loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wagombea wachochezi wadhibitiwe

KAMPENI za uchaguzi kwa ajili ya kupata viongozi katika ngazi ya urais,wabunge na madiwani zinaendelea nchini, kwa wagombea wa vyama mbalimbali wakitangaza sera zao huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kuhakikisha wanafanya uamuzi sahihi ifikapo Oktoba 28,mwaka huu.

Ikiwa zimebakia chache za kufanya kampeni, ni lazima vyama vyote kuhakikisha vinasiamamia sheria na taratibu katika kutangaza sera zao na kamwe visijikite katika kutoa lugha zisizofaa kwa vyama au wagombea wengine, jambo linaloweza kutishia amani ya nchi wakati huu muhimu katika nchi ya kidemokrasia.

Katika kuonesha kukerwa na baadhi ya wagombea, wagombea urais  watano wa nafasi ya urais wanaoviwakilisha vyama mbalimbali, walijitokeza na kukemea lugha za uvunjifu wa amani, zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa katika mikutano mbalimbali ya kampeni inayoendelea nchi nzima.

Wagombea hao waliojitokeza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ni Queen Sendiga kutoka Chama cha Alliance Democratic (ADC), Mutamwega Mgaywa wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Philipo Fumbo Chama cha Democratic (DP), Said Maalim Seif kutoka Chama cha Wakulima (AAFP) na Cecilia Mwanga wa Chama cha Demokrasia Makini.

Kwa pamoja, wagombea hao wamedai hawaridhishwi na uendeshwaji wa kampeni, unaofanywa na baadhi ya vyama na wagombea wao wa nafasi mbalimbali, kutokana na kujaa lugha nyingi zinazoashiria umwagaji wa damu. Walisema hawakutarajia suala hilo katika kampeni hizi zinazoendelea.

Kwa pamoja waliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya ulinzi na usalama, kuongeza umakini katika kipindi hiki kwa kuwafuatilia wanasiasa wote na vyama vya siasa vinavyotoa kauli hizo.

Hakika, wagombea hao wameonesha ukomavu wa kisiasa na mapenzi kwa nchi, kwa kuacha shughuli zao za kampeni na kuungana kutoa tahadhari kwa suala hili muhimu kwa taifa.

Hivyo, kuna kila sababu kwa NEC kuangalia sheria na kuwadhibiti wagombea wote wanaochochea chuki na vyama wanavyotoka.

Ni dhahiri kuwa wagombea wanaoshindwa kueleza sera zao na kuchochea chuki na ugomvi, hawana nia njema na hivyo hawana nafasi katika kushika madaraka.

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi