loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Msipige kura kwa jazba -Magufuli

MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amesema Oktoba 28, mwaka huu wananchi wasipige kura kwa jazba na wawachague wagombea wakweli.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi Kemondo, Bukoba Vijijini mkoani Kagera kwenye mkutano wa kampeni za kuomba kura. Aliomba wananchi wamchague aendelee kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano amalizie muhula wake wa mwisho apumzike.

Aidha, pia aliwaombea kura wagombea wote wa CCM ngazi ya ubunge na udiwani ili afanye kazi nao vizuri, kwa kuwa wakichaguliwa wagombea wa kutoka vyama vingine ni vigumu kuwabana.

“Tusichague kwa jazba, na kuangalia viongozi wapenda maneno, tukikosea, tutajuta maana hakuna maendeleo mtakayoyaona,”alisema Rais Magufuli.

Alirudia kauli yake kuwa akimaliza miaka mitano, hataongeza hata siku moja madarakani na kwamba CCM ina hazina ya viongozi, wanaoweza kuongoza kwenye nafasi hiyo.

“Naombeni mnipe miaka mitano tu, tutafanya makubwa katika muda huo, nikimaliza miaka yangu mitano hiyo, sitaki niongezewe hata siku moja, wapo wengine ndani ya CCM wanaoweza pia kuongoza, nataka nipumzike na mimi niangalie wengine wanavyofanya kazi,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza, “Sio kwamba napenda niwe Rais, urais ni mateso, kazi yoyote ukitaka kuifanya vizuri ni mateso, nasema kwa dhati nikishamaliza miaka hii mitano sitaki kuongezewa hata siku moja.”

Alitoa mfano wa viongozi waliomtangulia akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

“Ndio maana nasema chama kina hazina ya viongozi, na tuna mfumo mzuri, mimi naomba niongezeeni hiyo mitano nitafanya maajabu kwa nchi, halafu ikiisha nitapumzika,” alisema.

Akizungumzia changamoto za Kemondo, alisema kuna ukosefu wa maji wakati Ziwa Victoria lipo jirani. Alihoji kwa nini viongozi wa mkoa na wilaya, wameshindwa kujenga hata tangi kubwa la kuhifadhi maji.

Alisema baada ya meli za abiria kufanya kazi katika Ziwa Victoria, kuanzia sasa wafanyabiashara wanaosafirisha ndizi na mizigo yao kutoka eneo moja kwenda lingine watalipia tozo ya Sh 27,000 tu kwa tani moja, badala ya Sh 100,000 hadi 130,000 iliyokuwa ikitozwa awali.

“Tunataka Kemondo, hapa bandarini pawe salama wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru na tija, tumeamua kuanzia sasa tozo kwa tani moja ya mazao au bidhaa zitozwe shilingi 27, 000 badala ya ile ya awali ya hadi shilingi 130,000,” alisema Rais Magufuli.

Akiwa Muleba, aliwaasa wanachama wa CCM wamalize tofauti baina yao, hasa za makundi ya kisiasa yaliyokuwepo wakati wa mchakato wa uteuzi kugombea nafasi za ubunge.

“Ninafahamu hapa kuna maneno maneno, chama ndio kinachagua nani anafaa kwa wakati gani, sasa masuala ya nani kapitishwa yalishaisha, tuliamua tuwachague hao tuliowapitisha kwa sababu ndio wanaofaa kuongoza kwa muda huu, na pia uongozi ni kupeana nafasi… unaweza kuongoza leo kesho akaongoza mwingine,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa miaka mitano iliyopita, Muleba imenufaika na zaidi ya Sh bilioni 65.32 zilizotolewa kwenye miradi ikiwemo ya afya, elimu, miundombinu na mingine.

Alitoa mfano kuwa kwenye afya Sh bilioni 18.57 zimetumika kujenga vituo vya afya, Sh bilioni 14.8 zimetumika kununua vifaa tiba na dawa na pia kuna ujenzi wa zahanati tano ikiwemo Bugasha na Goziba, ambayo kila moja imegharimu takribani Sh milioni 400 hadi 500.

Kuhusu elimu, alisema zaidi ya Sh bilioni 9.94 zimetumika kuboresha elimu; na Sh bilioni 8.4 zimetumika kukarabati miundombinu ya elimu ikiwemo Shule ya Kaigala na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (VETA).

Aidha, alisema changamoto ya sasa ni vijiji 44 vilivyobaki kupata umeme na kuahidi kwamba iwapo CCM itashinda, miaka ya mwanzo baada ya uchaguzi vijiji hivyo vitaunganishiwa umeme.

Awali akiwa njiani kwenda Kagera, alizungumza na wananchi wa Kasharunga na kusema kero za eneo hilo zikiwemo maji, ardhi na elimu atazishughulikia.

Akizungumzia kero ya kutokamilika kwa ujenzi wa Shule ya Msingi Kyamola, Rais Magufuli alisema hadi sasa madarasa mawili yamejengwa na kuahidi atatoa Sh milioni 10 ziende kusaidia ujenzi huo ili wanafunzi wapate mahali pa kusoma.

“Nitatoa shilingi milioni 10, hizi sio rushwa ya uchaguzi ni kwa ajili ya maendeleo, lakini natumia hivi kwa maana mimi bado ni Rais, changamoto za wananchi lazima zitatuliwe,”alisema Magufuli

TIMU ya  Simba imethibitisha kiungo  wake Mbrazili Gerson Fraga ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi