loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wenye kisukari wahimiza dawa za kitaalamu

JAMII imehadharishwa dhidi ya tabia ya kuwapa watoto wenye ugonjwa wa kisukari dawa za mitishamba zisizo na vipimo wala viwango.

Rai hiyo ilitolewa na mmoja wa watoto wenye ugonjwa wa kisukari, Neema Paul kutoka kliniki ya kisukari ya Hospitali ya Rufaa Dodoma ambaye ni miongoni mwa watoto 28 kutoka kiliniki saba walioshiriki kambi maalumu ya siku tatu ya watoto wenye kisukari.

Kambi hiyo inayoratibiwa na Chama cha Kisukari Tanzania, imelenga kutoa elimu kuhusu namna ya kuenenda na ugonjwa wa kisukari kwa watoto na wazazi wenye watoto wenye ugonjwa huo.

Aidha, iliwalenga watoa huduma za afya wanaowahudumia wagonjwa hao ili kuwajengea uwezo zaidi mintarafu namna ya kuwahudumia wagonjwa.

Neema alisema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa watoto wao dawa za mitishamba wakiamini zinatibu ugonjwa wa kisukari huku dawa hizo zikiwa hazina vipimo hivyo, badala ya kuwahimiza kutumia dawa za hospitali.

"Kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa watoto wao dawa za mitishamba, hili si jambo jema, maana badala ya kupambana na tatizo moja, mtoto ataanza kuhangaika na magonjwa mengine kama figo na msongo wa mawazo," alisema.

Alitoa rai kwa jamii kutowanyanyapaa watoto wenye kisukari na badala yake, wawasaidie ili watimize ndoto zao.

Naye Moses Paul kutoka Kliniki ya Bugando aliwashukuru waandaaji wa mafunzo hayo akisemaamejifunza mambo mengi ambayo awali walishindwa kuyazingatia.

"Mfano mzuri ni kwenye mlo, nilikuwa nakula chakula ambacho mzazi kaniandalia, mfano unawekewa uji na viazi bila kujua kuwa hiyo ni aina mmoja tu ya chakula, lakini kwa sasa nimejua natakiwa kula makundi yote matano ya vyakula,” alisema.

Moses alimwomba Rais John Magufuli kusaidia upatikanaji kwa wingi wa dawa za kisukari katika maeneo mengi.

"Popote pale Rais Magufuli akinisikia, tunaomba kuongezewa kwa dawa za kisukari ili hata wale wanaotoka kwenye familia masikini, wapate huduma hii hususani watoto…,”alisema.

Akaongeza: "…Nikimnukuu Rais Magufuli wakati wa janga la ugonjwa wa corona, alisema tukubali na tujue kuishi na ugonjwa wa corona, pia kwa sisi tulio na tatizo la kisukari, tunatakiwa kujua namna ya kuishi nao, na hili litawezekana ikiwa upatikanaji wa dawa utakuwa mzuri na zitapatikana maeneo mengi, hivyo namuomba Rais kutusaidia katika hili."

Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), Happy Nchimbi, alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa watoto 28, wazazi na watoa huduma kutoka kliniki saba za Bugando na Sekoutoure (Mwanza), Nyakaanga na Rubya(Kagera), Singida, Mbeya na Dodoma.

"Katika kambi hii kama ilivyokuwa ile ya Bagamoyo, tunawafundisha watoto na wazazi namna ya kuenenda na ugonjwa, kujipima, kuudhibiti."

Kambi ya Bagamoyo ilishirikisha washiriki kutoka mikoa ya Dar es Salaam yenye kliniki nne, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

"Jamii na watoto wanaoumwa huu ugonjwa wanapaswa kujua kuwa tatizo hili halimfanya mtoto kuwa wa tofauti, hivyo wapaswa kusaidia kazi za nyumbani na kushiriki michezo kama wengine,” alisema.

Daktari wa watoto kutoka Wizara ya Afya katika Idara ya Tiba, Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza, Dk Julieth Kabengula, alishukuru Chama cha Kisukari Tanzania kwa kusaidia ustawi wa watoto wenye kisukari.

Alisema tatizo hilo lipo na linakuwa kwa kasi kwani katika kambi 38 ambazo Chama cha Kisukari Tanzania wanasaidia, wamesajiliwa watoto takriban 4,000 wenye tatizo hilo.

"Jamii inapaswa ijue kuwa ugonjwa wa kisukari kwa watoto upo, hivyo waonapo dalili za ugonjwa huo kwa mtoto wafike hospitali mapema, kwani magonjwa yasiyoambukizi yamekuwa yakichangia asilimia 33 ya vifo," alisema.

 

Waziri Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi