loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Barabara za mawe zinaboresha maisha Mwanza

WAKATI Rais John Magufuli anaingia madarakani, Serikali ilikuwa kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2025 (Vision 2025) inayolenga kuifanya Tanzania kumudu uchumi shindani. Wakati huo Serikali ilikuwa inaingia kwenye Mpango wa Pili wa miaka mitano (2016/17- 2020/21).

Katika mkakati huo wa kuinyanyua Tanzania kiuchumi, Serikali ilijipanga kuendelea kuboresha sekta za biashara, viwanda, kilimo, elimu, maji, umeme, ajira pamoja na ujenzi wa barabara.

Mpango huo unaobainisha kwamba miundombinu ya barabara ni moja ya mazingira wezeshi ya kunyanyua uchumi ulilenga kuandaa misingi ya kuifanya Tanzania kuwa nchi inayotegemea uchumi wa viwanda na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania yakiwemo mazao.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoishia mwaka huu (sura ya 39) iliahidi kuhakikisha mfuko wa barabara unaimarishwa na matumizi ya fedha yanadhibitiwa, hii ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia matengenezo ya barabara za mijini na vijijini.

Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) ambao unahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilomita 108,946 nchini umeshafanya kazi kubwa katika kipindi kifupi na hivyo kusaidia ukuaji wa uchumi na hivyo katika kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025 kama ilivyotarajiwa awali.

Uboreshaji wa babarabara umeimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na bidhaa na hivyo kuwa chachu ya maendeleo.

Katika mtandao huo wa barabara wa kilomita 108,946 zilizo chini ya Tarura, kilomita 2,025 ni barabara za lami huku zile za changarawe zikiwa kilomita 24,493 na zilizobaki ni barabara za udongo.

Tarura mkoani Mwanza

Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mwanza ndio unachukuliwa kuwa mkoa wenye uchumi mkubwa na kitovu cha kanda hiyo.

Shughuli kuu za kiuchumi mkoani Mwanza ni uvuvi katika Ziwa Victoria, usafirishaji wa nchi kavu na majini, kilimo, ufugaji, shughuli za viwanda, biashara, madini na ajira katika sekta ya umma.

Kwa upande wa kilimo, maeneo mengi ya mkoa huo yana ardhi nzuri na hali ya hewa inayowezesha shughuli mbalimbali za kilimo. Kama ilivyo kwa mikoa mingi ya kanda ya ziwa, zao kuu la biashara ni pamba lakini mazao mengine yanayotumika kwa ajili ya chakula na biashara ni pamoja na mpunga, mhogo, viazi viku, maharage na kadhalika.

Katika kuboresha barabara za Mwanza ili shughuli za kiuchumi ziendelee vyema, Tarura mkoa wa Mwanza imekua ikisimama imara katika matengenezo endelevu ya barabara kwa gharama nafuu.

Mohamed Muanda aliyekuwa akikaimu uratibu wa Tarura mkoani humo hivi karibuni, anasema kwa asili jiji la Mwanza limezungukwa na milima na watu pia wamejenga kwenye milima na hivyo Tarura ina dhima ya kupeleka barabara huko milimani.

Moja ya mbinu ambayo wakala huo wa barabara unatuimia ni kujenga barabara za mawe, hususani katika maeneo hayo ya milimani.

Muanda ambaye pia ni Meneja wa Tarura Manispaa ya Ilemela anasema hatua hiyo inapunguza gharama ya ujenzi na barabara hizo zinawasaidia sa wananchi kwa usafiri na usafirishaji, hasa katika kipindi cha mvua.

Anasema mradi wa ujenzi wa barabara za kiwango cha mawe katika barabara zenye urefu wa mita 889.65 ni moja ya miradi iliyotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwa gharama ya Sh milioni 511.3.

Mradi huo anasema unatekelezwa kwenye barabara za Isamilo-Nyanshana yenye urefu wa mita 200, Kleruu (mita 293), AIC Nyabulogoya mita 182.2, eneo la Shule ya Mbege na Mwarabu (mita 100) na Mlungushi (Mwanahenge) urefu wa mita 114.45.

Daraja la Fumagila

Mradi mwingine uliofanywa na Tarura ni ujenzi wa daraja la Fumagila lenye urefu wa mita 30 likiwa na midomo mitatu. Daraja hilo Muanda anasema ni muhimu kwa sababu kukamilika kwake kutaunganisha wilaya za Nyamagana, Misungwi, Magu na Kwimba.

Vilevile anasema daraja hilo litakuwa ni kiungo cha mradi wa machinjio ya jiji hilo na Bandari Kavu ya Fela inayotazamiwa kujengwa. Gharama za daraja hilo kwa uhakiki uliofanywa karibuni ni Sh milioni 552.2 na mkandarasi ameshalipwa Sh milioni 493.7.

Akizungumzia Manispaa yake ya Ilemela, Muanda anasema kwa mujibu wa takwimu za sasa mtandao wa barabara unaosimamiwa na Tarura katika  Manispaa hiyo una urefu wa km 875.85  ambapo barabara za lami ni km 35.26, zege ni km 1.52, mawe km 2.07, changarawe km 60.18 na udongo ni  km 776.83.

Anasema mbali ya sehemu kubwa ya gharama kutolewa na Mfuko wa Barabara, kuna wafadhili wengine hususani Benki ya Dunia.

Wananchi wa Manispaa ya Ilemela, hususani wanaokaa milimani wanapongeza hatua ya serikali ya awamu ya tano kuwapelekea barabara kwani huko nyuma walikuwa na shida kufika kwenye makazi yao hasa wanapokuwa na mizigo inayohitaji usafiri wa gari.

Gideon Nyanda, mkazi wa Ilemela anasema barabara ya Igogwe – Kabusungu – Igumamoyo – Sangabuye Secondary na ya Kahama – Igombe ikikamilika itawasaidia sana wananchi katika kupata huduma za kijamii katika hospitali mpya ya wilaya ya Ilemela na pia wanafunzi watapita kwa urahisi kwenda shuleni.

Muanda anasema kwa mwaka wa fedha 2019/20 Tarura katika Manispaa ya Ilemela imepangiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara.

Barabara nyingi Ukwerewe zafunguliwa

Mwanaidi Zakimwela, mkazi wa Nansio, Ukerewe, anaipongeza Tarura katika kuhakikisha barabara nyingi zinapitika wakati wote. Hata hivyo, anasema bado wana changamoto ya barabara ya Hamkoko – Bukimwi ambayo inaelekea mpaka kivukoni kwenye pantoni la MV Ilemela.

“Tunaiomba Serikali itusaidie kuitengeneza hiyo barabara,” anasema.

Kwa upande wake meneja wa Tarura, Halmashauri ya Ukerewe, Reuben Myungi anasema halmashauri hiyo ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 660 kwa sasa na kwamba kabla ya Tarura, Ukerewe ilikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 376 pekee.

“Kwa Takwimu hizo zinakuonyesha kwa sasa Tarura tumewafikia wananchi wengi zaidi wa Ukerewe kwenye sekta ya miundombinu. Yaani kuna maeneo yalikuw ahayana barabara lakini sasa tumezifungua,” anasema.

Anasema barabara ya Hamkoko – Bukimwi yenye urefu wa kilomita 5.6 inatakiwa kujengewa kalavati la midomo miwili na kwamba hatua hiyo tayari imetengewa shilingi milioni 158. Anasema barabara hiyo ni muhimu kwani inakwenda mpaka kwenye kivuko cha pantoni na hivyo kuwezesha kusafirisha wananchi na shehena zao.

Barabara zashamiri Misingwi, Kwimba

Alzabron Kayungi, Meneja wa Tarura Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi anasema wao wana tunamtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 927.57 baada ya kuhakikiwa. Anasema wamekuwa na miradi minne ya matengenezo ya kawaida ya barabara na mradi mmoja wa uwekaji wa lami katika barabara zilizopo katikati ya mji, ambao ni ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa kampeni mwaka 2015.

Naye Meneja wa Tarura wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Dickson Rukanazy anasema kabla ya kuanzishwa Tarura, Halmashauri halmashauri hiyo ilikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 587 lakini Tarura imeuongeza hadi kuwa kilometa 864.18.

Kwa mwaka wa Fedha wa 2019/2020 Kwimba ilitengewa Sh milioni 781.6 kwa ajili ya matengenezo ya barabara muda maalumu.

Rukanazy anasema Pamoja na barabara zingine pia wameweza kutengeneza barabara yenye urefu wa kilomita moja inayozunguka mji wa Ngudu, ambayo ni ahadi ya Rais Magufuli.

 

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi