loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Unapotumia vipodozi hatarishi jiandae kwa hasara mara mbili

VIPODOZI ni kitu chochote ambacho kinatumika katika kupaka, kupulizia au kujifukiza katika mwili wa binadamu kwa lengo la kusafi sha, kuboresha mwonekano na kumfanya mtu awe tofauti na hali yake ya asili.

Zipo malighafi nyingi zinazotumika kutengenezea vipodozi, lakini vipo viambato ambavyo haviruhusiwi kutumika kwenye uzalishaji wa vipodozi hivyo.

Viambato hivyo vimekuwa vikitumika kwa kuchanganywa kwenye vipodozi ikiwemo mafuta ya kupaka mwili hali inayosababisha kubadilisha rangi ya mwili.

Vipodozi vingi vinavyotumika kupakwa kwenye ngozi ya binadamu kwa kiasi kikubwa vinasababisha madhara katika mwili na wakati mwingine kusababisha maradhi ikiwemo saratani.

Vipo viambato ambavyo vimepigwa marufuku na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lenye dhima ya kusimamia ubora na usalama wa vipodozi vinavyoingizwa nchini.

Kutokana na juhudi zinazofanywa na TBS kwa kutoa elimu mara kwa mara kwa watumiaji na wauzaji wa vipodozi imesaidia vipodozi vingi ambavyo havikidhi viwango kutoingia sokoni.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa ili kudhibiti vipodozi hivyo, Mratibu wa Usajili wa Majengo na Bidhaa za Chakula na Vipodozi wa TBS, Moses Mbambe, anasema shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi ikiwemo maonesho ya Sabasaba na Nanenane.

Anasema wameandaa pia programu mbalimbali za kupita katika shule na vyuo ili kutoa elimu juu ya matumizi ya vipodozi hatarishi. “Utoaji wa elimu juu ya matumizi sahihi ya vipodozi kwa kiasi kikubwa yanaokoa maisha ya kesho kwa watu wengi wakiwemo watoto,” anasema Mbambe.

Mbambe anasema TBS imekuwa ikifanya ukaguzi za kushtukiza kwa wauzaji na wasambazaji wa biashara ya vipodozi ili kuwaelimisha matumizi sahihi ya bidhaa hizo.

“Mara nyingi wafanyabiashara hao wanaouza vipodozi hushauriwa kuuza vipodozi ambavyo vina alama ya ubora ya TBS na kuwapatia orodha ya vipodozi vyenye viambato sumu ambavyo hawatakiwi kuviuza,” anasema Mbambe na kuongeza; Kwa mujibu wa Mbambe, tafiti mbalimbali zimebainisha kuwa kuna zaidi ya asilimia 52 ya wanawake wanaotumia vipodozi mbalimbali vyenye viambato vya sumu ambavyo vinaweza kusababishia matatizo katika afya ya binadamu.

Anataja miongoni mwa magonjwa yanayoweza kutokea baada ya kutumia vipodozi vyenye viambato sumu kuwa ni pamoja na ugonjwa wa saratani ya ngozi, figo pamoja na kutoshika ama kuharibika kwa mimba.

Mbambe anasema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2011 zilionesha kwamba asilimia 40 ya wanawake barani Afrika hupausha ngozi zao kutokana na matumizi ya vipodozi vyenye viambato sumu.

“Katika mataifa mengine idadi hiyo ni ya juu kwani hufikia hadi asilimia 77 ya wanawake. Mfano Nigeria, Togo, wanawake wanaopausha ngozi kwa matumizi ya vipodozi hivyo ni kwa kiwango cha asilimia 59, Afrika Kusini ni asilimia 35, Senegal asilimia 27 huku Mali ikiwa na asilimia 25,” anasema.

Anafafanua kwamba matumizi ya muda mrefu ya vipodozi vyenye viambato vya sumu husababisha utegemezi au uraibu kwani ngozi hurejelea rangi ya asili pale matumizi yanapositishwa.

Akichambua madhara ya kila kipodozi chenye viambato sumu, Mbambe anasema vipodozi vyenye Hexachloraphene mtumiaji akijipaka hupenya kwenye ngozi na kuingia kwenye mishipa ya fahamu hasa kichwani.

Pia anasema husababisha ugonjwa wa ngozi na kuathiri ngozi pindi mtumiaji anapokuwa kwenye mwanga na vile vile inakuwa laini na kusababisha kupata ugonjwa kama fangasi au maambukizi ya vimelea vya maradhi.

Kwa mujibu Mbambe ,miongoni mwa vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini ni krimu na losheni zenye kiambato cha hydroquinone, losheni na sabuni zenye kiambato hicho.

Vingine ni sabuni zenye kiambato cha zebaki (mercury), krimu zenye kiambato cha zebaki na michanganyiko yake pamoja na kipodozi cha kupunguza unene chenye kiambato cha mmea (Phytolacea Spp).

Mbambe anasema vipodozi hivyo vinavyotokana na mmea wa ‘Arctostaphylos Uva URSI (bearberry extract) vyenye viambato vya “hydroquinone na abutin ambavyo ni sampuli zipatazo tano na vipodozi vyenye kiambato cha tin oxide kinachosababisha muwasho kikitumiwa karibu na eneo la jicho ni hatari sana kiafya.

Anataja vipodozi vingine ni vile vyenye kiambato cha Malic acid, ambacho kinachobabua cell za ngozi na kusababisha weupe, mfano Aha Whitening Cream.

“Vingine ni vipodozi vya kuzuia harufu (Antiperspirant) vilivyo na Aluminum Zirconium Compound mfano Triplc Dry Antiperspirant. Vingine ni krimu zenye misuguano (hormones in steroids), jeli zenye “steroids” na vipodozi vingine vyenye kiambato sumu cha hydroquinone & steroid na vingine.” Kwa vipodozi vyenye zebaki, Mbambe anasema husababisha madhara ya ngozi, ubongo, figo na kwenye viungo mbalimbali vya mwili.

“Zebaki inapopakwa kwenye ngozi huweza kupenya taratibu ndani ya mwili na kusababisha sumu yake kuingia kwenye damu, hivyo kuleta madhara mengi mwilini,” anasema Mbambe.

Anaongeza: “Mjamzito akitumia vipodozi vyenye zebaki mtoto huathirika akiwa bado tumboni na huzaliwa akiwa na mtindio wa ubongo.” Lakini pia anasema vipodozi hivyo husababisha ngozi kuwa laini na yenye mabaka meusi na meupe na kwamba husababisha mzio wa ngozi na muwasho.

Kuhusu kiambato chenye steroids, Mbambe anasema hilo ni kundi la homoni. “Homoni hizi hutengenezwa kwenye miili ya binadamu na wanyama, pia zinaweza kutengenezwa nje ya mwili wa binadamu (artificial hormones).

Corticosteroids ndizo hutumika sana kama viambato kwenye vipodozi,” anasema Mbambe. Anazidi kufafanua kwamba steroids zikitumika kwa muda mrefu husababisha madhara mbalimbali kama ugonjwa wa ngozi na kutokwa kwa chunusi kubwa.

“Pia ngozi huwa nyembamba sana na laini na endapo itapata jeraha au kufanyiwa upasuaji, kidonda hakitapona. Pia husababisha magonjwa ya moyo,” anasema Mbambe. Kwa upande wa vipodozi vyenye chroloform, mtaalamu huyo anasema husababisha kansa ya utumbo mpana na kibofu cha mkojo.

Kadhalika anasema husababisha pia ugonjwa wa akili na ule wa mishipa ya fahamu. Kwa mujibu wa Mbambe chroloform husababisha ngozi kuungua, maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu sana na kutokwa na vipele.

Akizungumzia vipodozi vyenye viambato vya chlorofluorocarbon (halogenated chlorofiuoroaikanes) anasema hivyo husababisha madhara kwenye mishipa ya katikati ya fahamu na hivyo kusababisha mtu kutopumua vizuri.

“Lakini pia husababisha kichefuchefu, kutapika, kuumwa kichwa, kusikia usingizi na kusikia kuzunguzungu,” anasema Mbambe. Kuhusu methylene chloride anasema husababisha saratani, madhara kwenye mishipa ya kati ya fahamu, kwenye maini na kwenye mishipa ya moyo.

Kwa upande wa matumizi ya vipodozi vyenye kiambato cha bithionol, Mbambe anafafanua kuwa athari zake ni kupata mzio wa ngozi na athari

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments