loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bandari Tanzania

SERIKALI imeridhishwa na mradi wa upanuzi Bandari ya Dar es Salaam, ambao umefi kia asilimia 80 kwa lengo kuziwezesha bandari za Tanzania kumudu ushindani na kudhibiti soko kutoka bandari zingine za Afrika. Mradi huo ulianza Juni 2017, utakamilika Januari mwakani na unatekelezwa na Kampuni ya China Harbour.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alipokagua maendeleo ya mradi huo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kamwelwe alisema kuwa serikali imetumia Sh bilioni 337 katika mradi huo, unaojumuisha ujenzi wa jumla ya magati saba na eneo la kuhifadhia magari (yadi) yanayoshushwa kutoka kwenye meli na kusubiri kuchukuliwa na wamiliki.

Alisema kuwa eneo hilo la kuhifadhia magari, lina ukubwa wa hekta 7.5 na lina uwezo wa kuhifadhi magari 3,000 kwa wakati mmoja na kubainisha kuwa kwa sasa bandari hiyo inapokea magari 170,000 kwa mwaka.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, lengo la Tanzania ni kuhakikisha inakamata soko la magari 600,000 kutoka nchi zote za Afrika Mashariki (EAC), kusini mwa Afrika (SADC) na nchi zingine za Afrika.

“Ili kuinua uchumi, miundombinu ni jambo la msingi, mpaka sasa gati namba 1 hadi 4 yameshakamilika, wakati gati namba 5 ujenzi wake umefikia asilimia 75, gati namba 6 asilimia 52 na gati namba 7 asilimia 15, lakini pia tunapanua Bandari ya Tanga na Mtwara ili kuzifanya bandari zetu zimudu ushindani kutoka bandari zingine za Afrika, tutoe huduma bora, salama na nafuu kwa saa 24,”alisema Kamwelwe.

Alisema kwa sasa Tanzania inapokea meli kubwa za mizigo zinazotoka moja kwa moja Ulaya na Asia kuja Bandari ya Dar es Salaam, tofauti na zamani meli hizo zilikuwa zinapitia nchi jirani na kisha mzigo hupunguzwa kwenye meli ndogo na kuuleta Bandari ya Dar es Salaam, hali iliyosababisha bidhaa kuuzwa kwa bei ghali.

Katika kuhakikisha Tanzania inadhibiti soko la bandari katika ukanda wa EAC, SADC na Afrika, Kamwelwe alisema kuwa serikali pia itaongeza kina cha mlango wa bahari kutoka mita 10.5 za sasa hadi kufikia mita 15.5 ili meli kubwa za mizigo ziweze kuingia bandarini kwa urahisi kwa kuwa magati yaliyopanuliwa yameongezwa kina hadi kufikia mita 15.

Kwa mujibu wa Kamwelwe, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imeingia mkataba na Kampuni ya Saruji ya Dangote ili kubeba saruji tani milioni mbili kwa mwaka kutoka kwenye kiwanda cha Mtwara hadi Bandari ya Dar es Salaam.

Bandari ya Dar es Salaam inapokea meli nane za mizigo zenye ukubwa tofauti kwa siku pamoja na magari 15,000 kwa mwezi. Aidha, Kamwelwe pia jana alitembelea mradi wa ujenzi wa mita za kupimia mafuta (flow meter) unaotekelezwa na serikali bandarini hapo.

Alisema serikali inajenga jumla ya mita 29 za kupimia mafuta kwa gharama ya Sh bilioni 47 huku mita 19 kati ya hizo zipo Bandari ya Dar es Salaam, sita zipo Bandari ya Tanga na nne zipo Bandari ya Mtwara.

SERIKALI imezindua Mpango Mkuu ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine