loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania ina chakula cha kutosha kwa sasa

SERIKALI imesema nchi ina chakula cha kutosha, lakini kuna uwezekano wa kutokea mvua kidogo msimu ujao. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya juzi alipofungua Kongamano la Pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao Baada ya Mavuno.

Kongamano hilo linafanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mkoani hapa. “Tunacho chakula cha kutosha hata mvua ikipungua kwa msimu ujao.

Serikali imejipanga kukabiliana na upungufu huo, hivyo wananchi endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kutunza chakula mlichonacho” alisema.

Alitoa rai kwa watanzania kutumia vizuri chakula kilichopo ili kukabili upungufu wa chakula kama utajitokeza. Kusaya alisema uzalishaji wa chakula nchini Tanzania, unatosheleza mahitaji ya taifa.

Alisema hali ya chakula mwaka huu ni nzuri kutokana na uzalishaji mzuri katika msimu wa 2019/2020. Tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya msimu wa 2019/2020, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajia kufikia tani 17,742,388 ambapo mahitaji ni tani 14, 347,955.

“Nchi inategemewa kuwa na ziada ya tani 3, 511,620 za chakula ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2, 072,413 ni za mazao yasiyo nafaka,” alisema.

Jitihada nyingine za serikali katika kuhakikisha nchi inakuwa na chakula za kutosha ni kuendelea kununua mazao ya nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Tayari tani 100,000 za mazao zimekwishanunuliwa ikiwemo mahindi na mpunga.

Kusaya alisema kuhusu suala la upotevu wa mazao, Wizara ya Kilimo imewashukuru wadau wa sekta ya kilimo kwa kuandaa kongamano hilo ili kujadili mikakati ya kudhibiti wa upotevu wa mazao baada ya mavuno ambao unaathiri uchumi wa wakulima.

Akizungumzia upotevu wa mazao baada ya mavuno nchini, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Kusimamia Udhibiti wa Mazao (TPMP), Julius Wambura alisema takwimu zinaonesha asilimia 30 hadi 35 ya mazao ya nafaka, hupotea wakati wa mavuno na baada ya kuvunwa shambani. “Jumla ya gunia tatu hadi 3.5 kati ya 10 zinapovunwa zinapotea shambani au baada ya kufikishwa ghalani, hali inayowatia umasikini wa kipato wakulima wetu na kuwapunguzia tija,” alisema Wambura.

Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda alisema upotevu wa mazao katika nchi za Afrika ni mwendelezo wa matatizo ambayo waliotawala waliyaacha na bado hayajapatiwa suluhisho .

Alikemea tabia ya watafiti wakiwemo kwenye vyuo vikuu, kutofanya tafiti za kusaidia wakulima kuondokana na tatizo la upotevu wa mazao, kwani vyuo vingi havifundishi wanafunzi kukabiliana na tatizo hilo Profesa Chibunda alitoa wito kwa mamlaka za udhibiti, kama TMDA, TBS na Polisi, kusaidia wakulima nchini kuwa na uhakika wa kusafirisha mazao yao na kupunguza vikwazo kwa wakulima ili mazao yasiharibike kabla hayajafika sokoni au ghalani.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wa kilimo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Wasio wa Kiserikali (ANSAF), Audax Rukonge alisema anaiomba serikali iendelee kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa teknolojia rahisi ya kuchakata na kuhifadhi mazao ili wakulima wapate faida, hali itakayosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.

MCHICHA ni aina nyingine za ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi