loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanesco yalalamikia uchomaji nguzo zao

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, limelalamikia vitendo vya baadhi ya watu kuchoma nguzo za umeme na kusababisha hitilafu ya upatikanaji wa nishati hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge wilaya humo, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Chamwino, Bartazar Massawe alisema uchomaji nguzo moto umekuwa ni mtihani kwa shirika hilo.

Alisema, vitendo vya uchomaji nguzo za shirika hizo, vinavyofanywa na watu wanaochoma misitu kwa nia ya kulisha mifugo yao, vimekuwa vikisababisha hitilafu ya umeme katika wilaya hiyo.

Massawe alisema shirika hilo pia linapambana na changamoto nyingine katika kusambaza huduma hiyo, ambayo ni barabara. Alisema barabara hupitika kwa shida wakati wa mvua hivyo kufanya shughuli zao kutokuwa na ufanisi mkubwa.

Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, kwa kutoa fedha kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi inayowezesha maeneo yao kupata umeme.

Pia kuanzishwa kwa miradi hiyo, kumekuwa fursa pekee kwa wananchi ya kuboresha na kuinua maisha yao kiuchumi na kijamii pia.

Massawe alisihi wananchi kuwa na shukrani kwa serikali, kwa kuwa sehemu ya wadau wa kutumia nishati hiyo na hivyo ni muhimu kulinda miundombinu na kutoa taarifa Tanesco mara hali yoyote hatarishi inapojitokeza.

Aliwataka wananchi hao kutumia fursa ya uwepo wa umeme wilayani kwao, kwani walisubiri umeme muda mrefu na sasa Serikali ya Awamu ya Tano imesikia kilio chao kwa kuwapa nishati hiyo.

Alisema baada ya kufikiwa na nishati hiyo, wananchi wanafaidika kwani inasaidia watoto na walimu katika shughuli za kielimu kwa kusoma na kutumia katika vifaa vya Tehama.

Pia wamekuwa wakipata maji kwa urahisi kwa kuwa nishati hiyo inasaidia kwa kiwango kikubwa kuyavuta maji kirahisi kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

Massawe alisema huduma za afya zimeboreka, kwani nishati hiyo inasaidia kurahisha mambo mengi ambayo yalikuwa hayafanyiki kwa kukosa huduma ya nishata ya umeme.

Pia nishati hiyo imechangia kuamsha shughuli za kiuchumi kwenye maeneo ya wananchi, kwa kuanzisha viwanda vidogo na shughuli nyingine zinazohitaji nishati hiyo.

Alisema hali ya upatikanaji wa umeme kwa wilaya ya Chamwino, inaridhisha na wanapata Megawati 3.6 kutoka Kituo vya Kupoozea Umeme cha Zuzu.

Wilaya hiyo ina laini nne, ambapo moja ni ya Chamwino Ikulu, ya Mpwapwa inayosambaza umeme Buigiri hadi Dabalo na Ndebwe na laini ya Brick ambayo inatoa huduma Mvumi hadi Mlowa.

Laini ya nne ni ya Kibaya inayotoa umeme Izava, Itiso hadi Zajilwa. Wilaya ya Chamwino ina majimbo mawili ya Chamwino na Mvumi, ambayo yana jumla ya vijiji 108.

Zaidi ya robo tatu ya vijiji hivyo vinapata umeme. Jimbo la Chamwino lina vijiji 48 na vinavyonufaika na umeme ni 26. Vijiji 22 vilivyosalia, kati yake vijiji vitano vitanufaika na miradi inayoendelea chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Vijiji 17 vilivyobaki vipo kwenye mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili. Jimbo la Mvumi lina vijiji 60, kati ya hivyo vijiji 31 vimeshapatiwa umeme.

Vijiji 29 vilivyobaki tayari vijiji 10 vipo kwenye miradi inayoendelea na 19 vilivyobaki vitaingia kwenye mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kondoa kwa tiketi ya Chama ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Chamwino

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi