loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maonesho Siku ya Mara yahitimishwa

MAADHIMISHO ya Tisa ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika uwanja wa Maria Nyerere wilayani Butiama mkoani Mara, yamehitimishwa Septemba15, mwaka huu.

Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka, kwa mzunguko kati ya Tanzania na Kenya ili kuhamasisha utunzaji na Ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa jamii inayolizunguka bonde hilo.

Maadhimisho ya Mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo: "Ikolojia ya Mara Iliyotunzwa - Ustawi Wetu.” Kwa kutambua umuhimu na changamoto za Ikolojia ya Bonde la Mto Mara, Baraza la Kisekta la 10 la Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria, lililofanyika Kigali, Rwanda Mei 4, mwaka 2012, liliazimia na kutangaza Septemba 15 kila mwaka kuwa Siku ya Mara.

Katika msimu huo kuna uhamaji mkubwa wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Serengeti iliyopo Tanzania kwenda Pori la Akiba la Kitaifa la Maasai-Mara nchini Kenya.

Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Tanzania na Kenya, Maadhimisho ya Tisa ya Mto Mara yaliyofanyika mwaka huu, yalipaswa kufanyika nchini Kenya, lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa wa covid-19, pande zote mbili zimekubaliana kufanya maadhimisho ya siku hiyo nchini mwao.

Madhimisho ya mwaka huu, yalienda sambamba na shughuli mbalimbali zikiwamo semina kuhusu masuala ya udongo na kilimo iliyotolewa kwa wakazi wa Mkoa wa Mara waliohudhuria katika uwanja wa Maria Nyerere, Butiama, maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiriamali, maonesho ya mashamba darasa na kazi za sanaa na ubunifu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Mara kwa ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa Tanzania na Kenya zinazolizunguka bonde hilo.

Sambamba na hilo Malima aliwahimiza wananchi kuendelea kutunza ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa kufuata taratibu zilizowekwa na kushauriwa na wataalamu ili kuendesha shughuli zao katika mazingira yanayozunguka bonde hilo.

Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Judith Ngoda katika maadhimisho hayo alipongeza utayari na ushiriki wa wananchi katika kulitunza Bonde la Mto Mara.

Alisema juhudi, nguvu na umoja unaooneshwa na serikali za Tanzania na Kenya unadhihirisha ushirikiano na mshikamano uliopo katika kuhakikisha ustawi wa uchumi kwa jamii inayozunguka Bonde la Mto Mara unakuwa endelevu kupitia mazingira.

Sherehe za Siku ya Mara huongozwa na malengo matatu ya kujenga uelewa kwa wadau muhimu kuhusu umuhimu wa Bonde la Mto Mara na rasilimali zake; kutambua na kuhusisha mchango wa watendaji wa umma na binafsi katika usimamizi wa rasilimali za Mto Mara, na kukuza ushirikiano wa umma na binafsi kama njia ya kuelekea katika usimamizi endelevu wa maji ya Mto Mara na baionuwai.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi