loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Biashara masoko ya madini yapaisha mkoa wa Geita

BIASHARA ya masoko ya madini inazidi kupaa na kuwezesha wajasiriamali na wachimbaji mkoani Geita, kunufaika na dhahabu kwa kuuza katika soko halali kwa bei ya dunia.

Aidha, mapinduzi makubwa katika sekta ya madini mkoani Geita, yaliyotokana na ongezeko la uzalishaji wa dhahabu, yanaendelea kubadilisha maisha ya wananchi, baada ya sehemu ya mapato kuelekezwa kwenye uboreshaji wa huduma za jamii na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel aliliambia gazeti hili jana kwamba sambamba na wajasiriamali kunufaika, kumekuwa na ongezeko la wamiliki wa leseni wakiwamo wanunuzi wakubwa wa madini na wanunuzi wadogo.

Alisema Geita ni kitovu cha biashara ya dhahabu na kwamba katika miezi mitatu iliyopita kuanzia Juni mwaka huu, mapato yatokanayo na madini yamekuwa yakiongezeka mwezi hadi mwezi.

Alisema uzalishaji umeongezeka kufikia kilogramu 5,500 kwa mwaka ikilinganishwa na kilogramu 300 zilizozalishwa mwaka 2016. Katika kipindi hicho, thamani ya dhahabu iliyouzwa iliingiza Sh bilioni 51.3 sawa na wastani wa Sh bilioni 1.7 kwa siku.

Katika mapato hayo, serikali ilipata tozo ya Sh bilioni 3.59 na halmashauri ilipata ushuru wa Sh milioni 153. Julai mwaka huu, thamani ya dhahabu iliyouzwa ilikuwa Sh bilioni 55.88 sawa na wastani wa Sh bilioni 1.86 kwa siku.

Serikali ilipata tozo ya Sh bilioni 3.9 na ushuru wa halmashauri ulikuwa Sh milioni 167. Mwezi Agosti , mauzo yalikuwa Sh bilioni 58.9 sawa na wastani wa Sh bilioni 1.9 kwa siku na tozo ya serikali ilikuwa Sh bilioni 4.12 huku ushuru wa halmashauri ulikuwa Sh milioni 176.

Alisema soko la madini la mkoa linaingiza Sh milioni 800 kwa mwaka na hivi karibuni kiasi hicho kitaongezeka na kufikia zaidi ya Sh bilioni 1.

“Kwa hiyo Geita si eneo dogo, ni eneo la kimkakati na sisi viongozi tunatakiwa kuhakikisha wananchi wanazidi kuelimika na kuwa wadau wakubwa katika kuchangia Pato la Taifa kwenye sekta ya madini, Geita tuna masoko tisa ya madini likiwemo soko kuu la madini Geita Mjini, lakini kila wilaya ina masoko, “ alisema Gabriel.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Geita, Modest Apolinary, alisema asilimia 60 ya mapato katika halmashauri hiyo imetumika katika kuboresha huduma za afya, elimu na ujenzi wa barabara.

Apolinary alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) vinavyoripoti Maonesho ya Tatu ya Kimataifa ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini.

Yalianza juzi na yatamalizika Septemba 27. Alisema katika kipindi cha mwaka 2015/2016, halmashauri ilikuwa ikikusanya Sh bilioni 2.5, lakini katika mwaka 2019/2020 imekusanya Sh bilioni 10 na asilimia 60 ya mapato hayo yametumika katika kuboresha huduma za jamii.

Mwaka 2016 kulikuwa na zahanati saba na sasa zimejengwa 22. Shule za msingi zilikuwa 47 na sasa zipo 61 baada ya kujengwa mpya 14. Shule za sekondari zilikuwa 10 na sasa zimeongezeka mpya saba na kufanya jumla ya shule 17.

“Mwaka 2016 kulikuwa na kilometa sita tu za barabara za lami, lakini kwa sasa tumejenga kilometa 20.3 za barabara za lami ili kuondoa vumbi,” alisema Apolinary.

Alisema zaidi ya asilimia 50 ya mapato yao yanatokana na dhahabu. Alisema halmashauri inataka ndani ya miaka mitatu ijayo ijitegemee, kwa kuongeza vyanzo vya mapato vitakavyowapatia fedha za kuendesha shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Halmashauri ya Mji pia inajenga machinjio ya kisasa katika eneo la Mpomvu na yamekamilika kwa asilimia 90. Machinjio hayo yaliyogharimu Sh bilioni 7.2, yatakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe kati ya 100 na 200 kwa siku na mbuzi zaidi ya 100 kwa siku.

Kuhusu maonesho, mkuu wa mkoa alisema maonesho hayo yanapaswa kuwatengeneza wajasiriamali na kuwajengea uwezo kumiliki uchumi wa madini na bidhaa, kama vile mboga na vyakula vinavyohitajika migodini.

MCHICHA ni aina nyingine za ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera, Geita

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi