loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Riadha taifa 2020 yafana, lakini…

MASHINDANO yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu kubwa ya taifa ya riadha yamefanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kushirikisha mikoa 28, wakiwa ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo.

Zaidi ya wanariadha 250 kutoka mikoa hiyo walishiriki na hivyo kuyafanya kuwa mashindano ya taifa yaliyowahi kushirikisha wanariadha wengi zaidi nchini.

Na hilo la kushirikisha wanariadha wengi zaidi limefanikiwa baada ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kuweka mkono wake kwa kutoa kiasi cha Sh milioni 45 ili kufanikisha.

TOC kupitia Olympic Solidarity (OS) na Kamati za Taifa za Olimpiki Afrika (ANOCA), ndizo zilizowezesha kufanyika kwa mashindano hayo, ambayo kwa miaka mingi haijafanyika.

MIAKA MITANO

Mashindano hayo ya taifa ambayo yanatakiwa kufanyika kila mwaka, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) lilishindwa kuyaendesha kwa sababu mbalimbali na badala yake waliiendesha yale ya wazi, ambayo huwa hayana utaratibu mzuri.

Makamu wa Kwanza wa Rais (Utawala) wa RT, William Kallaghe anakiri wakati wa ufungaji wa mashindano hayo ya taifa kuwa, hayajafanyika kwa miaka mitano na aliipongeza TOC kwa kuwezesha kufanyika.

Pamoja na kupewa fedha na kampuni na taasisi mbalimbali, lakini RT walishindwa kuendesha mashindano ya taifa na badala yake walifanya yale ya wazi tu, ambayo hayakuwa na msisimko wowote.

Wachezaji wengi wamefika katika mashindano hayo kutokana na TOC kubeba mzigo wa kuwahudumia kwa chakula na malazi, ambapo timu zote zilifikia katika hosteli za Chuo Kikuu cha Elimu (Duce), jirani kabisa na ulipo Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

MSISIMKO ULIOPO

Pamoja na kuwepo kwa wanariadha wengi zaidi, lakini bado wengi hawakuwa na viwango, kwani inadhihirisha kuwa mikoa yao haikuziandaa vizuri timu zao kushindana katika mashindano hayo makubwa.

Vyama vya riadha vya mikoa vilishindwa kabisa kuendesha mashindano hayo, ambayo yangewawezesha kupata timu zao za mikoa, ambayo ingeshiriki mashindano hayo ya taifa, lakini hawakufanya hivyo na wengi waliokotana tu.

Kwa miaka mingi, viongozi wa RT wameshindwa kuhamasisha mikoa kuandaa mashindano yao, na hata kuendesha chaguzi ili kupata viongozi halali, ambao watawakilisha mikoa katika mkutano mkuu wa mwaka au ule wa uchaguzi.

Pamoja na matatizo ya hapa na pale, ambayo ni ya kibinadamu, lakini mashindano ya mwaka huu yalifana baada ya kudhaminiwa na TOC na usimamizi mzuri uliokuwepo kutoka RT pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

FUNZO KWA WENGINE

Vyama na Mashirikisho ya Michezo nchini vina mengi ya kujifunza kupitia katika mashindano hayo, ambayo yaliandaliwa vizuri ukiondoa baadhi ya mikoa kutoleta wachezaji wenye ushindani.

TOC imesema kuwa iko tayari kusaidia vyama au mashirikisho mengine ya michezo kufanikisha mashindano yao au kuendeleza michezo husika kwa kuendesha mashindano mbalimbali.

Hata hivyo, uongozi wa RT ulionesha udhaifu pale uliposhindwa kutoa kiasi cha Sh milioni 15, ambacho waliahidi kukitoa wakati wa mikutano ya maandalizi ya mashindano hayo, na kuiacha TOC pekee kutoa fedha za kuendeshea mashindano hayo.

Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla aliahidi kuwa wao watatoa kiasi hicho cha fedha ili kuongezea nguvu baada ya TOC kutoa zaidi ya Sh milioni 45. Pamoja na ahadi hiyo, RT imeshindwa kutimiza ahadi hiyo na badala yake waliacha mzigo kwa TOC pekee, ambayo pia ilisaidia baadhi ya mambo ya kiutawala ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ubora mkubwa.

MIKOA YENYE MEDALI

Mikoa yenye medali ni hiyo 11 iliyoorodheshwa katika `table’ hapo juu na mingine 17 pamoja na kushiriki, imetoka bila ya kuambulia medali yoyote kutokana na maandalizi duni.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gongwe aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge anawapongeza waliopata medali huku akiwataka waliokosa kurudi kwao kujipanga upya.

Anasema mikoa isisubiri wakati wa mashindano tu ndio wajiandae, ambapo anawataka kuwa fiti wakati wote ili kulinda viwango vyao na kuweza kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali watakayoshiriki.

Makamu wa Rais TOC, Henry Tandau anasema kuwa wameamua kuisaidia RT kufanikisha mashindano hayo kutokana na mchezo huo kuongoza kufanya vizuri kimataifa miaka ya nyuma,hivyo wanataka makali hayo yarudi tena.

Hakuna rekodi iliyovunjwa katika mashindano hayo, hivyo timu za mikoa zitatakiwa kuwa makini zaidi na maandalizi hayo kama kweli wako makini na wanataka rekodi hizo zivunjwe.

Mashindano hayo hayakushirikisha michezo ya kuruka juu pamoja na ile ya kuruka viunzi na haikuelezwa ni kwa sababu gani michezo hiyo haikuwepo wakati ni sehemu ya mchezo wa riadha.

Pamoja na kuwepo baadhi ya kasoro hapa na pale, lakini mashindano hayo yaliandaliwa vizuri na wachezaji na baadhi ya makocha waliyasifia kuwa yalienda vizuri, huku wakiitaka RT kuyaendesha mashindano hayo kila mwaka.

INASIMULIWA kuwa miaka takribani 1000 iliyopita, eneo hili Ugogo ambalo ...

foto
Mwandishi: Cosmas Mlekani

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi