loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tasac waagizwa kusimamia

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuhakikisha wanakuwepo kwenye maeneo yote nchini ambako ujenzi na ukarabati wa meli na vivuko unafanyika.

Alisema kuwepo kwa Tasac katika maeneo hayo kutasaidia ukaguzi wa ujenzi kufanyika mara kwa mara na kuepuka ucheleweshaji usio wa lazima.

Alitoa maagizo hayo jana baada ya kukagua ujenzi wa Kivuko cha Mafia unaofanywa na Kampuni ya Songoro Marine eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu aliridhishwa na ujenzi wa kivuko hicho ambao umefikia zaidi ya asilimia 80. Majaliwa alisema kivuko hicho kitakuwa kinatoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Nyamisati wilayani Kibiti na Kisiwa cha Mafia.

Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo likiwemo lori aina ya semitrailer moja na magari madogo manne.

“Naiagiza Taasisi ya TASAC kuja kukagua ujenzi wa kivuko hiki na ujenzi na ukarabati meli na vivuko maeneo mbalimbali nchini, wafanye ukaguzi kwa kila hatua na kutoa cheti,” aliagiza Waziri Mkuu na kuongeza:

“Nawaagiza TASAC wasiwe mbali na ujenzi au ukarabati wa meli na vivuko, wanatakiwa kufanya ukaguzi hatua kwa hatua, na si kuchelewa halafu wakija kukagua na kuona mapungufu wanaagiza kibomolewe na ujenzi uanze upya.” Sambamba na hilo aliitaka TASAC kutoa vibali kwa meli ya New Mv Victoria na meli nyingine zote ambazo ujenzi au ukarabati wake umekamilika ili zianze kutoa huduma kwa wananchi.

Majaliwa alisema kwa muda mrefu wananchi wa Mafia hawana kivuko cha uhakika, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa kivuko hicho kitawaondolea wananchi hao adha ya usafiri.

Aidha aliwataka Watanzania kuwapuuza watu wanaobeza juhudi za serikali za kuwajengea na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa maji, anga, barabara na reli.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilipitia maeneo yote ya visiwa nchini ili kujenga vivuko vitakavyowasaidia wananchi kuendesha shughuli zao kiuchumi na kijamii bila tatizo.

Majaliwa alisema maendeleo ya watu hayawezi kufikiwa kama hakuna maendeleo ya miundombinu ikiwemo ya usafirshaji, afya na mingine mingi.

Aliipongeza kampuni ya Songoro Marine ambayo inamilikiwa na Mtanzania lakini pia hata wataalamu wake wote, Mkurugenzi Mtendaji na wafanyakazi ni Watanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine, Saleh Songoro, alisema ujenzi wa kivuko hicho cha Mafia ambao ulianza mwaka jana, utakamilika mwezi ujao na unagharimu Sh bilioni nne. Alisema kivuko hicho kina urefu wa mita 43 na upana mita 12.

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine