loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Trilioni 3.4/-  ilivyoboresha barabara za mijini, vijijini

KATIKA kuboresha usafiri na usafirishaji pamoja na utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imetekeleza kwa kiwango kikubwa miradi ya ujenzi wa barabara katika mamlaka ya serikali za mitaa.

Akizungumza na Habarileo wakati wa maadhimisho ya TAMISEMI Day, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo anasema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imetumia Sh trilioni 3.463 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya barabara katika mamlaka za serikali za mitaa.

Anasema katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 hadi Julai, 2020, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mikoa (Tamisemi) ilikuwa imetumia Sh trilioni 1.186 kutoka Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo, ukarabati na ujenzi wa barabara na madaraja kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wenye mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 108,946.19.

“Kiasi cha shilingi trilioni 1.080 pia kimetumia kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 133,192.77, madaraja 250, makalvati 3,361 na mifereji yenye urefu wa kilomita 67.766, sawa na wastani wa matengenezo ya kilomita 26,638.55, madaraja 50, makalavati 672 na mifereji urefu wa kilomita 14 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya kazi za matengenezo imetekelezwa na Tarura iliyoanzishwa Julai, 2017.”

Kwa upande wa ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, Jafo anasema katika kipindi hicho Sh bilioni 106.451 zimetumika katika ujenzi na ukarabati wa barabara za lami urefu kilomita, 136.95, barabara za changarawe urefu wa kilomita 1,092.63,  barabara za mawe kilomita 3.5 na madaraja 75.

“ Hatua hii imesaidia kuongezeka kwa mtandano wa barara za lami kwa mamlaka ya serikali za mitaa kwa urefu wa kilomita 699.5 ambayo ni asilimia 52 kutoka kilomita 1,325.49 mwaka 2015 hadi kufikia kilimita 2,024.99 mwaka 2020.

Anasema kwa upande wa barabara za changarawe kulikuwa na barabara zenye urefu wa kilomita 22,089 lakini baada ya maboresho zimefikia urefu wa kilomita 24,193, ikiwa na ongezeko kwa asilimia 11 huku Serikali ikiimarisha barabara za udongo na kufikia urefu wa kilomita 82,428, wakati madaraja makubwa yaliyojengwa ni 99.

“ Mtandao wa barabara zenye hali nzuri na wastani  umeongezeka kutoka kilomita 61,798.45 hadi kufikia kilomita 63,164.74 sawa na ongezeko la barabara zenye hali nzuri na wastani za urefu wa kilomita 1,366.29, hii inafanya barabara zenye hali nzuri kutoka asilimilia 56 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 58 mwaka huu.”

“Hii inaonesha utashi wa Rais wa kuhakikisha wananchi wanatengenezewa mtandao wa barabara na hii imesahidia hata wakulima kuweza kusafarisha mazao yao, siku za nyuma kwani watu walikuwa wanateseka sana, tunamshukuru Rais kwa kuwezesha hili.”

Anapozungumza miradi ya ushirikiano na wadau wa maendeleo, Jafo anasema katika kipindi hicho, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID) imetekeleza mradi wa uondoaji wa vikwazo vya upitikaji katika barabara maeneo ya vijijini kupitia Mradi wa Kuboresha Barabara katika Maeneo ya Vijijini (IRAT).

Anasema mradi yake ambayo ilikamilika mwaka wa Fedha 2018/19, zaidi ya Sh bilioni 90.449 zilizotolewa na kutumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa barabara, makalavati na madaraja kwenye maeneo yaliyokuwa na vikwazo vya upitikaji hasa kipindi cha mvua kwa awamu sita.

Mradi umetekelezwa katika Halmashauri 40 na jumla ya miradi iliyotekelezwa ni 55.

“ Mradi wa IRAT umeweza kufungua mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 2,000 ambao ulikuwa haupitiki kutokana na vikwazo vya mito, mabonde na maeneo yenye unyevunyevu kwa kujenga madaraja na makalavati, kuinua matuta ya barabara na kuweka changarawe na kujenga barabara za zege kwenye sehemu zenye miinuko mikali.”

 “ Mradi huu umenufaisha watu wapatao milioni tatu waishio maeneo ya vijijini ambao walikuwa na changamoto ya usafiri kutokana na vikwazo vya upitikaji wa barabara na pia Mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa barabara (Ddiomas) umeimarishwa na wahandisi na pamoja na mafundi sanifu wapatao 850 kutoka mikoa yote 26 nchi wamepatiwa mafunzo ya kutumia  mfumo huu.

Jafo anasema TamisemiI kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (Usaid) imekamilisha mradi wa kuimarisha barabara kwenye halmashauri zenye mazao ya chakula na zinazotumia kilimo cha umwagiliaji katika halmashauri za Kilombero, Mvomer, Kongwa na Kiteto ambapo kilometa 412.9 za barabara kwa kiwango cha changarawe zimejengwa kwa gharama ya Sh bilioni 30.2.

Anasema Tamisemi imetekeleza miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia Mfuko wa Serikali ambapo katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 hadi Julai, 2020, kiasi cha Sh bilioni 22.8 zimetolewa na kutumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 18.4 kwa kiwango cha lami, barabara zenye urefu wa kilomita 264.96 kwa kiwango cha changarawe na daraja  moja.

Anasema pia Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU - EDF) imetekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 53.8 kwa gharama ya Sh bilioni 24.8 katika Halmashauri za Mufindi DC, Songea DC na Mbinga DC.

Anasema pia Ofisi ya Rais – Tamisemi  kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Umoja wa Ulaya kupitia Programu ya Agri-connect, imeanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 87.60 kwa gharama ya Sh bilioni 36.7

“ Barabara hizi zinajengwa katika Halmashauri za Wilaya ya Kilolo DC, Mufindi DC, Mbeya DC na Rungwe DC na hadi sasa TARURA imeshapatiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 19.9 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo na kazi zimeanza.”

Akizungumzia ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali, Jafo anasema mtandano wa barabara wenye urefu wa kilomita 51.2 unajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 89.13 ukiwa na barabara zenye urefu wa kilometa 11.2 zenye njia nne na barabara zenye urefu wa kilometa 28.8 zitakuwa na njia mbili, mradi unaotekelezwa na mhandisi mshauri Afrisa Consulting kwa gharama ya Sh milioni 998.55.

“Miundombinu mingine itakayojengwa ni pamoja na; aakalavati makubwa 20, makalavati madogo 52, njia za watembea kwa miguu zenye upana wa mita 1.5 kila upande wa barabara, njia za waendesha baiskeli zenye upana wa mita 2.71 kila upande wa barabara, vituo vya kupakia na kushusha abiria 50, taa za barabarani 739, maeneo mawili yenye taa za kuongoza magari, mifereji ya maji ya mvua yenye kilometa 98 iliyojengwa kwa zege na makutano ya barabara ya mzunguko mbili.

Naye Katibu Mkuu wa Tamisemi, Joseph Nyamhanga anasema kwenye eneo la uendelezaji wa miundombinu mpango mkakati umejielekeza katika kutekeleza vipaumbele kadhaa ikiwamo ya kuhakikisha ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 23,531, madaraja 80, makalavati 2,052 na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 79.9 ambapo kiasi cha Sh bilioni 275.03 zimepangwa kutumika kupitia Mfuko wa Barabara.

Anasema Tamisemi pia inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ambapo kiasi cha Sh bilioni  186.8 kitatumia kujenga kilomita 70 za barabara kwa kiwango cha lami.

“Tutaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuboresha barabara katika maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo ambapo kiasi cha Sh bilioni 35.5 zimeidhinishiwa.

“Pia kufanya mapitio ya mradi mpya wa barabara wa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii nchini ambao umeidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 28.”

Mradi huu utatekelezwa katika mikoa 13 ya Iringa, Njombe, Mbeya, Geita,  Morogoro, Rukwa, Katavi, Songwe, Tanga, Pwani, Dodoma, Mtwara, Ruvuma na Lindi.

Nyamhanga anasema Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaanza maandalizi ya mradi mpya wa Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness Project (TACTIC) ambao utahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara katika halmashauri 45 za wilaya, miji, manispaa na majiji.

 

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi