loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shule zinapojali faida kuliko usalama wa watoto

“ WANAFUNZI wawili wa kiume wanalala kitanda kimoja! Tena kitanda chenyewe ni cha futi mbili kwa sita!” ndivyo anavyosema Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya huku akistaajabu baada ya kutembelea shule moja wilayani humo.

Waswahili wanasema ukistaajabu ya Musa, utayaona ya firauni. Mshangao wa Sabaya hakuishia katika kitendo cha shule kulaza wanafunzi wawili kwenye kitanda kimoja tu, bali hata kitendo cha shule hiyo kutoa huduma za bweni kwa takribani miaka saba bila kuwa na kibali kutoka mamlaka zinazohusika.

Picha moja ya video iliyorushwa katika mtandao ilimwonesha Mkuu wa Wilaya Sabaya akihoji na kutaka kujua gharama wanazotozwa wanafunzi hao kwa huduma ya bweni.

Anaambiwa ni Sh 850,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka. Kana kwamba hiyo haitoshi, jicho lake linabaini kituko kingine katika shule hiyo kuwa, badala ya kuweka vitanda vya ghorofa moja maarufu ‘double decker’, ambavyo ndivyo vinaruhusiwa, imeamua kuweka vitanda vitatu kwa moja yaani ‘triple decker.’

Kimsingi, kitendo hicho pia kinatajwa kuhatarisha usalama na maisha ya wanafunzi, hususani wanaolala juu maana ikitokea sababu yoyote ikiwamo ndoto ya kutisha na kushituka au wakati wa kujigeuza na kudondoka, siyo siri yatakayosemwa ni mengine.

Mmoja wa watendaji, baada ya kuhojiwa na mkuu wa wilaya huyo kama amewahi kufanya ukaguzi mintarafu suala hilo, anakiri kutofanya hivyo lakini akakiri kwamba mtoto anayelala kitanda cha juu (ngazi ya tatu), ikitokea kwa sababu yoyote iwayo akaanguka, atapata madhara makubwa.

Inabainika kuwa hata kwa upande wa wanafunzi wa kike, milango ya mabafu yao inatazamana na uwanja wa mpira jambo linaloathiri ‘usiri’ wa watoto hao.

Hilo nalo linamshangaza Mkuu wa Wilaya Sabaya na watu wengine wanaoshuhudia hali hiyo. Watendaji wengine waliotakiwa kueleza kama wanafahamu changamoto zilizopo shuleni hapo na namna walivyozishughulikia, ni pamoja na Ofisa Elimu Kata pamoja na wadhibiti ubora.

Majibu na utetezi wao, hayaingii akilini wala kumridhisha mkuu wa wilaya. Mambo hayo yanamfanya Sabaya azidi kuhoji sababu za watendaji hao kutobaini matatizo katika shule hiyo kwa miaka saba tangu iwepo.

Anahoji sababu za shule hiyo kusajiliwa lakini kwa kuficha utambulisho kuwa ni ya bweni. “Miaka saba hakuna mtu aliyeona,” alihoji na kuagiza, “mratibu wa elimu (ofisa elimu kata), mkurugenzi, nataka mambo haya yarekebishwe haraka.”

Mkuu wa shule anakiri kwamba shule ina wanafunzi 176 na ilianza kulaza wanafunzi mwaka 2013. Kwa upande wa bweni kuwa na vitanda vya ngazi tatu, Sabaya alishutumu wadhibiti ubora wa elimu akisema, ni mahiri kufuatilia mambo binafsi, lakini jambo kubwa kama hilo hawafuatilii.

Alihoji sababu za kutochukua hatua wanaposhauri jambo fulani lirekebishwe, lakini lisifanyiwe utekelezaji. Ndiyo maana DC Sabaya anawaambia, “lazima mheshimike kama serikali, mnaagiza jambo lisitekelezwe, lazima mchukue hatua.”

Baada ya yote hayo kubainika, mmiliki wa shule aliomba radhi akiahidi kufanyia kazi upungufu huo. Hata hivyo mkuu wa wilaya alisema hawezi kukubali wanafunzi wa kiume kuchangia kulala kitanda kimoja.

Alitoa saa 24 kwa uongozi wa shule kuhakikisha kila mwanafunzi analala katika kitanda peke yake akisisitiza kitendo cha kulala wawili si sahihi na si maadili.

Alitoa siku 30 kwa uongozi kuhakikisha shule inapata kibali cha kulaza wanafunzi na akaitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia masuala yote ya kodi.

Alibainisha kuwa kama uongozi ulikuwa ukichukua ada ya Sh 850,000 wakati wamesajiliwa kama shule ya kutwa, ni dhahiri kuna kasoro za kikodi. Ziara hii ya mkuu wa wilaya na ‘madudu’ aliyobaini, inaacha maswali mengi kuhusu hatma ya watoto kitaaluma, kisaikolojia, kiafya na kiusalama wawapo shuleni na hususani, shule za bweni.

Tukio hilo linadhihirisha kuwapo tatizo miongoni mwa wasimamizi wa elimu hususani upande wa shule za binafsi. Linaweka wazi kwamba yapo madudu mengi yanayofumbiwa macho katika baadhi ya shule.

Inawezekana mamlaka za usimamizi hazioni kasoro hizi ama kwa uzembe au makusudi kwa maslahi yao binafsi. Siyo siri, wapo baadhi ya watendaji ambao ni wazembe, wanaofanya kazi kwa mazoea huku wakijikita kuangalia maslahi binafsi.

Wengi wa hao, wamejikita kukaa ofisini na ‘kupika’ taarifa licha ya majukumu yao kuwataka wawe karibu na wadau, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa uendeshaji shule mbalimbali kubaini dosari zinazojitokeza kwa manufaa ya umma.

Wapo watendaji ambao inawezekana kasoro hizi wanaziona lakini ‘wanafungwa midomo’ na wamiliki wa shule wanaotanguliza faida nono, bila kujali usalama na mustakabali wa watoto kitaaluma.

Tukio hili na mengine yanayoripotiwa kutokea katika sehemu mbalimbali nchini yawafungue macho wazazi, walezi na serikali kuhusu hali ilivyo katika shule wanazopeleka watoto wao bila kujali ni za bweni au kutwa.

Licha ya kasoro zilizobainishwa na mkuu wa wilaya katika shule hiyo, yapo mambo mengine mengi yanayofanyika shuleni yenye athari za kisaikolojia, kiafya na kimwili ikiwamo watoto kulishwa chakula kibovu, adhabu kali kupindukia, kujazana kwenye mabasi yasiyo na waangalizi, kuwapo walezi wa mabweni wasiokidhi vigezo na hata uchafu wa vyoo.

Upo umuhimu wa wadau mbalimbali wakiwamo wazazi na walezi kufika katika shule au kuzungumza na watoto juu ya mazingira waliyomo kubaini changamoto zinazowakumba kutokana na baadhi ya wamiliki kuangalia faida kuliko usalama wa watoto.

Wadau wasisubiri kuweka wazi kasoro hizi baada ya kuwapo matokeo hasi, bali zibainishwe na kufikishwa kwenye mamlaka za uamuzi zifanyiwe kazi kwa uaminifu.

Waswahili wanasema, ‘Kinga ni bora kuliko tiba’.

KATIKA kipindi cha miezi michache iliypopita, dunia ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi