loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uchakataji korosho utakavyoleta neema kwa taifa

MLIPUKO wa ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona umeleta kizaazaa katika masoko mengi duniani, ikiwamo soko la korosho.

Pamoja na kusababisha bei ya korosho ghafi na korosho karanga kuwa za chini, matokeo yake yanatoa haja ya kuwapo na umuhimu wa pekee wa kufuatilia uchakataji wa zao hilo ili kutanua wigo wake kisoko.

Kwa kuwa bei ya korosho ghafi katika soko la dunia inategemea sana mwenendo wa bei  ya korosho karanga ni dhahiri Covid-19 imesababisha kupungua kwa mauzo yake kutokana na kupungua  kwa ulaji katika masoko makuu ya India, Vietnam pamoja na masoko ya China, Ulaya, Marekani na Mashariki ya Kati.

Aidha bei ya korosho karanga nchini India na Vietnam kwa madaraja mbalimbali ilishuka kwa kiasi kidogo kuanzia Machi hadi Julai 2020 ukilinganisha na mwezi Machi hadi Julai mwaka 2019 na kuleta kizaazaa katika soko la korosho ghafi.

Dk Fotunatus Kapinga wa kituo cha utafiti wa Kilimo cha Naliendele, Mtwara, anasema kutokana na covid-19 wamebaini kwamba wakati umefika kwa watanzania kujifunza na kuzalisha kwa kasi korosho ghafi si kwa kwenda kuziuza zilivyo bali kuzichakata ili kupata mahitaji mbalimbali ambayo yatasaidia bei ya korosho na mazao mengine mtambuka kuwa juu na kufaidisha jamii na taifa kwa ujumla.

Dk Kapinga anasema matumizi ya mazao ya korosho hapa nchini ni madogo sana kulinganisha na mahitaji halisi.

Anasema hapa nchini korosho ghafi inapewa kipaumbele kuliko mabibo ambayo yanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwamo juisi.

“Kwenye korosho ghafi tunachothamini ni korosho karanga ambazo kwa uzito ni wastani wa asilimia 20-25 tu ya korosho ghafi,” anasema Dk Kapinga na kuongeza kwamba ngozi laini (testa) ambayo ni asilimia 2 na maganda ambayo ni asilimia 75-80 ya uzito wa korosho ghafi hazihesabiwi kwenye thamani ya korosho.

Anasema kiujumla kuna matumizi madogo ya mazao ya korosho hapa nchini na kufanya kutegemea zaidi mauzo ya korosho ghafi ambayo kwa sasa soko lake limeyumba.

Anasema kwenye korosho pia kuna mafuta ya maganda (CNSL) ambayo hatuyatumii na kama kuna matumizi ni madogo huku makapi ya maganda yakiwa hayatumiki ipasavyo pia kwani kimsingi ni chakula kizuri kwa mifugo.

Dk Kapinga anasema uhamasishaji wa matumizi ya korosho nchini ni mdogo, ambapo kazi wanazofanya sasa wao kama Naliendele ni kuonesha kwamba inawezekana kuwa na soko kubwa la korosho nchini na hivyo kuwapo na haja ya upanuzi wa kilimo chenyewe kutokana na ukubwa wa mnyororo wa thamami.

Historia ya zao hili inaanzia karne ya 16 wakati Wareno walipoleta zao hilo Afrika Mashariki, si kwa sababu ya kupata matunda yake bali kwa sababu ya kuzuia mmomonyoko wa ardhi.

Kutokana na hali hiyo halikuangaliwa kama zao la biashara.

Akielezea kiundani zaidi kuhusu korosho Tanzania, Mratibu wa zao la korosho katika kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari-Naliendele), Dk Geradina Mzena anasema kwamba korosho zilianza kupandwa kwa wingi nchini Tanzania baada ya vita kuu ya pili ya dunia na kuendelea kuongezeka katika miaka ya sitini na uzalishaji kuongezeka kutoka tani 8,000 mwaka 1945 hadi tani 145,000 mwaka 1973/74.

“Kiwango hiki kilifanya Tanzania kuwa nchi ya pili duniani kuzalisha korosho kwa wingi ikitanguliwa na Msumbiji,” anasema Dk Mzena.

Hata hivyo, zao hilo lilikuja kuporomoka hadi tani 16,400 mwaka 1986/87 kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa ubwiriunga.

Hata hivyo, Dk Mzena anasema ugunduzi wa mbegu zenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa ubwiriunga na ugunduzi wa viuatilifu kutokana na juhudi za taasisi hiyo ilisaidia kufanya uzalishaji kuongezeka kufikia tani 313,000 katika msimu wa 2017/18.

Pamoja na utafiti wa mazao mengine ya mafuta, Tari Naliendele ina jukumu la kitaifa la kufanya utafiti wa zao la korosho nchini na matokeo ya utafiti wao ndio umekuza zao hilo na sasa wanalipa uwezo wa kuchakatwa.

“Katika kuongeza thamani ya zao la korosho, licha ya kubangua tumefanya utafiti na kupata njia za kuongeza thamani ya korosho kwa kutengeneza bidhaa za korosho kama vile siagi, maziwa, mvinyo na jamu,” anasema Dk Kapinga.

Pamoja na kufanikiwa katika tafiti kuanzia utanuaji wa mikoa inayolima korosho, Tari-Naliendele imekuwa na kiwanda kidogo cha kufundishia wakulima namna ya kuchakata zao la korosho.

Msimamizi wa kiwanda cha ubanguaji na uongezaji wa thamani wa zao la korosho katika taasisi ya Tari-Naliendele, Baraka Zebedayo anasema mkorosho una kila kitu kinachofaa kwa chakula na kinywaji kwa mwanadamu.

Anasema kwenye tafiti zao wametengeneza fomula zinazofaa kwa ajili ya mvinyo, juisi na jamu.

“Likiwa freshi linakuwa hai kwa muda mfupi lakini sisi tumefanikiwa kukausha na kukaa nalo kwa muda mrefu. Huku wanaita chokocho. Hili linaweza kutengeneza mvinyo na pia kitakasa mkono,” anasema Baraka.

Anasema si mvinyo pekee lakini pia korosho iliyobanguliwa inaweza kutoa unga wa korosho ambao ukichanganywa na fleva nyingine inaweza kuwa chakula kizuri kwa watoto. Aidha unga huo unaweza kuchanganywa na ngano na kutoa chapati nzuri, andazi na kadhalika.

Pia anasema maziwa ya korosho yanayotolewa katika karanga yana ladha na pia vitamini na protini kama yalivyo maziwa ya ng’ombe.

“Hapa sasa hivi kwa kweli tunatathmini muda wa kukaa katika usafirishaji na pia katika uhai wake. Haya maziwa unaweza kuyatengeneza kuwa mtindi kwa kuwa na virutubisho vinavyotakiwa kutengeneza mtindi,” anasema Baraka.

Lakini pia anasema maziwa hayo yanaweza kuwekwa fleva mbalimbali na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi mtambuko.

Anasema kituo hicho kwa sasa kipo tayari kwa mafunzo na ndio maana wana kiwanda kidogo na wangelipenda wanaotaka kujikita katika kutengeneza bidhaa mbalimbali kwenda kujifunza na kuelekezwa aina ya mashine zinazofaa kwa kazi hizo.

“Tunafanya hivi kwa kuwa korosho ina matumizi mengi na kama wananchi wakichukua bidhaa hizi na kuzitumia maana yake hakuna sababu za kuhangaika na soko la nje, soko la ndani na Afrika Mashariki ni kubwa,” anasema Baraka.

Kuwepo kwa bidhaa tofauti zinazoweza kusaidia kuinua bei ya korosho kumepokewa vyema na wakulima mbalimbali.

Mkulima wa Korosho wa Liwale, Hassan Mpako, anasema wananchi wakijikita katika kupata bidhaa mbalimbali zinazotokana na korosho ni dhahiri matumizi hayo ya ndani yataweka sawa bei ya korosho na kilimo chake kitakuwa na faida kubwa.

“Hiki kilimo tukifundishwa namna ya kutengeneza hizi bidhaa, tukachakata korosho kuanzia bibo hadi korosho karanga, tutakuwa hatuna sababu ya kuwa na kilio cha fedha, fedha ipo humu,” anasema Mpako.

Kwa sasa mikoa inayolima korosho ni 20 na hivyo kufanya katika miaka mitatu ijayo Tanzania kuwa na malighafi ya kutosha kwa bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kemikali inayotumika kutengeneza kutakasa mikono ambayo kwa sasa inaagizwa kutoka nje.

“Kuna ethanol nyingi kutoka katika mabibo na tutakapoweza kuwa na viwanda vidogo na vya kati tunaweza kutengeneza vitakasa mikono vya kwetu wenyewe,” anasema Baraka.

Kwa Dk Kapinga, korosho ni mpango mzima hasa katika kutengeneza ajira kuanzia kwa mkulima, muuzaji, mtengeneza vifungashio, wachakataji na hata wanaolima mazao yanaweza kutumika kama fleva.

Anasema korosho ina virutubisho vingi ikiwamo madini ya chuma, magneziamu, zinki na kadhalika na hata vitamisi C ambayo ni mara tano ya ile iliyomo katika chungwa.

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi