loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TFF yawafunda wanawake 300 kuongoza soka

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limezindua kozi ya utawala katika soka la wanawake, yenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.

Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kozi hiyo ya siku tano alikuwa Rais wa Shirikisho la Soka Burundi (FFB) na timu ya Eagle Noire, Reverien Ndikuriyo.

Ndikuriyo aliipongeza TFF kwa kuja na mpango huo ambao anatamani uwe endelevu ili kuwaandaa viongozi wanawake watakaoenda kuwashawishi wenzao na jamii kwa ujumla kuanza kufuatilia soka la wanawake.

“Duniani kote wanawake ni wengi, lakini kwenye mechi zao hawajitokezi kwa wingi, nilikuwa Siku ya Mwananchi (Tamasha la Yanga), watu walijitokeza kwa wingi tunataka tuone hivyo pia kwa wanawake,” alisema Ndikuriyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema uzinduzi huo ni tukio la kihistoria kwa maendeleo ya soka la wanawake, kwani kupitia mafunzo hayo wataenda kupata wataalamu wenye weledi.

“Soka la wanawake kwa asilimia kubwa linaongozwa na wanaume, sasa tumekuja na mpango wa kuendesha kozi hii ya utawala kuwajengea uwezo wanawake na kuwaandaa kuja kuwa viongozi wa kusimamia mpira na hata sekta nyingine ikiwamo siasa,” alisema Karia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred, alisema wana amini kupitia kozi hiyo itenda kuchochea maendeleo ya soka la wanawake nchini kama ilivyo upande wa wanaume.

“Masomo ya kozi yanaanza leo (jana) na washiriki wapo 32, itatolewa kwa siku tano kama muongozo wa Shirikisho la Soka la kimataifa (FIFA) unavyoelekeza na baada ya hapo tutakuja na kozi ya makocha,” alisema Kidao.

Naye Mwenyekiti wa Soka la Wanawake nchini, Amina Karuma, alisema kilio na ndoto yao ya muda mrefu sasa inaenda kupata majibu, akieleza kuwa, soka la wanawake haliwezi kupiga hatua kama hakutakuwa na wataalamu wa jinsia hiyo.

“Kama mlivyosikia kozi imezinduliwa na ikimalizika tunaenda kupata wataalamu 300 ambao watasambaa nchi nzima na maarifa wanayopata wataenda kusaidia kuinua mpira wetu,” alisema Amina.

TIMU ya soka ya Mtibwa Sugar imesema mchezo ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi