RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir amekubali kumuacha madarakani, Jenerali Akol Koor, kama mkurugenzi wa usalama wa taifa mpaka mwisho wa kipindi cha serikali ya mpito mwaka 2023.
Chanzo kimoja cha habari kutoka serikalini kimeeleza kuwa, Rais Kiir amefikia hatua hiyo baada ya mkutano wa maridhiano kati yake na Koor ulioandaliwa na Baraza la Wazee la Jieng.
“Mkutano ulifanyika Jumatatu kwa kuandaliwa na baraza hilo la wazee nchini Sudan umemshawishi Rais Kiir kumuacha Jenerali Koor katika nafasi yake mpaka mwaka huo ambapo itakuwa mwisho wa serikali ya mpito,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Siku za hivi karibuni, kumekuwa na msuguano baina ya viongozi hao baada ya Koor kufungua uwanja wake binafsi wa ndege kijijini kwake Awul katika kaunti ya Tonj North, jambo lililomkasirisha Rais Kiir na kuamuru uwanja huo kufungwa.