loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tetemeko laitikisa Dar es Salaam

WAKALA wa Jiolojia Tanzania (GST) umethibitisha kutokea tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha richa 6.0 jijini Dar es Salaam, mikoa ya Morogoro na Tanga na nchi jirani ya Kenya.

Wakala huo umetoa tahadhari kwa wajenzi na wananchi kwamba hakuna sababu ya kujenga nyumba ndefu kuliko kawaida au kupaua mapaa marefu kupita kiasi, kwa sababu inaweza kuwa chanzo cha madhara yanapotokea majanga ya asili yakiwemo matetemeko.

Akizungumza na HabariLeo jana kwa njia ya simu kutoka Dodoma, Mjiolojia Mwandamizi ambaye pia na Mkuu wa Kitengo cha Majanga ya Asili ya Jiolojia wa GST, Gabriel Mbogoni alisema kuwa tetemeko hilo lilitokea saa 2: 13 usiku.

Alisema kuwa kitovu cha tetemeko hilo ni umbali wa Kilomita 90 Kusini Mashariki ya jiji la Dar es Salaam kwenye mkondo wa mpasuko wa miamba baharini kwenye Kisiwa cha Madagascar.

Mbogoni alisema kuwa tetemeko hilo ni la kawaida la asili, linalotokana na nguvu ya miamba kusigana au kukandamizana, na kwamba halina uhusiano wowote na masuala ya hali ya hewa.

Alisema kuwa tetemeko hilo juzi usiku lilisikika pia mikoa ya Morogoro, Tanga, kisiwa cha Mafia na nchi jirani ya Kenya katika mikoa ya pembezoni mwa Bahari ya Hindi.

Alitoa wito kwa wananchi wachukue tahadhari linapotokea tetemeko na wasikimbilie kutoka nje ya nyumba, bali wakae chini ya kitanda, meza au pembezoni mwa kuta za nyumba zinapokutana ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea iwapo nyumba itabomoka.

Alisema kuwa mtu anapokaa chini ya meza au kitanda, husaidia vitu vizito kama vitaanguka havitamfikia kwa harana na hali hiyo inapunguza madhara na hata kama vitamfikia madhara yake yanakuwa madogo.

Alitaja tahadhari nyingine kuwa ni kuzima swichi kubwa ya umeme ili kuzuia madhara. Alisema kuwa wakati mwingine tetemeko linaweza kuharibu mfumo wa umeme na kusababisha moto.

Alishauri wananchi wakati wa tukio kama hilo wanapotaka kuomba msaada, watumie ujumbe mfupi wa maandishi badala ya kupiga simu. Kituo cha Jiolojia cha Marekani (USGS) kimesema tetemeko hilo limetikisha maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi hasa Dar es Saalam na mikoa jirani na kwamba zaidi ya watu milioni 8 walisikia mtikisiko wake.

Tetemeko hilo limetokea baada ya matetemeko mengine kadhaa yaliyotokea Tanga mapema Machi mwaka huu yenye ukubwa wa kipimo cha Richa 4.9. Kitovu cha tetemeko hilo ilikuwa eneo la Vulaya umbali wa Kilometa 19 kutoka Maramba, Korogwe mkoani Tanga.

Mengine ni yale yaliyotokea Mpanda, Katavi lililokuwa na kipimo cha richa 5.4 na mzingo wa kilometa 25 mwaka mmoja uliopita, la Mbulu mkoani Manyara lenye kipimo cha Richa 4.2 na kilometa 10 za mzingo na la Magugu, Manyara lililokuwa na kipimo cha Richa 4.1 na kilometa 10 za mzingo.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine