loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania yapunguza matumizi kemikali 86%

TANZANIA imepunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86 ya kiasi cha matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa tabaka la ozone, azma ikiwa ni kuondoa matumizi ya kemikali hizi kufikia mwaka 2030.

Haya yalisemwa jana jijini Dodoma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan katika kuadhimishia Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene.

Makamu wa Rais alisema katika jitihada za kuhifadhi Tabaka la Ozoni, mwaka 1996 Serikali ya Tanzania iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondoa matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa tabaka hilo ili kuhakikisha hakuna sekta ya uchumi au jamii inaathirika kutokana na matakwa ya Itifaki ya Montreal.

Aidha, programu hiyo ilianzisha utaratibu wa kusimamia na kudhibiti uingizaji wa kemikali na bidhaa zenye kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka nje ya nchi.

Makamu wa Rais aliikumbusha jamii wajibu wa kuendelea kulinda tabaka la Ozoni kwa kuepuka kuingiza nchini kemikali na vifaa vinavyotumika kumong'onyoa tabaka hilo, kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba), bali kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni.

“Natoa rai kwa jamii kununua bidhaa zilizowekwa nembo ya “Ozone friendly” yaani ‘sahibu wa Ozoni’ au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni,” alisisitiza Makamu wa Rais.

Maadhimisho ya mwaka huu yalienda sambamba na utoaji wa zawadi kwa washindi wa insha kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai kwa ngazi za shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu kwa lengo la kukuza na kupima uelewa, kuhamasisha ubunifu kwa wanafunzi na vijana kuhusu mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya bioanuai.

Alitoa wito kwa washirika wa maendeleo, kuunga mkono jitihada za kutunza mazingira katika: kuhifadhi tabaka la ozoni; kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi; kuhifadhi bioanuai na usafi wa mazingira.

Pia kuhusisha vijana wadogo na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za mazingira ili kuwa na kizazi chenye uelewa na kinachothamini hifadhi ya mazingira.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine alisema juhudi za kulinda tabaka la Ozoni zinaendelea kupata mafanikio duniani na kusisitiza kuwa huenda litarejea katika hali yake ya awali takribani miaka 30 mpaka 50 ijayo endapo hapatakuwa na kemikali haribifu zitakazoingia tena angani.

“Juhudi zozote za kupunguza matumizi ya kemikali hizo zitaleta matokeo ya manufaa kwenye kurejesha tabaka la Ozoni katika hali ya kawaida. Juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondoa madhara katika tabaka la Ozoni yanayosababishwa na shughuli zetu tunazofanya,” alisisitiza Balozi Sokoine.

Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya ardhi likiwa na kazi ya kuchuja kiwango kikubwa cha mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia.

Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho ya mwaka huu ni “Miaka 35 ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa manufaa ya afya ya binadamu na mazingira. Lengo la kaulimbiu hii ni kukumbusha umuhimu wa kulinda na kuhifadhi tabaka hilo kwa kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa Ozoni.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kondoa kwa tiketi ya Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi