa tujue “usipokithamini cha kwako hakuna atakayekithamini”. Hivyo lugha yako ina thamani kubwa hivyo usiidharu wala kuiona si bora kwa kuwa ndiyo inayokusaidia katika shughuli zako za kila siku.

Binadamu katika harakati zake za maisha tangu anapozaliwa, anaweza kujua lugha nyingi ili kukidhi mahitaji yake. 

Tuangazie lugha hizo;

Lugha ya kwanza ni lugha anayoipata mtoto baada ya kuzaliwa. Mfano hapa Tanzania, yawezekana lugha ya kwanza kwa wengi ikawa lugha za kimakabila  kama vile; Kisukuma, Kizigua, Kigogo, Kimasai, Kinyamwezi, Kipare, Kichaga n.k.

Kwa wengine hasa watu waliozaliwa katika miji na majiji, lugha yao ya kwanza yawezekana ni Kiswahili  na kwa asilimia chache, Kiingereza. 

Lugha ya pili,  ni lugha ya kujifunza, mara nyingi hujifunzwa kwa makusudi fulani baada ya kupata lugha ya kwanza.  Kwa mfano, hapa Tanzania Kiswahili ni lugha ya pili kwa watu wengi na Kingereza kwa wachache.

Ingawa kwa kizazi cha sasa kutokana na kupanuka  kwa miji,  watu wa makabila tofauti kuoana, Kiswahili kutumika shuleni n.k. lugha ya Kiswahli imeanza kuwa lugha ya kwanza.

Hata hivyo, maeneo mengi ya vijijini bado Kiswahili ni lugha ya pili kwa kuwa wengi hujifunza lugha hiyo wakiwa shuleni.

Lugha ya kigeni ni ile anayojifunza mtu na kuitumia, lakini wazungumzaji wake wa asili wako nje ya nchi au mbali na jamii anapokaa mwanafunzi huyo. Mfano lugha ya Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kijerumani ni lugha za kigeni nchini  Tanzania.

Mara nyingi lugha ya kigeni hujifunzwa kwa malengo ya kuwasiliana na wageni, kufanya biashara au utalii n.k.

Kumbe kuna watu wamepata lugha tu bila kufanya jitihada yoyote kuijua  lugha hiyo, badala yake, wameipata tu kwa wazazi au jamii inayowazunguka.

Hiyo ndio lugha ya kwanza.  Pia, kuna watu wamefanya jitihada kubwa ya kujua lugha wakiwa na malengo fulani. 

Hapa lugha ya pili na ya kigeni. Kujifunza na kujua lugha ya pili na kigeni kuna faida ya kuongeza fursa mbalimbali. Hii inaweza kuonekana kuwa ngumu, lakini kwa upatikanaji wa maeneo ya kujifunza lugha na programu, unaweza kujifunza lugha zaidi.

Huenda usione kuwa ni faida kujifunza lugha mpya hadi ukiwa katikati ya watu wanaozungumza lugha usiyoielewa.

Kimsingi, kuna ujasiri unaoupata unapoweza kuwasiliana na watu wa jamii na tamaduni tofauti, kwa lugha yao wenyewe. Mfano, rejelea mtu anayejua lugha ya kigeni vizuri akiwa kwenye jamii yake anavyopata ujasiri wa kuzungumza mambo.

Kujifunza lugha ya pili au kigeni siyo kazi rahisi kwani kuna mambo mengi. Mambo hayo ni yale ama yanayomwezesha au yanayomkwamisha mjifunzaji lugha kujua lugha.

Umri: Mtu mwenye umri mdogo ana uwezo mkubwa zaidi katika kujifunza lugha kuliko mwenye  umri mkubwa.

Mfano, mtoto mwenye  umri chini  ya miaka tisa, anaweza kujua lugha kwa haraka kwani hana vitu vingi katika ubongo wake na hana aibu katika kujifunza.

Kwa mtu mzima, inakuwa ngumu kidogo kwa kuwa tayari anakuwa na lugha nyingine inayosigana na lugha anayojifunza na pia, ana aibu ya kufanya makosa wakati wa kujifunza lugha.

Hii inatukumbusha kwamba, msingi mzuri wa kumjenga mtu ajue na kumudu lugha, unapaswa kufanyika katika umri mdogo.

Hivyo, watoto wapewe nafasi kubwa ya kufundishwa lugha katika umri mdogo japo mtu mzima pia anaweza kujifunza, japo itamchukua muda mrefu.

Hali ya kiuchumi ya mjifunzaji lugha:  Kujifunza lugha ni gharama. Kwa sasa ukitaka kujifunza lugha fulani itakupasa uweze kumlipa mwalimu na kununua vitabu na vifaa vitakavyokusaidia kujifunza lugha hiyo. 

Kwa upande mwingine mtu mwenye kipato cha chini anaweza akashindwa kununua vifaa vya kisasa, vitabu na  fedha ya kulimpa mwalimu ili kupata lugha, maana vyote hivyo vina  gharama kubwa. 

Vilevile, ieleweke  kwamba lugha inahitaji uwekezaji hivyo inahitaji kujinyima na kuwekeza, kwani huwezi ukajifunza bila gharama.

Msaada wa kifamilia/jamii lugha: Jamii ina mchango mkubwa katika kumfunza mtu mgeni lugha. Ikiwa mwanafunzi lugha anayojifunza inatumika ndani ya jamii hiyo, ataifahamu haraka lugha kuliko mwanafunzi ambaye anajifunza lugha ambayo haitumiki katika jamii. 

Kwa mfano, Mtanzania anayetaka kujifunza Kiingereza anapata shida kwa sababu wazungumzaji wake wako nje ya nchi.

Hivyo, ili kujifunza lugha kwa urahisi na ufasaha mjifunzaji  wa lugha ya kigeni  anashauriwa kuishi na jamii inayotumia lugha hiyo.

Hii inatokana na ukweli kwamba kuna vipengele vya kiutamaduni na muktadha wa lugha vinayoendana na mazingira ya watumiaji lugha, kwa hiyo mtu akijifunza lugha katika mazingira  ya wazawa, anajifunza mambo mengi zaidi.

Kiwango cha elimu: Mtu mwenye kiwango kikubwa cha elimu ana uwezo mkubwa wa kupata lugha kuliko mtu asiye ma elimu kabisa.

Elimu inamwezesha mtu kujifunza mambo mengi, kadri anavyojifunza anaongeza msamiati  wa lugha, hivyo inamuwia rahisi hata kulinganisha lugha aliyonayo/alizonazo na lugha mpya anayojifunza.

Matarajio, malengo na mtazamo: Kama mjifunzaji lugha ana lengo la kufanya utafiti sehemu fulani, kujiajiri/kuajiriwa nje ya nchi, kusafiri nje ya nchi, kusoma, kufanya biashara n.k. Matarajio yake ni kujifunza lugha na kuimudu ili akafanye kazi yake kwa wepesi.

Kama mwanafunzi hana matarajio yoyote, basi itakuwa ngumu kupata lugha. Pia, mwanafunzi kama ana mtazamo hasi na lugha anayojifunza, itakuwa ngumu kupata lugha.

Mtazamo chanya ndio utakaomsaidia mjifunzaji lugha kupata lugha kwa wepesi na haraka.

Kwa mfano, mwanafunzi anayeona kuwa Hesabu ni somo gumu, hawezi kulipenda na kuongeza bidii ya kujifunza kwani ameshakata tamaa kuhusu somo hilo.

Motisha: Ni tabia au msukumo katika kutimiza malengo fulani. Baadhi ya watu wanadai kuwa motisha ni kitu kama fedha inayotolewa ili kumtia mtu hamasa kujifunza jambo.

Hata hivyo, si lazima umpe kitu, bali unamtia moyo mwanafunzi na kumsaidia. Motisha ni kipengele muhimu katika ujifunzaji lugha.

Mwanafunzi mwenye motisha ya ndani ana uwezo wa kufanya uamuzi, kujifunza kwa jitihada kubwa, si mwepesi wa kukata tamaa hata akikutana na changamoto za kumkwamisha.

Jambo lolote lile ambalo mtu anaamua kufanya mwenyewe kwa hiari yake, ni rahisi kulitekeleza na kulikamilisha kuliko jambo la kushauriwa na kuamriwa na mtu mwingine. Hivyo, bidii ya kujifunza lugha ianze  na mtu mwenyewe kuliko kusubiri ushawishi kutoka kwa wazazi/jamii au serikali.

Haiba na viigwa: Wanafunzi wacheshi hupata lugha haraka kuliko wanafunzi ambao siyo wacheshi. Wacheshi hupenda ‘kujichanganya’ na watu.

Kujichanganya na watu kunamsaidia mjifunzaji kuisikia lugha inavyozungumzwa na kutumiwa hivyo ni rahisi kwake kujifunza na kujirekebisha anapokosea. Vilevile, watu wenye hadhi fulani katika nchi  huwafanya  wengine kujifunza kutoka kwao.

Hii ni kwamba mjifunzaji anatafuta mtu maarufu katika jamii ili azungumze kama yeye?  Hii inamsaidia kwa sababu mjifunzaji lugha atajaribu kujitahidi azungumze kama mtu huyo.

Muktadha/mazingira: Mazingira ni muhimu katika upataji lugha. Mazingira mazuri yenye miundombinu wezeshi humvutia na kumtengenezea mjifunzaji uelewa.

Darasa lililojengewa mazingira ya ukutani kama michezo mbalimbali, dhana za kufundishia kama picha, michoro na vitu halisi vinavyowezesha wanafunzi wamudu lugha haraka.

Kwa jumla kila lugha ina umuhimu wake, lugha ya Kiswahili kwa sasa ni lugha yenye thamani kubwa  duniani kutokana na kuwa imeenea maeneo mengi ndani na nje ya mipaka yake.

Hata hivyo, haimaanishi tusijifunze lugha nyingine za kigeni, bali tujifunze pia lugha zingine za kigeni kama Kiingereza na Kichina ili kupanua wigo wa mawasiliano ya kimataifa.

Mwandishi ni Mchunguzi wa Lugha II katika Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA). Anapatikana kwa 0762020227 namsoffearnoldm@gmail.com.

WAKATI Rais John Magufuli ...

foto
Mwandishi: Arnold Mayange Msofe

Post your comments

Habari Nyingine