loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wapinzani wakubali mafanikio ya CCM kiaina

VYAMA vya siasa vimeendelea kunadi sera zake vikiomba kuidhinishwa na wananchi kuongoza nchi, huku baadhi ya vyama vya upinzani kupitia ilani zake vikidhihirisha kukubali kiaina mambo yaliyotekelezwa na serikali ya awamu ya tano. 

Aidha, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejikita kuelezea mafanikio yaliyofanywa na serikali ya Awamu ya Tano hatua ambayo imekuwa ikitoa majibu ya baadhi ya hoja zilizomo kwenye ilani za vyama vya upinzani, kupitia majukwaa tofauti ikiwamo mikutano ya kampeni.  

Miongoni mwa maeneo ambayo CCM kinajivunia kufanya vizuri huku vyama tofauti vya upinzani vikieleza mipango ya kuyaendeleza, ni utoaji elimu bure, maendeleo vijijini,  utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. 

Mengine ni utekelezaji wa  ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Mradi wa Kufua Umeme wa Nyerere katika maporoko ya Mto Rufiji (NHPP), kufufuliwa kwa kampuni ya ndege (ATCL), ujenzi wa zahanati, barabara, madaraja ya juu na ya kawaida, uundwaji wa meli na vivuko na kurejesha nidhamu Serikalini.

ACT WAZALENDO

Ilani ya Chama cha ACT Wazalendo inatambua miundombinu ni nyenzo ya kufikia maendeleo hivyo kimeahidi kuendeleza  juhudi za kufufua reli ya kati. Kimesema kitafanya uchambuzi wa kina kwa miradi inayoendelea sasa kama vile SGR, NHPP na ufufuaji wa ATCL.

“Kwa kutumia wataalamu wa ndani na wa nje, serikali yetu itapata ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kutekeleza miradi mikubwa kwa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, kwa kuzingatia muda wa miradi husika kuanza kuzalisha mapato ya kulipia madeni ya ununuzi/ujenzi wake,” inasema sehemu ya ilani. 

CUF 

Kwa upande wa ilani ya Chama cha Wananchi  (CUF), inasema miradi mikubwa iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ikiwamo ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge na ufuaji wa umeme wa Mto Rufiji, itatafutiwa fedha za uhakika za kuigharimia kutoka Benki ya Maendeleo ya BRICS na taasisi nyingine za kimataifa.

CUF ambacho mgombea wake wa urais ni Profesa Ibrahim Lipumba, kinakiri kwamba mafaniko ya kiuchumi kwa taifa lolote hutegemea mfumo wa kisera na uwekezaji wa serikali katika sekta muhimu. 

Kimesema kitahakikisha mawasiliano ya barabara na reli yanakuwa miongoni mwa mambo yanayoendelea kupewa umuhimu wa kipekee huku kikiahidi kutenga fedha za kutosha kukarabati na kujenga barabara na reli mpya. 

Kinaunga mkono ukusanyaji kodi kikisema, kulipa kodi ni wajibu wa kila mwananchi mwenye uwezo wa kiuchumi hivyo kitaongeza ukusanyaji wa kodi kutoka wastani wa asilimia 12.1 kwa mwaka katika kipindi cha awamu ya tano na kufikia asilimia 17 mwaka 2024/25. 

 

Vile vile CUF kinaunga mkono elimu bure kikisisitiza kuwa kitapiga marufuku michango ya aina zote na huduma  zinazotakiwa katika elimu ya msingi zinakuwa jukumu la serikali. 

 

CHADEMA 

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika kuboresha uwekezaji kwenye usafiri wa nchi kavu, majini na anga,  kinasema kitaboresha na kupanua mtandao wa reli kwa ajili ya abiria na mizigo nchini na kuunganisha mtandao huo katika nchi zinazopakana na Tanzania.  

Chadema kinakiri kwamba mfumo wa uchukuzi ulioboreshwa utaongeza ajira zenye kipato na pia kuboresha sekta nyingine zinazoambatana kama vile hoteli, utalii, ujenzi na shughuli nyingine mbalimbali za kiuchumi na kijamii. 

CCM

Wakati vyama vya upinzani vikiendelea kunadi sera na kuahidi mambo mbalimbali vitakavyowafanyia Watanzania, CCM imeendelea kunadi mafanikio ya serikali na kuahidi kufanya makubwa zaidi kupitia ilani ya 2020-2025. 

 “Ilani hii inalenga kuendeleza mafanikio  yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015,” inasema. 

Mafanikio hayo ni pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati yenye tija kubwa katika uchumi na ustawi wa jamii ikiwamo mradi RHPP, SGR, kufufuliwa kwa ATC kwa kununua ndege mpya 11, kununua meli mbili mpya Zanzibar na ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume;

Mengine ni kuimarisha mfumo wa udhibiti, usimamizi na umiliki wa madini na hivyo kuongeza mapato yatokanayo na mazao ya madini kutoka Sh bilioni 168 mwaka 2015 hadi  Sh bilioni 346 mwaka 2019. 

Ilani inataja mafanikio mengine ni kuendelea kupiga hatua za maendeleo katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa, kukua kwa kasi kwa uchumi na kuimarika kwa ustawi wa jamii. “Tanzania ni miongoni mwa nchi kumi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika na hivyo kuwezesha kufikia nchi ya uchumi wa kati,” inasema ilani. 

TIMU ya  Simba imethibitisha kiungo  wake Mbrazili Gerson Fraga ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi