loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Mwinyi aahidi mabadiliko uchumi Pemba

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi amewaomba wananchi Pemba wamuamini kuwa akichaguliwa kuwa Rais ataleta mabadiliko ya kiuchumi, maendeleo na kubadili maisha yao.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati akihutubia wananchi wa mikoa miwili ya Pemba katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni, uliofanyika Uwanja wa Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.

Aliahidi kufanya mabadiliko makubwa ya uchumi wa kisasa wa bluu, uliojikita katika uvuvi wa bahari kuu, kwa kuwawezesha wavuvi kuvuna rasilimali za utajiri mkubwa baharini.

Alisema katika kulifikia eneo la uvuvi wa bahari kuu, serikali itahakikisha wavuvi wanakuwa na zana za kisasa, zitakazowawezesha kuyafikia maeneo hayo na kujipatia kipato kikubwa.

Alisema serikali itafungua milango kwa wawekezaji kuwekeza, ikiwamo kununua meli kubwa zitakazowafikisha maeneo hayo na kuwawezesha pia wavuvi wa kawaida kupata kipato kwa kuvua kwa kuzingatia mazingira ya baharini.

 “Uvuvi unaofanyika kwa sasa ni wa kawaida ambao hauna tija...tunataka wananchi wetu kulifikia eneo la uvuvi wa bahari kuu, hatua ambayo itatuwezesha kuwekeza viwanda vya kusindika samaki,” alisema.

Aidha, alisema akiingia madarakani, kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, anakusudia kuimarisha sekta ya utalii ambayo kwa bahati mbaya kisiwa cha Pemba utalii upo nyuma.

 Kwa mfano, alisema ilani hiyo katika sekta ya utalii imelenga kuingiza zaidi ya watalii 850,000 kwa mwaka. Alisema uwezekano huo upo, kwa kufanya utalii wa kisasa wa fukwe pamoja na majengo ya kale.

“Nikifanikiwa kuingia madarakani nataka kukigeuza kisiwa cha Pemba kuwa kivutio cha watalii...zipo fukwe na majengo mengi ya kale ya makumbusho ya historia ambayo hayajatumika kikamilifu na kutangazwa,” alisema.

Aliyataja mafanikio makubwa ya usambazaji wa umeme yaliyofanyika katika kisiwa cha Pemba, ambacho kwa sasa kimeunganishwa na Gridi ya Taifa kutoka Tanga.

Alieleza kuwa umeme unaopatikana katika kisiwa cha Pemba ni megawati 20 wakati matumizi halisi ya wananchi pamoja na huduma nyingine ni megawati 10 tu.

“Maendeleo makubwa ya nishati ya umeme yamepatikana katika kisiwa cha Pemba ambapo tumekiunganisha kisiwa hiki na gridi ya taifa kutoka Tanga....umeme unaopatikana sasa ni megawati 20 wakati matumizi halisi kwa sasa ni megawati kumi tu,” alisema.

Alisema anakusudia kufanya upanuzi mkubwa wa Kiwanja cha Ndege cha Karume kilichopo Pemba ili kiwe na uwezo wa kupokea abiria wengi na kwenda sambamba na mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii.

“Mikakati yote hiyo ya kuimarisha miundo mbinu ya umeme pamoja na sekta ya uvuvi wa bahari kuu...tunakusudia kuongeza ajira na kufikia 300,000 kutoka serikalini na sekta isiyo rasmi huku akisisitiza wananchi kuimarisha amani na utulivu,” alisema.

Akimtambulisha kwa wananchi wa mikoa miwili ya kisiwa cha Pemba, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema Dk Mwinyi anatosha kuwa Rais wa Zanzibar kwa sababu ameonesha uwezo mkubwa na uzoefu wa kuongoza, baada ya kushika nafasi nyeti za uwaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema wagombea wa vyama vingine, hawana sifa za Dk Mwinyi. Alisisitiza kuwa CCM haikubahatisha kumpa dhamana ya kupeperusha bendera ya urais Zanzibar.

 ''Nataka niwaambie wapinzani kwamba CCM itashinda kwa ushindi wa kishindo...ipo nyimbo ambayo hawaipendi wapinzani inayosema 'Mpewa hapokonyeki na aliyepewa kapewa,” alisema Dk Shein.

 Aliwataka wananchi wa kisiwa cha Pemba, wasikubali kuyumbishwa na kudanganywa na viongozi wenye uchu, tamaa na uroho wa madaraka.

 

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kondoa kwa tiketi ya Chama ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Pemba

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi