loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Trafiki wajipange upya kukabiliana na ajali

MIAKA kadhaa iliyopita kulikuwa na habari za mara kwa mara kuhusu ajali za barabarani na ilikuwa ni kawaida kusikia mabasi yamegongana na kusababisha vifo vya watu wengi.

Lakini, umakini uliowekwa na kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na wadau, ulizaa matunda. Watanzania walishaanza kusahau matukio hayo ya ajali.

Hata hivyo, hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya ajali hizo katika sehemu mbalimbali za nchi.

Kati ya ajali hizo za karibuni ni ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, iliyohusisha basi na gari dogo na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi kadhaa.

Ifahamike kuwa ajali zimekuwa zikileta athari kwa waliojeruhiwa na jamii nzima, yaani wategemezi wa waliokufa au kujeruhiwa kwenye ajali husika. Kama wazazi au walezi wamekufa kwenye ajali ni wazi kuwa maisha ya watoto au wategemezi yatatetereka kwa kiasi kikubwa.

Nguvu kazi ya taifa nayo inapotea. Suala la msingi ambalo wadau wanakabiliana na ajali za barabarani, wanapaswa kujiuliza kwa sasa ni kwa nini ajali zinaanza kurejea tena; huku mabasi nayo yakiungua.

Nadhani kuna haja ya kikosi cha usalama barabarani, kujipanga upya kukabiliana na ajali hizo. Ni imani yangu kama ambavyo kikosi hicho kilifanikiwa kukabili ajali huko nyuma, kuna haja ya kujipanga na kuongeza tena nguvu zaidi.

Kikosi hicho kitoe elimu ya mara kwa mara kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri na kiwachukulie hatua za kinidhamu madereva watakaobainika kukiuka maelekezo.

Hatua hii itadhibiti ajali hizo. Kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau ili kukabiliana na ajali hizo. Binafsi naungana na baadhi ya hoja za wadau hao kwa kuwa kama zikifanyiwa kazi, hakika ajali zitapungua.

Mfano ni mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ambayo haiendani na hali halisi ya sasa. Sheria hiyo imepitwa na wakati na haiendani na matakwa ya sasa ya usalama barabarani.

Kwa mfano sheria hiyo inamtaka mwendesha pikipiki kuvaa kofia ngumu, huku anayepakiwa (abiria) hatajwi kama anapaswa pia kuvaa kofia hiyo. Ifahamike kuwa mwaka huo ilikuwa ni sawa, kwa kuwa pikipiki hazikuwa zikitumika kibiashara.

Lakini kwa sasa pikipiki ni huduma ya kibiashara na imeajiri watu wengi na inatumiwa kama njia kuu ya usafiri, hivyo kwa sasa kuna haja ya Sheria ya Usalama Barabarani kutaja wazi kuwa abiria naye anapaswa kuvaa kofia ngumu na adhabu kali itolewe kwa atakayekaidi.

Huo ni mfano mmoja tu wa upungufu huo. Lakini, kuna haja ya mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kukabili ajali za aina zote, za magari, pikipiki, baiskeli na nyinginezo.

KAMPENI za uchaguzi kwa ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi