loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Krmpotic apewe muda Yanga

ZLATKO Krmpotic hadi sasa hajamaliza hata mwezi, tangu amejiunga na kikosi cha mabingwa wa kihistoria, Yanga, lakini anaonekana kukumbana na upepo mbaya.

Kwa michezo aliyoiongoza timu hiyo tangu ajiunge inaonesha kikosi cha Yanga kwa siku zijazo kitakuwa na ushindani na kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara lakini mashabiki wenye kiu ya kutamani ushindi kwa sasa wanatakiwa kuwa na subira.

Kocha huyo raia wa Serbia, ametua Yanga akiwa na mipango mikubwa ya kukata kiu ya ukame wa mataji ya ligi baada ya kuyakosa ndani ya misimu mitatu mfululizo lakini amekuta mageuzi makubwa yameshafanyika kwa kusajili wachezaji wengi wapya.

Yanga imesajili wachezaji 16, sawa na kikosi kizima kinachotakiwa kutumika kwenye michezo ya ligi hiyo, na Krmpotic hakutoa maoni ya usajili wa nyota wapya na sasa ana kibarua cha muda mfupi kuhakikisha anatengeneza muunganiko utakaokifanya kikosi hicho kushindana na kupata pointi tatu.

Bahati mbaya inayomkuta hajapata muda wa kukaa na kikosi kuwaandaa wachezaji kabla ya kuanza ligi, ambapo kitaalamu kocha anatakiwa kutumia wiki tano mpaka sita kutengeneza maelewano na kupata kikosi cha kwanza.

Krmpotic kabla hajalifanya hilo la kuunganisha kikosi kwa sasa ,anasumbuliwa na tatizo la presha ya mashabiki wenye kiu ya ushindi licha ya kutoa sababu za kiufundi bado anashindwa kueleweka kwenye vichwa vya mashabiki wa Yanga.

Tangu amejiunga na Yanga ,amecheza mechi mbili za ligi dhidi ya Tanzania Prisons waliopata pointi moja baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 ,mchezo wa pili waliibuka na pointi tatu dhidi ya Mbeya City kwa kushinda bao 1-0 mechi zote zikifanyika Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons, kikosi cha Yanga kilionekana kukosa muunganiko licha ya kwamba mchezaji mmoja alijitahidi kuonesha kiwango ambacho mwisho wa siku kilionekana kutokuleta ushindi wa mabao mengi waliokuwa wanatarajia mashabiki wengi wa Yanga.

Baada ya mchezo huo mashabiki walionekana kulaumu benchi la ufundi ,kwa kushindwa kuwatumia wachezaji wa kigeni na kumponda kocha kwanini aliwaanzisha wachezaji wazawa ambao wanaamini waliwakosesha ushindi kwenye mechi hiyo.

Mchezo dhidi ya Mbeya City licha ya kwamba Yanga ilichomoza na ushindi mwembamba wa bao 1-0 ,uliopatikana dakika za mwisho bado kikosi kilionekana kukosa mipango ya kutengeneza mazingira ya kupata ushindi mkubwa kwenye mchezo huo ambao mashabiki walikuwa na matarajio ya kuona timu yao kuibuka na ushindi wa mabao mengi.

Pamoja na kwamba kwenye mechi hiyo wachezaji hao wa kimataifa walianzishwa tofauti na mechi ya awali mambo yaliendelea kuwa magumu kwani wapinzani wao walionekana kuwa bora kwa kucheza mpira wa malengo ingawa walikosa ufanisi sehemu ya kumalizia.

Mechi ilikuwa ngumu ni wazi kikosi cha Yanga kimeanza kuonesha mwanga wa kuanza kutengeneza muunganiko wa kufika kule mashabiki na viongozi wanatamani kuona kikosi chao kinaleta ushindani na kupata ushindi.

Leo Yanga wanaanza kucheza ugenini kikosi chao kinavaana na Kagera Sugar na wakitoka hapo wanaenda kucheza na Mtibwa Sugar mechi zote ngumu lakini bado kikosi cha Yanga naona kinanafasi kubwa ya kuibuka na ushindi .

Sababu inayonifanya kueleza hilo kikosi cha Yanga kinawachezaji wengi wenye uwezo binafsi na inaweza kuwa chachu ya kupata ushindi kwenye mechi hizo za ugenini na kuendelea kusogea kwenye nafasi za juu kwenye msimamo.

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi