loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hospitali ya Aga Khan yajivunia utoaji wa huduma bora

HOSPITALI ya Aga Khan inajivunia kwa kutekeleza sera, zilizofanikisha utoaji huduma za ubora wa hali ya juu za wagonjwa katika hospitali zake zote na vituo vya afya

Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk Ahmed Jusabani alisema hayo wakati akizungumzia siku ya kimataifa ya usalama wa wagonjwa duniani.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni ‘ Usalama wa Wafanyakazi wa Afya’ na kipaumbele chake ni usalama wa wagonjwa.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika hospitali hiyo, ambapo idara mbalimbali zilionesha kazi zao kuhusu usalama wa wafanyakazi, ambao pia ni usalama wa wagonjwa. Hospitali hiyo ina zaidi ya miaka 90 ya kutoa huduma bora za afya nchini.

Dk Jusabani alisema wakati wa ugonjwa wa covid-19, hospitali hiyo ililazimika kuchukua hatua kadhaa za ziada na msaada kuwakinga wafanyakazi, ikiwemo kuwa na mpango wa afya na bima maalumu kwa wafanyakazi wakati wa ugonjwa huo.

Hatua nyingine ni kutoa mafunzo kwa wafanyakazi kujiandaa kutibu wagonjwa wa covid-19 na kuwa na timu ya usaidizi wa kisaikolojia kukabiliana na matatizo ya kisaikolojia.

Pia walikuwa na mpango wa wafanyakazi kufanya kazi wakiwa nyumbani na pia walishirikiana na sekta za umma na binafsi kutoa vifaa vya kujikinga.

“Hospitali ya Aga Khan inaungana na WHO na wabia wengine wa kimataifa kuadhimisha mpango huo unaosaidia kutoa mwongozo wa mfumo wa utoaji tiba huku kukiwa na kipaumbele kwa usalama wa wafanyakazi na wagonjwa,” alisema.

Mkurugenzi wa wauguzi katika hospitali hiyo, Aika Mongi alisema ugonjwa wa Covid-19 umeonesha changamoto kubwa zinazowakabili wafanyakazi wa afya duniani kote.

Alisema ugonjwa huo umeonesha jinsi wafanyakazi wanavyokabiliwa na hatari ya kuambukizwa magonjwa, kutokana na kuuguza wagonjwa, kufanyiwa ukatili, ajali, unyanyapaa, magonjwa na vifo.

“Madhumuni ya maadhimisho ya mwaka huu ni kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa usalama wa wafanyakazi wa afya unavyohusiana na  usalama wa wagonjwa. Kuna haja ya kuwa na mazingira salama ya kufanya kazi kwa wafanyakazi wa afya,” alisema.

Siku ya kimataifa ya usalama wa wagonjwa duniani, chimbuko lake ni kanuni isemayo ‘Matibabu Kwanza, Usisababishe Madhara’.

Huadhimishwa Septemba 17 kila mwaka kwa lengo la kukuza ufahamu kuhusu usalama wa wagonjwa, kuongeza ushiriki wa wananchi katika kutibu wagonjwa na kukuza uelewa wa kimataifa wa usalama wa wagonjwa na kupunguza madhara kwa wagonjwa.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi