loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Tuilinde amani kwa gharama yoyote

AKIHUTUBIA wananchi juzi kwenye mkutano wa kampeni wilayani Chato mkoani Geita, Rais John Magufuli amewatahadharisha Watanzania kuwa makini na watu wanaoichezea amani nchini.

Rais Magufuli aliwaeleza wananchi waliofurika kumsikiliza kuwa nchi ikikosa amani, ulinzi na usalama, hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana na hata ujenzi wa shule, vituo vya afya hauwezi kufanyika.

“Ilifikia wakati unatoka Chato kwenda Biharamulo lazima usindikizwe na Polisi, ukitoka Biharamulo kwenda Bukoba ukipita Kasindaga, lazima usindikizwe na Polisi, ukitoka Biharamulo kwenda Ngara pale Mlima wa Simba lazima usindikizwe na Polisi kwa sababu ya majambazi.

Tukasema hapana majambazi hawawezi kutawala katika nchi hii, na ndio maana navipongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema. Alisema bila amani watu hawataweza kwenda kanisani wala msikitini kwa kuwa watakuwa na hofu kwamba majambazi watawavamia ili waibe sadaka.

Mbali ya hilo, alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia amani ya nchi, akitolea mfano walivyosimama kidete kumaliza mauaji ya Kibiti mkoani Pwani.

Alieleza kuwa ulinzi na usalama wa nchi ndio kipaumbele namba moja. Kauli hii ya Rais Magufuli imekuja kwa wakati mwafaka hasa wakati huo ambao wanasiasa wa vyama mbali mbali nchini wako katika maeneo mbali mbali wakiomba ridhaa ya Watanzania wenzao wawachague ili kuwaongoza katika nafasi ya Urais, udiwani na ubunge.

Amani ya nchi ndio msingi wa kila kitu hivyo wanasiasa wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao wanapaswa kufahamu hilo, na kama msingi wa kulinda utaifa, wanapaswa kusisitiza amani na kuwa tayari kuilinda kwa gharama yoyote.

Tumeshuhudia Tanzania kwa miaka mingi tangu ipate huru wake ikiwa nchi yenye kupigiwa mfano kwa kuwa na amani na utulivu na watu wake kuwa huru kujihusisha na masuala mbali mbali ya ustawi wao.

Kwa msingi huo, tunaamini kila Mtanzania analo jukumu kubwa la kulinda amani ya nchi bila kujali nafasi wake, lakini wanasiasa wana dhamana kubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa baadhi yao wamekuwa wakitoa maneno yenye kuhatarisha amani na utulivu nchini na yenye kutaka kuwagawa Watanzania.

Viongozi wenye kuhubiri mgawanyiko miongoni mwa Watanzania hawana nafasi na wananchi wanapaswa kuwakemea na kuwakataa kupitia sanduku la kura wakati wa kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu.

Tunasema hivyo kwa sababu Tanzania inahitaji amani kwa ajili ya ustawi wa taifa na hasa wakati huu ambao nchi inapiga hatua kubwa za kimaendeleo chini ya usimamizi wa Serikali ya Awamu ya Tano, hatua ambazo zimelifanya taifa liwe mfano wa kuigwa na mataifa mengine duniani

HABARI kwamba ajali za barabarani nchini zimepungua kwa asilimia 35 ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi