loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tujadili kampeni tuwaache ‘wajumbe’

UKIIWEKA kando kidogo habari ya kifo cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa inayoendelea kutikisa na kuhuzunisha nchi, hivi karibuni upande mwingine wa habari na mijadala umetawaliwa na habari ya watu wanaoitwa ‘wajumbe’.

Hawa, wamejizolea umaarufu mkubwa tangu mchakato wa kura za maoni uanze kwa vyama mbalimbali kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wajumbe wametengenezewa kila aina ya vibonzo, vibwagizo, utani na vichekesho vya picha, video na mazungumzo ya kila namna. Stori za utani na vichekesho kuwahusu wajumbe zimetawala mijadala ya Watanzania.

Hata baadhi ya viongozi nao, wameingia katika mkumbo huu wa kuipa uzito habari ya utani na kuchekesha ya wajumbe na kuyaacha mengi muhimu na yenye tija.

Kwa mfano, hakuna anayejadili mchakato mzima wa kura za maoni ambao kimsingi ni jambo zito na muhimu kwa taifa.

Kwa Watanzania wengi, utani, vichekesho na vibwagizo kuhusu wajumbe umekuwa ndiyo habari pekee ‘waliyoishikia bango’ na kuendelea kuipa uzito mkubwa.

Hakuna anayejadili mchakato wenyewe wa kura za maoni unaoenda kutupatia wawakilishi na watatuzi wa shida zetu kupitia vyama hivyo.

Kwa mfano kwamba, je, mchakato uliendaje? Je, hao walioongoza kura za maoni wanaakisi kweli shida za watu? Wamepatikanaje?

Kwamba ni akina nani waliopiga kura za kuwachagua watu hao? Weledi na umakini wa watu hao waliopiga kura za maoni ukoje? Hali ya rushwa ikoje na mambo mengine ya msingi ndani ya mchakato huo yakoje!

Hii sasa imekuwa kama homa katika taifa, kwamba vitu visivyo vya msingi hupata muda mwingi kujadiliwa na watu mitaani, kuliko yale ya msingi.

Hapa ni lazima kuwa makini na kujua upungufu uliojitokeza hata kama utakuwa ndani ya chama tawala ambacho hata walio upande wa upinzani, hawapaswi kuchekelea, bali kujitazame ‘walivyosimama,’ badala ya kusubiri anguko la chama tawala hata kama labda kuna sehemu wajumbe walikosea.

Hii ni kwa kuwa chama tawala kikiharibikiwa, imeharibikiwa nchi maana ndicho hupanga sera na mipango na safu ya uongozi ya serikali inayokwenda kutekeleza haja za watu.

Hivyo, upo uhusiano mkubwa kati ya chama tawala na kustawi, au kudorora kwa nchi.

Sasa inashangaza kuona anayejali kuhusu suala la rushwa lililoonekana kushamiri kwenye mchakato  wa kura za maoni katika vyama.

Kwamba hata tunapokwenda kwenye kampeni na uchaguzi, tunawezaje kupata viongozi makini nje ya uwanja uliogubikwa na rushwa.

Kwamba ni kwa namna gani kupunguzwa kwa idadi ya wapigakura kuliwapa au kuwanyima nafasi watoa rushwa (waliokuwapo) kumwaga fedha zaidi kwa wajumbe ili wawapigie kura; nani anayejadili hili?

Na vipi kuhusu aina ya wajumbe waliokuwa kwenye chobo chenyewe cha uamuzi wa kupiga kura za maoni; uwezo wao kupinga rushwa na kupima sera za wagombea badala ya kuegemea fedha ukoje?

Tujadili sasa mintarafu mwamko na idadi ya vijana waliopo kwenye eneo hilo la maamuzi.

Nani anayejadili hayo au nani anayejadili weledi wa wajumbe wanaopiga kura za maoni ngazi za mashina, matawi na kata; kwamba weledi wa watu hao katika kupinga rushwa na ugumu wao kununulika ukoje!

Sasa Watanzania tujipe pia muda wa kutafakari sababu za anguko la vijana wengi katika mchakato huu licha kuhamasishwa na kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea.

Wakati tunaelekea kupiga kampeni na hatimaye kupiga kura, Watanzania tutafakari kama azma ya kuhamasisha vijana kugombea walisaidie taifa kama itafanikiwa kutokana na hali ilivyo katika vyama ambapo vijana wengi wanaonekana kuachwa nje.

Tujiulize kuwa, baada ya uchaguzi, nani anafikiria kuhamasisha vijana wasichoke wala kukata tamaa, bali wajitokeze kuomba nafasi za chini za uongozi, uwakilishi na maamuzi hasa za ujumbe katika kata na matawi.

Kimsingi, umefika wakati Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake, tumsaidie Rais John Magufuli kufanikisha azma ya kupata ushindi dhidi ya rushwa katika kupata na kutumia haki mbalimbali ikiwamo ya kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi wa kisiasa.

Mungu Ibariki Tanzania.

 

Mwandishi wa makala haya ni msomaji na mchangiaji katika gazeti hili.

foto
Mwandishi: Galila Wabanhu

Post your comments

Habari Nyingine