loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Wafugaji nchini acheni kufuga kwa mazoea’

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Elisante Ole Gabriel, amewataka wafugaji waache kufuga kwa mazoea, bali wawe na ng’ombe bora na wenye tija.

Pia amesema serikali imelenga kuhakikisha wafugaji nchini, wanakuwa na ng'ombe bora wanaotoa mazao bora yakiwamo ya nyama na maziwa mengi yanayopatikana kwa njia ya uhimilishaji.

Profesa Gabriel alisema hayo katika Kijiji cha Matebete wilayani Mbarali mkoani Mbeya, wakati akizindua kambi ya uhamilishaji katika kijiji hicho kwa wafugaji wa jamii ya Kimasai.

Aliwataka waache kufuga kwa mazoea, bali wawe na ng'ombe bora na wenye tija huku akiwalenga zaidi akinamama nchini kujikita katika ufugaji wa kisasa.

"Haya ni mafanikio makubwa; niwaombe akinamama wengine Tanzania waige mfano wa akinamama wenzao wa jamii ya Kimasai walioamua kufuga kisasa kwa kuwa na ng'ombe bora,” alisema na kuongeza:

“Hatuwezi kuendelea kwenye ufugaji wa zamani lazima tufuge kisasa na uhamilishaji unaofanyika hata kwa ng'ombe wa kienyeji," alisema.

Akizungumzia faida za uhimilishaji, alisema njia hiyo ya kumpatia ng'ombe mimba kwa njia ya mrija ni muhimu katika kuendeleza ubora wa mifugo ili kutengeneza mbari na kosaafu bora ya ng'ombe.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, uhimilishaji ni muhimu kwa kuwa mfugaji anaweza kuchagua ng'ombe anayemtaka na ubora wake na kudhibiti magonjwa ya mifugo hiyo kwa ng'ombe dume kupanda ng'ombe wengi kwa wakati mmoja.

Ili kutoa hamasa kwa wafugaji wa jamii ya Kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Katibu Mkuu huyo alisema wafugaji watakaohimilisha ng'ombe 1,000 wa mwanzo, wizara itagharamia kama sehemu ya uzinduzi na uimarishaji wa kambi za uhimilishaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo, Stephen Michael alisema wizara imekuwa ikifanya kazi karibu na wananchi hali iliyofikia kuweka kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete na kuwafanyia ng'ombe vipimo kabla ya kupandikizwa mbegu.

Ofisa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Fadhil Chamwazi, alisema kambi za uhimilishaji zinalenga kuhamasisha wafugaji kutumia huduma ya uhamilishaji na kuijengea uwezo jamii ya wafugaji na wataalamu juu ya faida ya uhamilishaji.

Chamwazi alisema kazi hiyo ilianza katika Mwaka wa Fedha 2019/20 na kwa mwaka 2020/2021, imezinduliwa mkoani Tabora na sasa ipo katika Mkoa wa Mbeya kijijini Matebete.

Alielezea vigezo vinavyoangaliwa kwa ng'ombe kabla ya kupandikizwa mbegu ya uzazi kwa njia ya mrija, kuwa ni afya ya ng'ombe, umri na mwonekano.

Baadhi ya wafugaji wa jamii ya Kimasai katika kijiji hicho wamefurahishwa na zoezi hilo na kuiomba serikali kuendelea kuwapatia elimu zaidi na kuwafahamisha namna bora zaidi za ufugaji wa ng'ombe bora wa kisasa ili wapate matokeo chanya katika ufugaji wao.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kondoa kwa tiketi ya Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi