loader
Simba, Yanga mambo bado

Simba, Yanga mambo bado

KWA jinsi msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21 ulivyoanza, ni kama umewabadilikia timu vigogo Simba SC na Yanga SC zilizomaliza kwenye nafasi mbili za juu msimu uliopita.

Simba ambao ndio mabingwa watetezi na Yanga iliyoshika nafasi ya pili, zote zimeshacheza mechi mbili lakini zimeshindwa kuvuna pointi zote sita.

Kati ya timu nne zilizomaliza nafasi za juu msimu uliopita, ni Azam FC pekee ndiyo iliyobeba pointi sita kwenye mechi zake mbili za mwanzo, ikijiweka nafasi ya pili baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Polisi FC na 2-0 mbele ya Coastal Union.

Namungo FC nao hali si shwari kwao. Msimamo kwa sasa unaonesha KMC ndio vinara wakifuatiwa na Azam FC iliyomaliza nafasi ya tatu msimu uliopita, ya tatu ni wageni wa ligi Dodoma Jiji na ya nne ni Biashara United, timu zote hizo zina pointi sita zikitofautiana uwiano wa mabao.

Simba ni ya tano ikifuatiwa na Yanga, zote zina pointi nne, nazo zinatofautiana kwa uwiano wa mabao, zimeshinda mechi moja na sare moja. Namungo ipo nafasi ya tisa imeshinda moja na kufungwa moja.

Pointi nne za Simba zilizopatikana kwenye ushindi mbele ya Ihefu FC na sare kwa Mtibwa Sugar, kwao wanaona sio matokeo mabaya kutokana na mechi zote kucheza ugenini, ambapo mara nyingi viwanja vya mikoani huwa wanavilalamikia kuwanyima wachezaji wao uhuru wa kucheza soka lao la kutandaza mpira.

Kwa Yanga ambao pointi nne wamezipata katika sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Mbeya City, kocha wake, Zlatko Krmpotic, alieleza moja ya sababu ya matokeo hayo ni kutokana na baadhi ya wachezaji wake hasa waliosajiliwa msimu huu kutokuwa kwenye kiwango bora hivyo wanahitaji muda zaidi.

Timu tatu zilizopanda ligi msimu huu mbali na Dodoma iliyo nafasi ya tatu, Ihefu FC ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi tatu, imefungwa moja na kushinda moja, Gwambina ya 15 ikiwa na pointi moja, imefungwa moja na sare moja.

Kwa matokeo hayo ya mechi hizo za mwanzo, ni dhahiri ligi ya safari hii itakuwa ngumu na yenye msisimko wa hali ya juu kutokana na kila timu kujipanga vilivyo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/47a31e4aa863c4fbfa54c3b8ff719fae.jpg

ZAIDI ya Vijana 25,000 kutoka ...

foto
Mwandishi: Mohammed Mdose

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi