loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Taasisi hizi zimeonesha uungwana kwa JPM

KATIKATI ya wiki hii taasisi tatu nchini zilionesha uungwana kupitia tamko lao la pamoja.

Taasisi hizo ni Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) na Global Peace Foundation (GPF) Tamko hilo lilihusu nafasi na ushiriki wa wanawake katika uchaguzi mkuu wa kisiasa nchini, ambapo zilimshukuru na kumpongeza Rais John Magufuli kwa namna anavyozingatia haki na usawa katika jamii ikiwamo usawa wa kijinsia katika uchaguzi wa kisiasa.

Taasisi hizo zilimpongeza Rais Magufuli kwa kuendelea kumchagua Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Pia zilipongeza vyama vya siasa vilivyowapitisha wanawake kugombea urais na umakamu wa rais.

Ikumbukwe kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Rais Magufuli alimteua Samia kuwa mgombea mwenza na sasa ni Makamu wa Rais. Rais alifanya hivyo baada ya kuteuliwa kugombea na chama chake.

Tunasema taasisi za Tamwa, WiLDAF na GPF zimeonesha uungwana mkubwa kwa kumpongeza Rais na kueleza kuwa zitahakikisha wanawake wanashikirikishwa zaidi katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuanzia ngazi ya vyama ili wanawake wasiachwe nyuma.

Kwa mujibu wa taasisi hizo, wanawake wengi hawashiriki kikamilifu katika uchaguzi kutokana na kutopata baraka kutoka vyama vyao.

Chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa’, taasisi hizo zimeendesha midahalo ya wanawake kutoka vyama vya siasa na viongozi wa dini katika Kanda za Dodoma, Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam na kubaini changamoto zinazosababisha ushiriki duni wa wanawake katika siasa.

Changamoto hizo ni kuwapo matumizi ya lugha dhalilishi zinazowavunja moyo wanawake wanaogombea, rushwa ya fedha na baadhi ya wenye nafasi kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono.

Kimsingi, hizi ni changamoto zinazosababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa.

Tunaungana na taasisi hizo kuunga mkono kauli ya Rais Magufuli kutaka viongozi wa vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wadau wote wa uchaguzi, kutumikia vema nafasi zao ili uchaguzi wa mwaka huu uwe huru, haki na wa amani.

Ndiyo maana tunasema Tamwa, WiLDAF na GPF wameonesha uungwana kwa kumpongeza Rais Magufuli na kuonesha nia ya dhati ya kuchangia kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa huru, haki na wa amani.

HATIMAYE safari za ndege kati ya Tanzania na Kenya zimerejea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi