loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga, Mbeya City kutifuana leo

MABINGWA wa kihistoria Yanga leo wanashuka dimbani kuwakabili Mbeya City katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu soka Tanzania utakaochezwa kwenye dimba la Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo uliopita, Yanga walilazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye uwanja huo,  mchezo wa ufunguzi dhidi ya Tanzania Prisons.

Yanga ikiwa na safu yake kali ya ushambuliaji inayoongozwa na Michael Sarpong itakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha inafunga mabao ya kutosha dhidi ya Mbeya City, ambayo ilifungwa 4-0 dhidi ya KMC.

Mbeya City wataingia katika mchezo huo wakiwa bado wana kiwewe cha kupokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa KMC katika mchezo wao wa kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru.

Katika mechi mbili za msimu uliopita zilizokutanisha timu hizi, hazikutoa mbabe, mchezo wa kwanza ulipigwa Desemba 24, 2019 katika dimba la Sokoine ulimalizika kwa suluhu na wa pili uliopigwa Uwanja wa Mkapa (wakati huo Taifa), Februari 11, 2020 ulimalizika kwa kufungana 1-1.

Mbali na mchezo huo wa Yanga dhidi ya Mbeya City, kutakuwa na mingine itakayochezwa kwenye viwanja tofauti.

Wageni wa ligi Ihefu FC baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Simba SC, watakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kupambana na Ruvu Shooting waliotoka suluhu na Mtibwa Sugar katika mchezo wao uliopita.

Biashara United walioshinda bao 1-0 katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Gwambina watakuwa kwenye dimba lao la nyumbani la Karume kuwaalika Mwadui FC waliopokea kipigo cha bao 1-0 katika mchezo wao uliopita.

foto
Mwandishi: Mohammed Mdose

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi