loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM atambia Ilani ya Uchaguzi

RAIS John Magufuli amewaomba Watanzania kumuamini, kwa kuwa ahadi anazozitoa, zipo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Alisema jana kuwa wananchi wakimchagua Oktoba 28, mwaka huu aendelee kuwa Rais wa Tanzania, atazitekeleza ahadi hizo kama alivyotekeleza za kwenye ilani iliyopita.

Aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa Gymkhana mjini Bukoba mkoani Kagera wakati akiomba kura kwa maelfu ya wananchi waliofika kusikiliza sera za CCM.

Katika mkutano huo, miongoni mwa ahadi za Magufuli ni kuubadili ukanda wa Kagera na Ziwa Victoria uwe wa utalii, kama ilivyo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Alizungumzia pia suala la malipo ya kahawa na kusema amelichukua na serikali lazima italipa madeni yote, kama ilivyofanya kwenye mazao mengine kama korosho na pamba.

“Wale wote wanaodai fedha za kahawa vyama vya ushirika nalichukua hilo, serikali tutalipa yote, nimemuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na Waziri wa Kilimo wanapanga njia bora ya kuzilipa, CCM haiwezi kuwa serikali ya kudhulumu wananchi,”alisema Rais Magufuli.

Alisema ahadi anazotoa si kiinimacho, hivyo wananchi wamuamini na wasiifananishe ilani hiyo na zile za vyama ambavyo baadhi yao wanatoa ahadi kichwani.

“Nataka mniamini, ahadi ninazozitaja ziko ndani ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020-25, sio kama baadhi ya vyama vya siasa ambavyo wanatoa ahadi zao kichwani, hawana ilani, nikiahidi, ninatekeleza, na mfano nzuri ni Ilani ya mwaka 2015, tumetekeleza ahadi nyingi,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia masuala ya umeme mkoani humo, Rais Magufuli alisema wakati akiingia madarakani mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 168, lakini  mwaka 2020 vijiji vyenye umeme vimefikia 535.

Alisema Mkoa wa Kagera una jumla ya vijiji 644 na vilivyopata umeme hadi sasa ni 535; na kwamba vijiji 129 havina. Aliahidi iwapo atachaguliwa muhula wa pili, miaka ya mwanzo vijiji vyote vitapata umeme.

Alisema nia ipo, uwezo upo kwa sababu vyanzo vya umeme vimeongezeka nchini, baada ya miradi mipya ya kuzalisha umeme kuanza kujengwa ukiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji unaotegemewa kuzalisha megawati 2,115.

“Tukiunganisha umeme wa gridi ya taifa suala la kukatika halitakuwepo tena, maporomoko ya Mto Rusumo mkoani Kagera nayo yatazalisha megawati 80, ya Kakono kule Misenyi tutapata megawati 87, bado miradi mingine, tutaunganisha pamoja ikiwemo gesi asili megawati 33,naomba mniamini, tukiwa na umeme wa kutosha viwanda vyetu vitapata umeme wa kutosha, na nchi itakuwa na maendeleo,”alisema.

Alisema katika awamu ya pili ya utawala wake iwapo atachaguliwa, wamepanga kufufua viwanda vya samaki mkoani humo ambavyo awali vilikuwepo lakini vikafa kwa sababu ya baadhi wa mafisadi.

Alisema mwaka 2015 alitoa ahadi mkoani humo ya kufufua na kuimarisha usafiri katika Ziwa Victoria ambao ulikufa zaidi ya miaka 12, tangu kuzama kwa Mv Bukoba na kuleta kero na usumbufu kwa wananchi.

“Sasa Mv Victoria mpya imeanza kufanya kazi, inaitwa Mama Koku, hii meli tumeikarabati upya kwa gharama ya shilingi bilioni 22, tumeifufua na kuijenga upya. Tunaendelea na ukarabati wa nyingine na tunataka Ziwa Victoria kama ule wa waasisi wa taifa hili, Uganda, Kenya ambao waliunganishwa kwa usafiri ndani ya ziwa.

“Nataka mtu akitoka hapa aende Kemondo, wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru, waende Musoma, Kisumu (Kenya), Uganda kisha warudi Bukoba ili mzunguko wa pesa uwe mkubwa, watu watengeneze maisha yao,” alisema Rais Magufuli.

Alisema mbali na meli hiyo mpya kuanza kufanya kazi, pia ipo meli nyingine mpya kubwa inatengenezwa kwa gharama ya Sh bilioni 90. Ikikamilika itakuwa kubwa kuliko Mv Vicktoria na itakuwa na uwezo wa kubeba watu 1,200 na tani 400 za mizigo.

Akizungumza ukarabati wa miundombinu ya usafiri mingine, alisema Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kimekarabatiwa na hiyo imesaidia kupunguza gharama za usafiri.

Aliahidi kuwa Desemba mwaka huu serikali inategemea kuleta ndege mpya moja ; na ndege tano ikiwemo ya mizigo zitanunuliwa katika miaka mitano ijayo.

Aliwataka wananchi wa Kagera kuchangamkia fursa ya bomba la mafuta kutoka Hoima kwenda Tanga, kwani ni mradi wa kipekee mkubwa unaotazamiwa kutoa ajira na kufungua fursa za biashara.

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kondoa kwa tiketi ya Chama ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi