loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli: Tusichezee amani

MGOMBEA Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ametahadharisha Watanzania wasifanye majaribio ya kuchagua, kwani kufanya hivyo ni kucheza na amani.

Amesema tangu enzi wa waasisi wa taifa, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amani Karume kwa Zanzibar hadi sasa, amani na usalama wa nchi vimekuwa vikipewa kipaumbele cha kwanza na Serikali ya CCM.

“Tunaitengeneza nchi kuwa nchi ya kisasa. Nipeni miaka mingine mitano, msifanye majaribio, simuoni katika wagombea urais atakayeweza kutekeleza haya hata kwa robo hayupo.

Kama mnataka kujaribu jaribuni, hayupo, huwezi kusema ubwabwa wakati kwake haupo, unasema mtakula bata wakati hakuna vya bure, Biblia inasema asiyefanya kazi na asile,” alisema Magufuli.

Aliyasema hayo jana katika Uwanja wa Mazaina, Chato, mkoani Geita alipozungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni. Katika mkutano huo, Magufuli pia aliwaombea kura wagombea wa ubunge na udiwani kutoka majimbo yote ya mkoa wa Geita.

“Kamwe msikubali watu wanaokuja kutugawa, kutudanganya, wanaokuja na maneno matamu kumbe ni machungu, watu wanaojifanya wanaijua Tanzania, msikubali Watanzania, tutapotea, majuto huwa ni mjukuu, eti vyama vingi, nini nini, chama hiki (CCM) kiliachwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, akafanya katika kipindi chake akaliongoza taifa tukapata uhuru na kule Zanzibar ni Mzee Karume, wakafanya kwa wakati wao”alisema na kuongeza; “Nchi hii haijawahi kuwa na vita, isipokuwa ya Iddi Amini ambaye alitandikwa kisawaswa alipojaribu kutuchokoza.

Akaja Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) tukapita, akaja Mkapa (Hayati Benjamin) akasema nipeni huyu kijana...huyu ndiye aliyeniokota jalalani, mtu akipewa kazi wanasema ameokotwa jalalani na Magufuli.

Akaja Jakaya Kikwete miaka 10, katika vipindi hivi vyote Tanzania imekuwa nchi ya amani,” alisema. Magufuli alisema katika miaka yote hiyo, Watanzania wamekuwa wakifanya shughuli kwa uhuru, wanatembea, wanaabudu na kuendesha maisha kwa uhuru na kueleza kuwa uhuru huo usije ukawalevya kwani siku zote majuto ni makubwa.

“Ninyi mnafahamu hata katika nchi za jirani, mnakumbuka mauaji ya Rwanda, watu walitembea kwa miguu mpaka Chato, nampongeza Rais Kagame (Paul) alipoingia madarakani Rwanda ina amani.

Msicheze na kukosekana kwa amani, msije mkajaribu kitu ambacho mnakiona ni kitamu wakati ni kichungu”alisema. Aliwataka watanzania wakumbuke walipotoka, walipo na wanapoelekea na wawe imara katika umoja bila kubaguana kwa dini, makabila au vyama.

Magufuli aliomba Oktoba 28 Watanzania wampigie kura, aendelee kubaki madarakani kwa miaka mitano mingine. Aliahidi kufanya maajabu zaidi ya aliyofanya kwa miaka mitano iliyopita.

“Navishukuru sana vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia amani ya nchi yetu. Wakati naingia madarakani palifikia hatua hasa kule maeneo ya Kibiti (Pwani) watu wanauawa, zaidi ya Polisi kumi na kitu waliuawa kwa kupigwa risasi, ndio maana tulisimama imara kwamba ulinzi na usalama wa nchi yetu ndio kipuambele namba moja,” alisema.

Magufuli aliwaeleza wananchi waliofurika kumsikiliza kuwa nchi ikikosa amani, ulinzi na usalama, hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana na hata ujenzi wa shule, vituo vya afya hauwezi kufanyika.

“Ilifikia wakati unatoka Chato kwenda Biharamulo lazima usindikizwe na Polisi, ukitoka Biharamulo kwenda Bukoba ukipita Kasindaga, lazima usindikizwe na Polisi, ukitoka Biharamulo kwenda Ngara pale Mlima wa Simba lazima usindikizwe na Polisi kwasababu ya majambazi.

Tukasema hapana majambazi hawawezi kutawala katika nchi hii, na ndio maana navipongeza sana vyombo vya ulinzi na usalam”alisema. Alisema bila amani watu hawataweza kwenda kanisani wala msikitini, kwa kuwa watakuwa na hofu kwamba majambazi watawavamia ili waibe sadaka.

Aliwaomba wananchi wa Chato kama walivyomuamini katika miaka 20 akawa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 1995 hadi 2015, amejifunza mengi ndio sababu anaomba wamchague yeye, wabunge wa CCM na madiwani ili akamilishe alipoachia.

“Nafahamu kazi ya urais si nyepesi, uzoefu wa miaka ishirini na tano ya uongozi (20 ubunge na mitano urais) nimejifunza mengi, nimeijua Tanzania yote na shida za Watanzania.

Ninyi ni mashahidi nimekuwa kweli mtumishi wa kweli. Mambo yaliofanyika nchi hii ni makubwa sana. Kuongoza panahitaji karama, upendo si kuzungumza tu, ntafanya hivi ntafanya hivi,” alisema Magufuli.

Afya Magufuli alisema kwa miaka mitano, Serikali ya CCM imefanikiwa kujenga zahanati zaidi ya 1,200, vituo vya afya zaidi ya 487, hospitali za wilaya zaidi ya 98, hospitali za mikoa 10, za rufaa tatu na nyingine zinajengwa.

Alisema bajeti ya dawa imeongezeka kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 270 kwa mwaka, huku usambazaji kupitia Bohari ya Dawa (MSD) umeongezeka. Miundombinu Magufuli alisema serikali imeimarisha usafiri wa majini kwa kuwa baada ya meli ya MV Bukoba kuzama mwaka 1996, meli hazikuwa zikionekana tena kwa wingi.

Elimu Kwa upande wa elimu, Magufuli alisema alipoingia madarakani, alikuta shule chache huku akitoa mfano wakati akisoma waliochaguliwa kwenda sekondari ni wawili tu, yeye na mtu mwingine ambaye sasa ni marehemu.

Umeme Magufuli aliwoamba wananchi wa Chato kumchagua tena Dk Medard Kalemani ili akamsaidie kuendeleza miradi ya umeme kwa vijiji 2500 vilivyobaki kote nchini.

Alisema nchi yenye vijiji 12,268 kwa takwimu za jana vyenye umeme ni vijiji 9,700 ikimaanisha kuwa vimebaki vijiji hivyo 2,500 tu kwa nzima.

Viwanja vya Ndege “Mtu anasema nimejenga uwanja nyumbani, nikifa ntaenda na hilo liuwanja kaburini.

Simiyu kiwanja kinajengwa, Singida kinajengwa, Mtwara tunapanua, Dodoma tumepanua mpaka Air bus inatua na tunajenga uwanja mwingine wa kimataifa, hivyo vyote mtu havioni, anaona cha Chato tu, ashindwe na akalegee kweli kweli,” alisema Magufuli.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments