loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mpango wa Maendeleo Sekta ya Fedha Miaka 10 wazinduliwa

SERIKALI imezindua Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha wa Miaka 10 (2020/21-2029/2030).

Mpango huo una lengo la kuongeza wigo na fursa za upatikanaji huduma za kifedha kwa wananchi, zikiwemo za bima, mikopo, akiba na uwekezaji.

Aidha, unalenga kuongeza mchango wa huduma za kifedha na bima kwenye Pato la Taifa (GDP), ambao kwa miaka mitano iliyopita unaendelea kuwa wa wastani wa asilimia 3.5, kiasi ambacho bado ni kidogo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga alizindua mpango huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Hazina, Doto James.

James alisema kwa sasa ni asilimia 8.6 tu ya wananchi waishio vijijini, wanapata huduma za kibenki, ikilinganishwa na asilimia 32.1 wanaoishi mijini.

Alisema mpango huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa uchumi na katika sekta ya viwanda.

Alitoa rai kwa sekta hiyo kuendelea kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma za fedha, ili kuboresha huduma kwa wateja, kuongeza vipato, kulipa kodi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Aliwataka wasimamizi na waratibu wa sekta ndogo za benki, bima, masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya hifadhi ya jamii na sekta ya huduma ndogo ya fedha, kuainisha mipango yao ili iendane na mpango huo.

Alisema azma ya serikali kuandaa mpango huo ni kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya fedha ili pia kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na kulinda watumiaji wa huduma za fedha.

Pia kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha, kudhibiti upatikanaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshaji ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika sekta ya fedha.

James alisema kabla ya mpango huo, serikali imefanya maboresho mengi katika sekta hiyo yakiwemo ya kutunga Sheria ya Taasisi za Kifedha na Kibenki ya Mwaka 2006, Sheria ya Bima ya Mwaka 2009, Sheria ya Masoko ya Bidhaa ya Mwaka 2015 na Kanuni zake, zilizowezeshwa uanzishwaji wa soko la bidhaa.

Pia imeandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Kwanza na wa Pili wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2014/15-2016/17 na 2018/19-2020/21 na Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2007 na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 na Kanuni zake ya Mwaka 2019.

Pia ilifanya uboreshaji wa sekta hiyo ili kuimarisha usimamizi wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha, mfumo wa malipo wa papo kwa hapo, Kanuni za Kuwalinda Watumiaji wa Huduma za Fedha za Mwaka 2009.

Pia ilianzisha kanzidata ya huduma za fedha, ambayo itatumika kusajili na kuonesha vituo katika maeneo mbalimbali yaliyofikiwa na huduma za fedha nchini.

Maboresho hayo yameleta matokeo chanya katika sekta hiyo ambapo hadi Desemba 2019, kumekuwa na ongezeko la benki na taasisi za fedha kutoka 10 hadi 60, kampuni za bima kutoka mbili hadi 32 na kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kufikia 28.

“Pia imeanzishwa mifuko ya uwekezaji wa pamoja na kufikia tisa, taasisi za huduma ndogo za fedha kufikia 450 na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) 4,770 Tanzania Bara na 231 Tanzania Visiwani,” alisema Katibu Mkuu Hazina.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha katika wizara hiyo, Dk Charles Mwamwaja alisema maendeleo ya sekta ya fedha ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

Maandalizi ya mpango huo yalifanywa na timu ya wataalamu waliotumia mapitio ya nyaraka, zikiwemo za taarifa ya maboresho ya sekta ya fedha, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini ZSGRP III na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21).

Waziri Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi