loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

…Sitoi ahadi hewa

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ameendelea kuahidi mambo mbalimbali makubwa atakayoyetekeleza baada ya kuchaguliwa kipindi kingine, huku akisisitiza kuwa hatoi ahadi hewa.

Kama alivyoahidi katika mikoa mingine ambayo ameshapita kuomba kura kwa wananchi, akiwa katika Viwanja vya Lake Tanganyika mkoani Kigoma jana aliwaahidi mambo mbalimbali, ikiwamo kununua meli mbili kubwa zitakazofanya kazi kwenye Ziwa Tanganyika.

“Sitoi ahadi hewa. Meli moja itakuwa ya watu 600 na tani 400. Ya pili itabeba mizigo tu tani 4,000. Nataka watu mfanye biashara, nataka Kigoma niifungue, najua siku moja mtanikumbuka. Nasema kwa dhati na kwa uwazi haya nitayafanya,” alisisitiza.

Alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwaka 2015, imefanya mambo makubwa mengi ya maendeleo kwa mujibu wa Ilani ya CCM.

Alisema katika miaka mitano ijayo, kwa mujibu wa Ilani ya CCM, meli ya Mv Liemba itakarabatiwa na Sh bilioni 10 zimetengwa. Vile vile Mv Sangara itarabaratiwa na Sh bilioni sita zimetengwa kwa ajili hiyo.

Alisema sambamba na ujenzi wa meli, itajengwa ofisi kubwa ya bandari, jengo la abiria na ghala la kuhifadhia mizigo. Pia zitajengwa bandari mbili mkoani Rukwa, huku bandari ya Kigoma ikiwa ndiyo ofisi kuu ya kuhudumia bandari zote za Ziwa Tangayika.

Matapeli wa kisiasa

Rais Magufuli aliwataka Watanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi, kujiepusha na matapeli wa kisiasa wanaodai kuwa wamewaletea maendeleo wakati kazi kubwa imefanywa na serikali ya CCM.

“Tumemaliza uchaguzi wa mwaka 2015, tukabaki kufanya kazi kwa kutambua maendeleo hayana chama. Hapa Kigoma tumeendelea na mradi wa maji na uwekaji mifereji ya maji, taa barabarani na ujenzi wa dampo. Kigoma ni mashahidi inawezekana wapo wengine wakazungumza wameweka wao, lakini hapana, si kweli,” alisema.

Alisema, “Hata haya maendeleo mnayoyaona ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, mimi nafahamu fedha ilitoka wapi nawaeleza ukweli. Uboreshaji wa miundombinu tuliyofanya hapa Kigoma ni sehemu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya uendeshaji wa miji ya kimkakati na tuliuweka mji huu wa Kigoma kwenye miji ya kimkakati (TSCP) wenye kwenda ku-google waka-google,” alisema.

Alisema katika mradi huo wa TSCP, serikali imetekeleza kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa mkopo kutokana na ukweli kuwa Tanzania inakopesheka.

“Ukiwa na uwezo wa kukopa unakopeshwa. Tanzania tuna uwezo wa kukopa na aliyesaini mikataba ya mikopo ni Mpango (Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip). Mbunge au hata mimi siwezi kusaini kwa sababu wapo vijana wangu,” alisema.

Alisema mradi huo wote wenye kushirikisha mikoa nane ikiwamo Kigoma, umegharimu Sh bilioni 799.52. Mikoa mingine iliyonufaika ni Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Tanga, Mtwara na Mwanza.

“Nawaeleza haya mpate ukweli, ukisikia mtu anasema nimeleta huu mradi mimi maana yake na Mwanza, Tanga, Mtwara, Dodoma aliupelela yeye. Muanze kuchambua, msema kweli siku zote ni mpenzi wa Mungu,” alisema.

Aliwataka Watanzania wakiwamo wana Kigoma, kujiepusha na matapeli wa siasa, akisisitiza kwamba kwenye siasa wapo matapeli.

Alisema mradi huo ulishughulikiwa na serikali na ulikuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. “Maendeleo hayana chama, hapa Kigoma mradi huu umetumia Sh bilioni 31.19 ukajenga barabara za kilometa 15.13” alisema.

Utekelezaji Kigoma

Akizungumzia maendeleo yaliyofanywa mkoani Kigoma, alisema pamoja na ujenzi wa barabara, serikali imefufua zao la chikichi, ujenzi wa mifereji ya maji, miradi ya maji, kuweka taa za barabarani na ujenzi wa dampo.

Alisema serikali  imefanya maendeleo nchini kote. Alitoa mfano wa Dodoma ambako imejenga soko kuu la kisasa na stendi ya kisasa. Pia imeweka taa barabarani.

Kazi  hiyo imefanywa pia kwenye maeneo mengine ikiwamo Arusha na Chato. “Mkiona taa barabarani mtu asije akasimama akatafuta umaarufu, hapana” alisema.

Magufuli alisema serikali imepeleka jumla ya Sh bilioni 567 kwa ajili ya miradi ya barabara pekee, huku mojawapo  iliyojengwa ni ya kimataifa, kwa kuwa inauuganisha mkoa na nchi jirani .

“Nawaomba Kigoma sasa mkae mkao wa kula, kwa maana ya Kigoma sasa kuanza kutengeneza biashara. Dagaa za hapa zitaenda kuliwa Afrika Kusini na migebuka itaenda hadi Uganda,” alisema, huku akiwataka vijana kutumia fursa hiyo na kujipanga kwa ajili ya maendeleo.

Waziri Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi