loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi anguruma Zanzibar

MGOMBEA Urais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi ameainisha vipaumbele atakavyovifanyia kazi baada ya kuchaguliwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar ikiwamo ya kutengeneza ajira 300,000.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu zilizohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Demokrasia uliopo Kibandamaiti, mjini Zanzibar, Dk Mwinyi amewataka wanaotafsiri upole wake kuwa ni udhaifu wafahamu kwamba ipo siku watamuelewa.

Uzinduzi huo uliofanywa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Makamu wa Rais mstaafu, Gharib Bilal.

Vipaumbele

Dk Mwinyi alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kukuza uchumi; kukuza utalii; miundombinu bora; viwanda; kutengeneza ajira 300,000 na kilimo.

Alisema ataweka mkazo kwenye uchumi wa bluu yaani bahari kwa kuipa kipaumbele cha pekee sekta ya uvuvi .

“Katika uchumi wa bluu pia tutaweka mkazo kwenye uchumi wa mafuta na gesi. Hapa tutahakikisha tunasimamia mikataba vizuri kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar, tutahakikisha kazi zinazoweza kufanywa na wazawa hawapewi wageni kwenye kampuni za mafuta na gesi, tutasimamia sheria na sera ili Wazanzibari washiriki kikamilifu kwenye uchumi huu,”alisema Dk Mwinyi.

Kwenye miundombinu, atafanikisha bandari ya kisasa, umeme, barabara za lami, maji na huduma bora za jamii. Bandari itakuwa na uwezo wa kupokea kontena nyingi,  kupokea mizigo ya mafuta, mizigo ya meli za kitalii na mizigo ya uvuvi ili kutosheleza ukuaji wa uchumi anaotarajia kuujenga.

Aidha atahakikisha Zanzibar inapata vyanzo vipya vya kuzalisha umeme, wananchi wanapata nishati hiyo kwa uhakika na gharama nafuu, pia kujenga barabara za lami zenye jumla ya kilometa 198.

Serikali yake itajikita kwenye ujenzi wa viwanda na ajira 300,000 kwa vijana zitapatikana. Ataimarisha, kilimo, amani na utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa, utawala bora na uwajibikaji. Vile vile atapambana dhidi ya maovu ikiwamo unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto, dawa za kulevya, dhuluma na uonevu.

Aliwataka watumishi wa serikali kufanya kazi kwa bidii na kutimiza wajibu wao kwa kuongeza ufanisi wa kazi  akiahidi kuwa, hatawavumilia wafanyakazi wazembe na wabadhirifu pamoja na wala rushwa.

“Upole wangu si udhaifu....natoa onyo kwa watumishi wa serikali ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao wajue nitawashughulikia mara moja”alisema.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mchakato wa utafutaji wa mafuta na gesi ambapo aliahidi kama rasilimali hiyo itapatikana atahakikisha mikataba itakayofungwa inakuwa na maslahi kwa taifa.

 “Mafuta na gesi yakipatikana, nitahakikisha yanawanufaisha wananchi wote kwa maslahi ya taifa,''alisema.

 

Dk Shein amnadi

Awali,  Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk Shein alimnadi Dk Mwinyi kwa wananchi kwa kumwombea kura nyingi kwa kuwa ana sifa za kuwa Rais wa Zanzibar, ana uwezo wa kuongoza, ana heshima, mtulivu, mwadilifu, daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu.

“Nawaomba wananchi msijemkafanya makosa kwa kumpa uongozi mtu asiye na uwezo na mwenye malengo binafsi, uchaguzi hautaki utani, tusifanye mzaha, nawaombea kura wote, Dk Mwinyi, Rais John Magufuli, wabunge, wawakilishi na madiwani, naomba Oktoba 28 tukapige kura kwa dhati ili CCM ishinde,”alisema Dk Shein.

Alisema Dk Mwinyi ndiye kiongozi atakayelinda muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu anaufahamu kikamilifu pamoja na mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964.

 

foto
Mwandishi: Martein Kayera na Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi