loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia aahidi masoko mazao ya wakulima

MGOMBEA mwenza wa urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan amesema, serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kujenga masoko katika mikoa inayozalisha mazao kwa wingi ili wakulima wapate sehemu za kuuza mazao yao.

Mama Samia amesema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa Kigonsera , kata ya Kigonsera , Mbinga mkoani Ruvuma.

Mama Samia alikuwa hapo kuomba kura kwa ajili ya mgombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho John Magufuli

Alisema, serikali kwa kuthamini mchango wa wakulima itahakikisha inaweka mazingira bora kuwawezesha wakulima waendelee kuongeza uzalishaji.

Alitoa wito kwa wakulima mkoani Ruvuma kutumia vituo vilivyowekwa na Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kuuza mahindi kwa bei ya shilingi 530 na kuepuka kuuza mazao kwa walanguzi.

Kwa mujibu wake,Serikali licha ya kutekeleza kwa vitendo miradi iliyorahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, itaendelea kutekeleza mingine kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Aliomba wananchi kwenye kata ya Kigonsera wasifanye makosa kuchagua wagombea wa vyama vya upinzani kwa kuwa wanaweza kurudisha nyuma juhudi na mikakati iliyoanzishwa.

Alisema serikali itaendelea kuongeza kiwango cha fedha kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) ili uweze kuboresha na kujenga miundombinu ya barabara katika maeneo mengi ya wilaya ya Mbinga.

Mama Samia alisema katika awamu ya pili  serikali ya Awamu ya Tano imepanga kuhakikisha inatekeleza na kukamilisha miradi yote ambayo imekuwa changamoto kwa wananchi ikiwemo barabara ya Kigonsera hadi Matiri ambayo wakazi wa maeneo hayo ni wakulima wakubwa.

Amewaomba wananchi wa Kigonsera na wilaya ya Mbinga kuhakikisha wanamchagua Magufuli, na wagombea ubunge na udiwani kutoka CCM.

Awali mgombea ubunge jimbo la Mbinga vijijini Benaya Kapinga ameishukuru Serikali kwa kutekeleza kwa vitendo miradi itakayoharakisha maendeleo kwa wananchi.

Ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga soko la mazao katika kijiji cha Kigonsera kwa kuwa wakazi wake ni wakulima na wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara.

Alisema, iwapo Serikali itajenga soko katika eneo hilo wakulima watafaidika na shughuli zao za kilimo kwa sababu watakuwa na uhakika wa soko tofauti na sasa.

Waziri Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Muhidin Amri, Mbinga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi