loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanasiasa na mwito wa kuhubiri amani

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeingia katika kipindi muhimu cha uchaguzi mkuu ambao ni mchakato wa kidemokrasia wenye lengo la kuwawezesha wananchi kuchagua viongozi watakaoshika madaraka katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Suala la kudumisha amani na utulivu bila kuathiriwa na uchaguzi ni jambo ambalo limekuwa likigusa fikra za Watanzania wengi na kusababisha mijadala mbalimbali.

Hofu ya kuvurugika kwa amani kutokana na uchaguzi si kitu kigeni, kwani kimeshayakumba mataifa mengi duniani na hata Tanzania, hususani visiwani, kuliwahi kutokea machafuko ya 2001 yaliyosababishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.

Ni katika muktadha huo, viongozi wa dini Zanzibar walijitokeza hivi karibuni kuandaa kongamano lililowakutanisha wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kwa ajili ya kuitahadharisha jamii kuepuka matukio au maeneo yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu.

Uongozi wa Kanisa la Anglikana Zanzibar kwa kushirikiana na uongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ofisi ya Mufti Zanzibar pamoja na Jeshi la Polisi waliandaa kongamano kubwa lililobeba ujumbe wa uchaguzi mkuu wenye amani.

Kongamano hilo pia lilitumika kuwataka wanasiasa kuhubiri amani katika kipindi cha kampeni za kisiasa katika majukwaa.

Akizungumza katika kongamano hilo, Askofu mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk Michael Hafidh anasema tangu muungano ulipoasisiwa Aprili 26 mwaka 1964, wananchi wa pande zote za muungano wamekuwa wakiishi katika mazingira ya amani na utulivu, hatua ambayo imesaidia kukua kwa uchumi na ustawi wa jamii wa wananchi wake.

Anasema utulivu uliopo nchini kwa kiasi kikubwa umeiwezesha Tanzania kuwa kimbilio la raia mbalimbali wa nchi jirani ambapo nchi zao zimeingia katika vurugu za kisiasa na kuzalisha wakimbizi.

Anawataka wanasiasa kuchunga kauli zao katika kipindi hiki cha kampeni na hatimaye uchaguzi mkuu huku wakihakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na wananchi wanatumia uhuru wao wa demokrasia kuchagua viongozi wanaowataka.

“Watanzania wakiwemo wanasiasa tuendelee kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki. Tuendeshe kampeni katika mikutano ya hadhara kwa utulivu. Vurugu zikiibuka hata ndege wakisikia milio ya bunduki wanakimbia kwa sababu wanajua hapa amani imevurugika,” anasema.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Shehe Mziwanda Ngwali anawaomba viongozi wa kisiasa kuchunga ndimi zao katika kipindi hiki muhimu kwa kutumia kauli za kistaarabu, bila kuhamasisha vurugu wala kuwatukana wengine.

Ni kwa mantiki hiyo, anawataka viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia kanuni na masharti ya maadili ya uchaguzi ambayo wametia saini na hivyo kuwa sawa na mkataba unaowawezesha kushiriki katika uchaguzi mkuu.

“Fanyeni kampeni zenu za uchaguzi mkuu huku mkiweka kipaumbele suala la amani na utulivu mbele kwani baada ya uchaguzi wa siku moja yapo maisha ya muda mrefu yatakayoendelea,” anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Hassan Khatib ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo anasema viongozi wa dini wanao wajibu mkubwa wa kuendelea kuhubiri umuhimu wa amani na utulivu kwa wafuasi wao pamoja na kuliombea taifa kufanya uchaguzi mkuu kwa amani.

Anasema mchango wa viongozi wa dini ni mkubwa kwa sababu wanakubalika kwa kiasi kikubwa mbele ya jamii pamoja na waumini wao wenye imani na itikadi ya vyama mbali mbali vya siasa.

“Nimefurahishwa na uamuzi wenu wa kutayarisha kongamano kubwa kama hili lenye ujumbe wa kuliombea dua Taifa la Tanzania na kuhimiza kufanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu... Nashauri muitumie fursa hii ya kufanya mikutano mingine zaidi kwa ajili ya kuhamasisha amani na utulivu katika kipindi hiki,” anasema.

Mkuu wa upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Obasi Nguvule, anasema wamejipanga vizuri kulinda amani na utulivu pamoja na mali za raia licha ya majukumu makubwa ya kila siku ya jeshi hilo wanayokabiliana nayo.

Anawataka wanasiasa kutumia uwanja wa siasa kwa ajili ya kutoa sera za vyama vyao na kamwe uchaguzi usitumiwe kwa ajili ya kuwagawa wananchi wa Zanzibar.

“Jeshi la polisi lipo kwa ajili ya kulinda amani na utulivu pamoja na mali za raia... Tunafahamu kipindi cha uchaguzi hutumiwa na baadhi ya wanasiasa kujenga chuki na kusababisha joto la jazba za kisiasa, lakini sisi tumekabidhiwa jukumu la kulinda dola na mali za raia,” anasema.

Meneja wa mradi wa Amani Zanzibar ambao unasimamiwa na Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbali mbali pamoja na makanisa mawili ikiwemo Kanisa Katoliki na KTT, Jamali Ali Hussein anasema lengo la mradi huo ni kuona Zanzibar inakuwa salama muda wote.

Hussein anasema mradi huo unawashirikisha wadau mbali mbali kwa ajili ya utekelezaji wake ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mufti pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Anasema suala la amani ndiyo kipaumbele kikubwa cha utekelezaji wa mradi huo kwa sababu bila ya amani hakuna kitu chochote kinachoweza kufanyika ikiwemo ukuaji wa uchumi na maendeleo.

Anawataka wananchi wa Zanzibar katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kudumisha amani kwani watu hawataki kuona damu inamwagika kwa sababu ya kugombea madaraka. “Mwito wangu, tuheshimu vyombo vya dola.

Hatuna sababu ya kumwaga damu katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa sababu uchaguzi ni njia moja wapo ya kudai demokrasia kwa njia ya amani na utulivu,” anasema Hussein.

Mradi wa Amani Zanzibar ulioanza kufanya kazi mwaka 2019 Novemba ni wa miaka sita. Unakusudia kufanya mikutano na makongamano ya amani 18 kwa mwaka huu pekee.

Ni mradi ambao uko chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Umoja wa Majimbo ya Kianglikana Afrika (CAPA).

Katika kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika katika mazingira mazuri ya utulivu, vyama vya siasa Zanzibar vimetia saini makubaliano ya maadili ya uchaguzi mbele ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na msajili wa vyama vya siasa.

Akizungumza katika utiaji saini wa makubaliano ya maadili ya vyama vya siasa katika kufanya kampeni za kistaarabu, Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini, Mohamed Ahmed aliwataka viongozi wa vyama hivyo kutanguliza uzalendo na kuweka maslahi ya taifa mbele.

Alisema sheria za maadili ya uchaguzi lengo lake kubwa ni kuhakikisha vyama vya siasa vinafanya kampeni za kiungwana ambazo zitaweka mbele uzalendo sambamba kudumisha amani na utulivu wa visiwa vya Unguja na Pemba.

“Tupo hapa kutia saini tamko la maadili kwa vyama vya siasa ambalo lengo lake kubwa ni kuhakikisha tunafanya uchaguzi wa amani na utulivu ambapo matamko ya chuki na uhasama kamwe yasipewe nafasi,” alisema.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments