loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ustaadh, Kibira wanastahili kuenziwa

TASNIA ya michezo Tanzania imegubikwa na wingu zito baada ya kuwapoteza manguli wawili kwenye michezo tofauti, ambao walikuwa chachu ya maendeleo.

 Upande wa masumbwi  bado wanaendelea kumlilia aliyekuwa Rais  wa Kamisheni  za Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO), Yassin  Mwaipaya  ‘Ustaadh’aliyefariki Jumatatu  iliyopita baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa moyo.

 Ustaadh  aliyejizolea umaarufu kwenye mchezo huo kwa kupigania haki za mabondia kuhakikisha wanapata  haki zao, aliongoza chama  hicho chini ya vyama vingi kabla ya kuungana na sasa kuitwa (TPBRC) iliyokuwa chini ya Rais Joe Anea, ambaye baadaye aliyejiuzulu.

Ustaadh anakumbukwa  na ataendelea kubaki alama kwa baadhi ya mabondia kwani aliwafungulia milango kwenda kucheza mapambano nje ya Tanzania kwa kuwakatia tiketi ya kusafiri.

Pia alikuwa muandaaji wa mapambano makubwa, yote hayo alifanya lengo likiwa ni kuona watanzania wanafanikiwa na mchezo huo unapata heshima inayostahiki kama michezo mingine inayopendwa duniani.

Tukio la kumpoteza nguli huyo limetokea siku chache baada ya kumpoteza  aliyekuwa Mwenyekiti  wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Anna Kibira aliyefariki kwa kusumbuliwa na maradhi ya presha yaliyosababisha kupooza.

Kibira aliyekuwa mwenyekiti wa  chama hicho kabla ya uongozi wa sasa kuingia madarakani, wakati wa kipindi cha utawala wake alitoa mchango mkubwa  kimaendeleo kwenye tasnia ya mchezo huo ambao kimsingi utaendelea kukumbukwa na kizazi kijacho.

Manguli hao walikuwa wanajua mengi  ambayo bado jamii ya wanamichezo wa kizazi hiki  tulikuwa tunategemea kujifunza  kutoka kwao, lakini wametangulia mbele ya haki.

Kipindi cha uhai wao walikuwa wanafanya mengi ambayo yalikuwa msaada kuendeleza michezo hiyo, na tulivyokuwa tunapata shida au changamoto  wakati mwingine tulikuwa na utamaduni wa kuwakimbilia kupokea ushauri wao. 

Sasa wameondoka na ninavyojua tulivyo Watanzania sidhani kama kuna watu walikuwa wanatumia uwepo wao kwenda kujifunza mambo mbalimbali.

Ni wazi hata historia zao licha kuandikwa sana kwenye magazeti sidhani kama wameacha vitabu ili kuviwezesha vizazi vya sasa kujifunza kupitia katika vitabu hivyo.

Ni wakati wa kujifunza sasa manguli wetu tuliokuwa tunawategemea wameanza kutangulia mbele ya haki kwa kila chama kuanza kutengeneza maktaba ya kumbukumbu  ya kusimamia kwa kila anayefanya jambo kubwa kuandika historia yake.

Kufanya hivyo, sio kupoteza muda kwani itakuwa faida kwa kizazi kijacho kwa kufanya rejea ya maendeleo ya mchezo husika lakini pili itakuwa chanzo cha mapato kwani kama wataandika vitabu kuna watu watanunua na faida itaenda kunufaisha chama.

Kwa sasa dunia imekuwa kijiji sio vibaya kukubali kujifunza kutoka kwa watu wengine walivyofanya mfano hai Benjamin Mkapa Rais wa Tanzania wa awamu ya tatu amefariki na ameacha kitabu ‘My Life My Purpose’   kinachoelezea kumbukumbu ya maisha yake.

Manguli wote waliofanya makubwa wanatakiwa kupewa heshima kwa kuenziwa na kuheshimu makubwa waliyofanya licha ya kwamba wamepambana kikamilifu na kuondoka bila kuonja ladha ya mafanikio.

Ustaadh, Kibira tutawakumbuka.

UKABILA ni tatizo linalozitafuna baadhi ya nchi za Jumuiya ya ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi