loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake wajasiriamali changamkieni tuzo zenu

CHAMA cha Wanawake wenye Viwanda na Biashara (TWCC), kimezindua tuzo za wanawake waliofanikiwa kwenye sekta za viwanda na biashara mwaka 2020.

Tuzo hizo zimelenga kuwajengea uwezo zaidi wanawake wajasiriamali, ambao ni wanachama na wasiokuwa wanachama wa TWCC na zitatolewa Novemba 28 mwaka huu.

Ifahamike kuwa tuzo ni utambulisho wa heshima anayopewa mtu, ikiwa ni ishara ya kutambua na kupongeza jitihada zake katika kitu husika anachokifanya.

Hivyo tuzo za mwaka huu za TWCC, zimelenga kutambua na kuwaheshimu wanawake waliofanikiwa na wanaochipukia katika sekta za viwanda na biashara, kama alivyobainisha Mwenyekiti wa TWCC, Jacquline Maleko.

Binafsi ninaunga mkono jitihada kama hizi, zinazofanywa na wanawake hawa wa TWCC katika kuzienzi harakati za wanawake wenzao katika sekta ya biashara.

Hakika wanawatia moyo wanawake wenzao na pia wanawatangaza. Ni muda sasa kwa wanawake wenyewe, kuhakikisha kuwa wanachangamkia tuzo hizo kwa kila namna kwa kushiriki kikamilifu.

Ninaposema kuzichangamkia kwa kila namna, ninamaanisha kuwa wasiishie kushiriki wachache wenye taarifa, lakini wao wenyewe wanalo jukumu la kusambaza taarifa za tuzo hizo kwa umbali zaidi hadi wanawake wenzao ambao wanawaona wanastahili kushinda ila hawana taarifa za tuzo hizo, nao wawezeshwe kushiriki.

Mfano mzuri ni kuwa fomu za ushiriki zinapatikana katika tovuti ya TWCC, ofisi za serikali za mikoa, halmashauri, ofisi za TWCC za mikoa mbalimbali na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), lakini inawezekana wawepo wanawake ambao ni wajasiriamali, lakini hawana hizo taarifa.

Kwa kuwa mwisho wa kujaza na kurejesha tuzo ni Oktoba 9, nawakumbusha wanawake kukimbizana na muda huu, kwa kujaza fomu husika mapema na kuziwasilisha kwa kamati husika.

Kwa kuwa siku ya utoaji wa tuzo hizo, itaambatana na uzinduzi wa Jarida la Wanawake 100 Wajasiriamali Waliothubutu, litakalotumika kutangaza kazi mbalimbali za wanawake wajasiriamali nchini, napenda kuisihi kamati ya habari inayohusika na kuandikia makala za wanawake wenye mafanikio, ihakikishe inawafikia wanawake waliopo vijijini waliopata mafanikio katika viwanda na biashara na kuwaandikia.

Hakika, kama tuzo hizo zitafanyika kwa ufanisi, zitajenga imani juu ya ujasiriamali na kuhamasisha wanawake wa vizazi vijavyo kuwekeza na kujishughulisha katika shughuli za viwanda na biashara.

Kwa kuwa mwanamke ni nguzo muhimu katika maendeleo ya jamii, tuzo hizo zitumike kuonesha mchango wa mwanamke mjasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na kuchochea maendeleo ya jamii, kwa kuwa wanawake wana uwezo wa kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara, endapo wataaminiwa na kupewa nafasi ya kufanya hivyo.

Kwa kuwa serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ambapo wanawake wengi wameweza kuanzisha biashara na viwanda vidogo ambavyo vimewaongezea kipato, kuzalisha ajira na kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi, naishauri TWCC kuwa katika tuzo hizo kuwepo kwa tuzo maalum, inayotambua mchango wa serikali katika shughuli zao hizo.

UKABILA ni tatizo linalozitafuna baadhi ya nchi za Jumuiya ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments