loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Haki ya uhuru wa mawazo isitumike vibaya

HAKI ya Uhuru wa Mawazo au Haki ya Kujieleza, ni haki ya mwananchi yeyote wa Tanzania, unaoelezwa vizuri katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake ; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi na  pia anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

Pia, kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii. 

Ni wazi kuwa kutokana na ibara hiyo, haki ya uhuru wa mawazo inajumuisha haki ya kutoa mawazo au maoni ya aina yote, yawe ya kupendeza au kukosoa, kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja anakuwa huru kutoa maoni yake katika jambo lolote katika ngazi ya familia, kazini, katika jamii na kwa nchi, kwa kuzingatia mipaka ya utoaji wa maoni yake.

Lakini, watu wamekuwa wakitumia vibaya haki hiyo au uhuru huo, hususan katika mitandao ya kijamii kwa kutoa maoni bila kujali athari za jinsi wanavyojieleza kwa jamii,  kama wanajenga au wanachafua nchi, kwa kuhusisha masuala mbalimbali.

Watu wengi hivi sasa wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kutoa maoni yao mengi ambayo wakati mwingine husababisha madhara kwa jamii na matatizo mengineyo bila kutarajia.

Nao baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia vibaya haki hiyo. Watu hao wamekuwa wakikosoa masuala mbalimbali ya nchi bila kutumia njia zenye staha. Hali hiyo inaweza kusababisha chuki kwenye jamii na kuchafua taswira ya nchi kimataifa.

Kwa hiyo ingawa kuna haki ya uhuru wa mawazo, ni vema kila mmoja aangalie madhara ya maoni yake kwenye jamii. Uhuru wa kutoa mawazo usitumike vibaya kwani ukitumika vibaya mfano kwenye mitandao ya kijamii, huzusha manung’uniko mengi katika jamii na kuleta hisia mbaya baina ya makundi mbalimbali.

Kwa hiyo, kila mtu anastahili kuwa na haki ya uhuru wa mawazo, lakini ni vyema fursa hiyo itumike vizuri katika ngazi zote. Watu wakumbuke kuwa nafasi ya uhuru wa kujieleza ikitumika vibaya, inaweza kuleta mifarakano na madhara mengine mengi katika jamii.

UKABILA ni tatizo linalozitafuna baadhi ya nchi za Jumuiya ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi