loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

EU waombwa kufungua mipaka kama Tanzania

JUMUIYA ya Nchi za Afrika, Carribean na Pacifi c (OACPS) imetoa mwito kwa Umoja wa Ulaya (EU) kuondoa vizuizi vya kusafi ri kwa baadhi ya nchi hizo, hasa zilizoonesha kuwa salama zaidi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona kama ilivyofanya Tanzania.

Aidha, OACPS na EU zimejadili mikakati inayolenga kupunguza, kufuta au kubadilisha masharti ya ulipaji wa madeni ya nchi zao.

OACPS imetaka EU kusogeza mbele utekelezaji wa baadhi ya kanuni na taratibu mpya za biashara, zilizopangwa kuanza kutumika mwakani kuzipa nafasi nchi hizo kujipanga zaidi kabla ya kuanza kuzitumia.

Mwito huo ulitolewa katika kikao maalumu cha mashauriano baina ya OACPS na Ujerumani, ambayo kwa sasa ni Rais wa Baraza la EU. Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, jijini Dodoma, ilieleza kuwa kikao hicho kilichofanyika Septemba 9 katika ofisi za jumuiya hiyo Brussels nchini Ubelgiji.

Ujerumani imeonesha nia ya kufanyia kazi mapendekezo hayo ya OACPS. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashauriano hayo yaliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi wa Tanzania EU ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa OACPS walioko Brussels, Jestas Nyamanga.

Ujumbe wa Ujerumani uliongozwa na Waziri wa Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dk Gerd Muller.

“Katika kikao hicho wajumbe walisisitiza umuhimu wa Umoja wa Ulaya kuendelea kuunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kusimamia ithibati za tafiti za chanjo za ugonjwa wa virusi vya corona na shirika hilo kuendelea kujengewa uwezo wa kusimamia utaratibu wa kuhakikisha kuwa chanjo itakayothibitika inawafikia mataifa yote kwa usawa na kwa gharama nafuu,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao hicho kilijadili pia hatua zinazopaswa kuongeza msukumo kwa EU katika kuzisaidia nchi za OACPS, kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na ugonjwa wa Covid-19 hususan sekta za utalii na kilimo.

“Mikakati iliyojadiliwa ni ile inayolenga kupunguza, kufuta au kubadilisha masharti ya ulipaji wa madeni ya nchi za Jumuiya ya OACPS na wito wa nchi za OACPS kuitaka EU kusogeza mbele utekelezaji wa baadhi ya kanuni na taratibu mpya za biashara zilizopangwa kuanza kutumika mwanzoni mwa mwaka ujao ili kuzipa nafasi nchi hizo kujipanga zaidi kabla ya kuanza kutumia kanuni hizo,” ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa kupitia mashauriano hayo, pande zote zilitathmini mwenendo wa majadiliano ya mkataba mpya wa ubia wa ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi za OACPS na EU yanayoendelea hivi sasa baada ya mkataba wa sasa kufikia kikomo Desemba mwaka huu.

Aidha, ilieleza kuwa pande hizo mbili zilijadili kwa kina namna ya kushirikiana katika maeneo yanayolenga kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo, uwiano ulio sawa katika biashara na maendeleo ya teknolojia katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilisema katika kipindi hiki ambacho inashika nafasi ya Rais wa Baraza la Mawaziri wa nchi 79 wanachama wa OACPS, itaendelea kushirikiana na EU na kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Ujerumani kwenye Baraza la Umoja huo wa Ulaya kusukuma ajenda zenye manufaa na maslahi kwa pande zote.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi